Ni vigumu kuamini Kamanda Upelelezi Moro ataka:
Wachapishaji Qur'an wafikishwe mahakamani
HUENDA ikawa vigumu kuaminika, lakini ndivyo ilivyotokea, Mkuu wa polisi upepelezi mkoa wa Morogoro(RCO), Steven Ngowi ametaka walioandika Qur'an, wachapishaji na wauzaji wake wakamatwe na kufikishwa makamani. Amedai hatua hiyo inachukuliwa kwa kuwa kitabu hicho kinakashifu imani za wengine.

Afisa huyo aliyasema hayo wiki iliyopita wakati akitoa ushahidi katika mahakama ya hakimu mkazi mjini hapa katika kesi ya kufanya mhadhara bila ya kibali inayowakabili wahubiri wa kikundi cha ALMALLID tawi la Morogoro.

Bwana Ngowi ambaye aliieleza mahakama hiyo kuwa alikuwa akitoa ushahidi kama mmoja kati ya wakristo wanaokerwa na kashfa za kikundi hicho na vile vile kama kiongozi wa chombo cha Dola mkoani, alisema alisikia kwa masikio yake wahubiri hao wakisema Yesu sio Mungu jambo ambalo alidai linaumiza imani za watu wengine akiwemo yeye.

Kwa mujibu wa Uislamu Qur'an iliteremshwa kwa mtume Muhammad (s.a.w) kwa njia ya Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia Malaika Jibril(a.s).

Kutokana na mafundisho hayo ya Uislamu dai la RCO Ngowi kutaka walioandika Qur'an wafikishwe mahakamani ina maanisha kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad (s.a.w) wakamatwe ili wapandishwe kizimbani kujibu shitaka la kukashifu watu wengine.

Kauli ya kutaka wasomaji wa Msahafu(Qur'an), wauzaji na wachapishaji wa kitabu hicho wakamatwe ilikuja baada ya wahadhiri kuthibitisha kwamba kauli ya kuukana uungu wa Yesu siyo yao bali ni ya Mwenyezi Mungu.

Walipotakiwa kuonesha kauli hizo katika Qur'an wahubiri hao walisoma sura ya 5 aya 72, aya hiyo inasomeka "Bila shaka wamekufuru wale waliosema, Hakika Mwenyezi Mungu ni Masihi Bin Maryamu. Masihi(Yesu) alisema: Enyi wana Israel mwabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu na Mola wenu.

Aya inaendelea kufafanua kuwa "Kwa yakini anayemshirikisha Mwenyezi Mungu ameharamishiwa Pepo na mahali pake ni Motoni na madhalimu hawatakuwa na wasaidizi".

Baada ya kusomwa aya hiyo Hakimu anayesikiliza kesi hiyo Bwana Mganya akadakia na kusema kwamba hakuna ushahidi kuwa Qur'an ni kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Hoja ya Hakimu ilimchochea RCO ambaye alidai kuwa kwa mujibu wa sheria, yule anayesoma maandiko hayo, muuzaji, aliyeandika na mpiga chapa wanatakiwa wanatakiwa na kushitakiwa.

Wahubiri hao walipohoji mbona wahusika hao(waandishi wa Qur'an) hawajakamatwa, afisa huyo wa upelelezi alisema, kwa kuwa wahubiri hao wameshakamatwa, ni wao watakaowajibika kuwaonesha waandishi na wauzaji wa Qur'an ili hatimaye nao wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa Chaurembo A. Chaurembo, Mohammed Hilali, Athumani Mataula na Awadhi Mlongachaka walifanya Mhadhara Bila ya Kibali katika Viwanja vya Shule Msingi Kichangani mwezi Julai mwaka jana jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya Jamhuri ya Muungano.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi mbili ambazo ni kutoa maneno ya kashfa dhidi ya waumini wengine na kufanya mhadhara bila ya kibali.

Kesi ya kashfa itatajwa tena Jumatatu Aprili 3 mwaka huu ambapo ile ya kufanya mhadhara bila ya kibali itakuwa Aprili 16 mwaka huu.

Waislamu wa mkoa wa morogoro wamewataka Waislamu wote kufika mahakamani tarehe hizo ili kushuhudia hatima ya kesi hizo za aina yake.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook