Lipumba asema, chini ya sera za CCM:
Wananchi wanabanwa wageni wakitanua


'MAKABURU' walionunua NBC kwa bei ya bure, hivi sasa wanajigamba kuwa wameacha wake zao ili kuja kuwasaidia Watanzania maskini.

Aidha, serikali imekuwa ikiwabana Watanzania walipe kodi wakati huo huo ikiyasamehe makampuni ya nje kulipa kodi.

Profesa Lipumba aliuambia umati mkubwa wa wananchi uliohudhuria mkutano wa hadhara wa chama chake uliofanyika Jangwani Jumapili iliyopita.

Alisema, mali za nchi zinauzwa kwa wageni, viongozi hawajali hali ngumu inayowakabili raia, katika mazingira hayo wananchi hawana budi kutumia kikamilifu demokrasia kuwaondoa madarakani.

"Hata wakoloni, kina Karl Peters hawakuja na wake zao walipokuja kututawala, hawana huruma yoyote kwetu, lakini viongozi wetu hawaoni hilo", alisema Profesa Lipumba.

Amesema, makampui ya nje ya madini, hulipa serikali shilingi 2400 tu katika kila mauzo ya dhahabu ya thamani ya shilingi 80,000.

Ameeleza, mbali ya kulipa kodi ndogo ya

machimbo, makampuni hayo hupewa pia misamaha ya kodi.

"...hata mashirika ya kimataifa yanatushangaa jinsi tunavyotoa misamaha ya kodi kwa makampuni makubwa", amesema na kuongeza "... ajabu zaidi TRA (Mamlaka ya Kodi) inawabana wafanyabiashara wa hapa nchini...".

Kuhusu NBC, Prof. Lipumba amesema, CCM imekiuka ilani yake ya uchaguzi kwa kuiuza benki hiyo.

Amesema, ilani ya uchaguzi ya CCM ya 1995 iliahidi kutoyauza mabenki makubwa ya serikali.

Akielezea hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili wananchi, Mwenyekiti huyo wa CUF ambaye kabla ya mkutano huo alikuwa wilayani Handeni, Tanga, alisema, ameshuhudia shule ikiwa na mwalimu mmoja, wanafunzi wote hawana viatu, mwalimu akiwa amevaa kandambili.

Huku akisikilizwa kwa utulivu mkubwa, Profesa Lipumba aliongeza kusema kuwa aliwaona akinamama wauza mboga mboga za majani wakitozwa ushuru mkubwa kuliko mapato yao.

"Wanauza mafungu mzigo ya msusa na matembele kwa shilingi 10 tu na mpaka saa nane mchana zilikuwa hazijanunuliwa, wakati huo mboga hizo zilikuwa zimeanza kunyauka", alieleza kwa masikitiko.

Katika mazingira hayo magumu ya biashara ambayo huifanyia chini ya mti, Profesa Lipumba alisema akina mama hao hulazimika kulipa ushuru wa soko shilingi 100.

Kuhusu hali ya kisiasa, alisema, Afrika imekumbwa na wimbi la kutaka mabadiliko, hali inayovitisha vyama tawala.

Kwa sababu hiyo, alisema, ndiyo maana hapa nchini kulifanyika mabadiliko ya 13 ya katiba ya Muungano wa Tanzania ili kumpa fursa mgombea wa chama tawala aendelee kutawala.

"Mabadiliko ya katiba ni kielelezo kuwa mgombea huyo hakubaliki, hawezi kupata asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa", alisema.

Aidha, matokeo ya uchaguzi wa Senegal, Profesa Lipumba alisema yamezidi kuongeza hofu inayowafanya viongozi walioko madarakani wazidi kuhamanika.

Aliitahadharisha CCM kutokujaribu kufanya vitendo vinavyoweza kusababisha kuvurugika kwa amani.

"Hatukubali kuibiwa kura, nguvu ya wananchi itatumika", alisema.

Awali katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Bwana Wilfred Rwakatare aliitaka CCM ikubali kukaa kando ili iangalie wengine wana kiwango gani cha kufikiri.

Alidai jitihada ya "kukifitini" chama cha CUF zimeshindwa baada ya wananchi kupuuza propaganda.

"Kwanza kiliitwa chama cha Wapemba, halafu kikaitwa chama cha Waislamu, baadaye kiliitwa chama cha Wanyamwezi na Wasukuma wakiwemo Wahaya, wakitoka hapo watakiita rasmi chama cha wananchi", alisema Katibu huyo huku akishangiliwa.

Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotazamiwa kuwa na upinzani mkubwa kati ya vyama vya CUF na CCM utafanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook