KWA mtu anayetoka katika Taifa lenye serikali inayojali au kuthamini wananchi wke na nguvu kazi yao vilivyo ni vigumu kwake kuamini kuwa zipo familia za wanadamu zenye mkusanyiko wa zaidi ya watu kumi wanaoponea si zaidi ya shilingi 800 kw siku katika ardhi hii ya Mwenyezi Mungu. Mwandishi MUSSA ALLY wa Morogoro anaelezea zaidi katika sehemu hii ya tatu.
TANGU mwaka 1988 hadi hivi sasa hakuna matumaini yoyote ya mabadiliko ya haraka katika maeneo yote yanyohusiana na mifugo pamoja na ufugaji kwa ujumla wake, ikiwa ni pamoja na ongezeko la idadi ya wafugaji na mazao yake kama vile nyama, ngozi, mayai na maziwa, wala hakuna ubunifu wowote wa kutumia mazao mengine ya mifugo kama kwato, pembe na mifupa ili kututumua uchumi wa mkoa kupitia sekta hiyo adhimu.
Aidha, hakuna matumaini yoyote ya mabadiliko makubwa katika wastani wa matumizi ya nyama, mayai na maziwa katika kuboresha afya za wakazi wa Morogoro ambao ni sehemu ya nguvu kazi muhimu ya uchumi wa mkoa na taifa kiujumla.
Ushahidi wa hilo tunapata katika taarifa ya mwaka 1988 ya maendeleo ya mkoa huo kitakwimu (Vol. 2) iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inaonesha wazi kuwa idadi ya mifugo iliyochinjwa na mkoa wa Morogoro ilikuwa zaidi ya 11,986 (ng'ombe 11,020, mbuzi 800, kondoo 79 na wanyama wengineo 87).
Hivyo zikapatikana tani 3,00 za nyama na vipande 20,572 vya ngozi, huku maziwa ya ng'ombe yakiwa ni lita zaidi ya 1,080,958 na dazeni 426,424 za mayai ya kuku.
Lakini kiwango cha matumizi (ulaji) kwa wastani kwa mtu wa Morogoro mmoja kinasikitisha.
Viwanda na Biashara
Endapo utazungumzia viwanda mkoa wa Morogoro, basi mawazo yako yote yaelekekze katika "Nyundo" za mafundi majiko ya mkaa, mabanda ya mafundi koroboi, vigenge vya mafundi chuma na kadhalika.
Kwa mujibu wa mamlaka husika, Morogoro ina "viwanda" vidogo zaidi ya 40 ambavyo ndio msingi wa viwanda vikubwa vikubwa zaidi ya 15, vingi kati ya hivyo vikiendeshwa kwa kusuasua na karibu vyote viko nyuma ya karne ya 21 ya sayansi na teknolojia.
Unapozungumzia biashara elekeza mawazo yako kwa mama ntilie na wamachinga wanaoishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao.
Tunapoanza kutupia macho sekta ya viwanda kwa kifupi sana, hususan vile tunavyoviita kuwa ni "viwanda" vikubwa, kama vile kiwanda cha Maturubai (Morogoro Canvas Mill), kiwanda cha Mabegi, magunia, mazulia Kilosa, viatu (T & T Shoe Co), Nguo (Polytex/Polyster), Mbegu (TANSEED), Ngozi, Sukari Mtibwa na Kilombero, bidhaa za ngozi (Tanzania Lather goods) na kadhalika tunapata picha nyingi ya kuhuzunisha.
Picha hiyo ya kuhuzunisha ni na baadhi ya viwanda hivyo kufa au kusimamisha uzalishaji, pia hali mbaya ya wafanyakazi wake, wengi wao hawana hata mikataba halisi na halali ya kazi kama sheria za kazi zinavyoainisha, hawana bima, vitendea kazi vifaavyo wala mishahara inayooana na kazi ngumu kabisa wazifanyazo.
Sura ya wafanyakazi hao niionavyo mbele ya waajiri wao ni ile ile ya "watumwa" mbele ya "mabwana". Mfanyakazi wa ngazi ya chini na mara nyingine hata ile ya kati huingia kazini (hasa katika viwanda vingi vya binafsi) mapema alfajiri na muda wa kutoka huwa ni kitendawili.
Mshahara wa mfanyakazi huyo ni mdogo sana kiasi cha shilingi 17,500 na 35,000 kwa mwezi!
Wakati wafanyakazi wa ngazi za juu (aghalabu huwa ni washirika wa karibu na wenye viwanda husika kwa mahusiano ya kidini, kirafiki, rangi, kabila na kadhalika) hulipwa malaki kwa mwezi! Si tu mshahara bali na marupurupu juu!! Je, uwiano wa mshahara kati ya kima cha juu na kile cha chini (KCC) unaswihi? Je, vyama vya wafanyakazi na serikali havioni au viko likizo? Na kama hivyo ndivyo, likizo hiyo isiyo rasmi itakwisha lini? Wafanyakazi wenyewe ambao ndio wahanga wa kadhia hii wana majibu yafaayo.
Wafanyakazi hao ambao ndiyo chachu ya kunawirisha viwanda hivyo na wamiliki wake kama si kuchangia ukuwaji wa uchumi wa Taifa endapo hali zao ni hizi, sekta ya viwanda itanawiri au kusuasua?
Tukirejea katika hali ya uzalishaji kwenye viwanda hivyo bado si ya kuridhisha sana, na baadhi ya viwanda hivyo bidhaa zake si nzuri sana ukiziweka katika mizania ya viwango vya kimataifa.
Hebu jaribu kuangalia uwezo wa uzalishaji wa viwanda vifuatavyo tangu mwaka 1985, na kisha jiulize je, kuna mabadiliko yoyote ya uzalishaji (kuongezeka au kupungua) katika baadhi ya viwanda hivyo vifanyavyo kazi hadi hivi leo?
Kiwanda cha Mazulia Kilosa uzalishaji wake kwa mwaka ulikuwa tani mbili kwa siku, kiwanda cha mbao Mang'ula kilizalisha kiubiki mita (Cubic Metres) 20,000 za mbao kwa mwaka.
Mtibwa nao walizalisha tani 35,000 za sukari
kwa mwaka, Kilombero (K 1) kikizalisha sukari tani 40,000 kwa mwaka, huku
Kilombero (K 2) kikitoa tani 45,000 za bidhaa hiyo kwa mwaka nyakati hizo.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |