Mkuu wa Wilaya atuhumiwa kutaka kuzuia Itikaf


UONGOZI wa msikiti wa Irshaad Nyamanoro mjini Mwanza, umemtuhumu mkuu wa Wilaya kutaka kuzuia Itikaf iliyopangwa kufanyika msikitini hapo jumamosi iliyopita.

Katibu wa Msikiti huo amedai kupokea maagizo ya kuzuia Itikaf hiyo kupitia kwa dereva wa DC, Bwana Juma Sazia.

Katibu huyo amedai kuwa dreva na mtu mwingine aliyesemekana ni afisa usalama, walimuomba azuie Itikaf hiyo kwa sababu za kiusalama.

Hata hivyo dreva huyo hakuwa na maagizo ya maandishi bali magizo ya mdomo aliyodai kupewa na DC huyo.

Imedaiwa kuwa sababu za kuzuia Itikaf hiyo zilitokana na vyombo vya usalama kudai kuwa na taarifa ya matamshi ya uchochezi ambayo yametolewa na wahadhiri.

Maofisa wa vyombo hivyo wamedai matamshi hayo yalisababisha kuvurugika kwa amani hivyo wale wote ambao wangehudhuria eneo hilo wangekamatwa.

Pamoja na vitisho hivyo vinavyodaiwa kutolewa na vyombo vya dola, waumini walifurika kwa wingi msikitini hapo tayari kuendelea na Itikaf.

Waumini hao walishikilia kuwa wao wako Msikitini hivyo wasingekuwa tayari kumsikiliza yeyote hata akiwa kiongozi wa juu kabisa wa nchi au hata jini.

Mwandishi alishuhudia kufanyika kwa Itikaf hiyo huku waumini wakiwa wamefurika kwa wingi msikitini hapo.

Wakati huohuo, kesi inayowakabili Waislamu 10 mjini hapa itaanza kusikilizwa leo Ijumaa, Machi 31, 2000 mbele ya hakimu mkazi Machila Mang'ina.

Ilipotajwa kwa mara ya mwisho kesi hiyo Na. 164/2000 mwendesha mashitaka aliiambia mahakama kuwa upelelezi ulikuwa umekwisha kamilika.

Wakili anayetetea washitakiwa hao ni bwana Taslima wa jijini Dar es Salaam.


Shida ya maji Dodoma yawapatia watu ajira

SHIDA ya maji iliyodumu kwa miaka kadhaa katika baadhi ya maeneo ya mji wa Dodoma, imeleta nafuu kwa baadhi ya watu kujipatia ajira. Hata hivyo kwa wengine ni machungu ya kununua maji kila siku huku wakiwa wanayo mabomba ya maji ndani.

Katika maeneo ya Nkuhungu Juu (Mwishoni), Chang'ombe juu, Mbwanga Hazina ya Magereza, na Chadulu A na B, tatizo hilo limezoeleka kuwa ni la kawaida.

Pamoja na kuwa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kuwa na mabomba ndani, lakini mabomba hayo hayajawahi kutoa maji licha ya kuyalipia bili kila mwezi.

Mkazi mmoja wa eneo la Nkuhungu juu, Bwana Bakari alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa kiwango cha chini cha mtu mwenye familia ya watu wachache kwa mwezi atatumia zaidi ya shilingi 12,000 kununulia maji yanayotembezwa kwa mkokoteni.

Dumu (debe) moja la maji huuzwa kati ya shilingi 70 na 100 au zaidi ya hapo kutegemea umbali yanakopatikana maji hayo.

Aidha, baadhi ya maeneo hayana huduma za afya ukiachilia vituo vidogo vya watu binafsi na maduka ya madawa. Eneo kama Nkuhungu ni zaidi ya kilometa tatu kuweza kufika hospitali ya mkoa ili mwananchi asiye na uwezo apate huduma kwa gharama ndogo.

Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mwaka 1995 miongoni mwa ahadi walizozitoa wagombea walipofika maeneo hayo ilikuwa ni kuwaondolea kero au adha ya maji wakazi wa eneo hilo.

Katika Ilani ya Chama Tawala, CCM, iliwahakikishia wananchi kupitia serikali kuwa ifikapo mwaka 2000 serikali itakuwa imewapatia wananchi wake maji safi na salama, na kuboresha huduma za afya. Hali hiyo imebadilika na wananchi wamebebeshwa mzigo huo kwa nembo ya hali mbaya ya uchumi.


Amani na dhulma haviendi pamoja - Sheikh Zuberi

IMAMU Mkuu wa Masjid Sunni (Nunge) mjini Dodoma, Sheikh Ahmed Zuberi amesema misingi mibovu ya utawala haiwezi kusimamisha haki.

Amesema amani katika jamii haiwezi kuwepo mpaka watu wapate haki zao za msingi bila ya urasimu na kucheleweshewa.

Akitoa hotuba yake baada ya swala ya Ijumaa hivi karibuni, Sheikh Zuberi aliwataka Waislamu washikamane na elimu na wajiepushe na makundi ya watu wanaodai haki ambazo haziendani kimaumbile.

Alisema haki za usawa za jamii ziko wazi katika Uislamu na hazimdhalilishi yeyote yule.

Wakati huo huo, Waislamu wametakiwa kujitoa muhanga katika kusimamisha dini ya Allah (s.w.) kama vile alivyofanya Nabii Ibrahim (a.s.).

Akitilia mkazo kwa hadithi ya Mtume (s.a.w.), Sheikh Saidi amesema ibada zetu pamoja na dua haziwezi kukubaliwa iwapowatu wataendelea kula, kunywa na kuvaa kwa chumo linalopatikana kwa njia ya haramu.

Hata hivyo amesema, suala la kupatikana riziki ya halali haliwezi kupatikana katika nchi zenye mifumo ya maisha ya kitwaghuti.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook