KUTOKANA na ile ari yao ya kutafuta uhakika wa mambo kwa kufuata taratibu za kuthibitisha ukweli wa masuala ya elimu za aina mbalimbali; wanasayansi huwa kama watu wenye ushirikiano wa pekee. Umoja huu hujibainisha katika lugha wanayotumia ili kunatisha na kuhifadhi vitu walivyovibainisha katika utafiti wao. Ili kuimarisha umoja huu wanasayansi wamejenga taratibu nzuri ya kusanifu lugha zao kwa ajili ya mawasiliano (Kiputiputi; 1999:112). Kuna kanuni kadhaa ambazo kwa kawaida hupendekezwa na taasisi mbalimbali za kimataifa kama vile Shirika la Viwango la Ulimwengu, yaani International Standards Organization (ISO).
ZIFUATAZO ni baadhi tu ya kanuni ambazo ni lazima waalimu na waandishi wa sayansi wazifuate hata wanapoandika maudhui ya sayansi kwa Kiswahili.
Alama
Alama hutumika sana kuwakilisha dhana, viasi na vizio mbalimbali katika maandishi. Kwa mfano, kani hufafanuliwa kuwa,
kile kinachoweza kubadili hali ya mwendo ya gimba.
Lakini kwa kutumia alama, kani huweza kufafanuliwa kwa ufupi na kuwa,
F= ma
ambapo F ni kani, m ni masi na a ni mchapuo.
Ufafanuzi huu wa kihisabati, licha ya kuwa fasaha zaidi kuliko ule wa maneno matupu, unatoa uhusiano wa kihisabati kati ya kani yenyewe, masi ya gimba ambalo hukabiliwa na kani hiyo na mchapuko, ambao ni kina cha badiliko la mwendo wa gimba hilo. Kwa mfano, endapo kani yenye ukubwa wa 10 N itakabili gimba lenye masi 2 kg, basi gimba litapata mchapuko wa 20 m s-2 , yaani gimba hilo litabadili mwendo wake katika kima cha 20 m s-2.
Mfano mwingine mwepesi ni uhusiano kati kasi awali kasi tamati na muda na masafa ya gimba liendalo katika mwendo sare, unaelezwa kwa ufasaha zaidi na milingano ya mwendo ya galileo Galilei kama ifuatavyo;
v = u + at
s = ut + 1at2
v2 = u2 + 2as
Ambapo, u ni kasi awali, v ni kasi tamati, t muda, na s masafa.
Bila shaka, mwanafunzi aliyejifunza fizikia kwa Kiswahili akisoma kitabu cha fizikia kilichoandikwa kwa lugha nyingine kama vile Kiingereza hatapata taabu kuelewa maudhui yanayozungumzwa mara atakapokutana na milinganyo hii. Hali kadhalika kwa mwanafunzi aliyejifunza fizikia kwa Kiingereza atakaposoma kitabu cha fizikia kilichoandikwa kwa Kiswahili.
Hata hivyo, utafiti mdogo nilioufanya juu ya maandishi ya sayansi hususan vitabu vya sayansi kwa shule za msingi, alama hizi hazikuzingatiwa vilivyo. Kwa mfano, kwa vile, kwa Kiswahili neno sentimita linaanza kwa herufi s, vitabu vingi vinatumia alama ya sentimita kuwa sm. Hii sio sahihi. Kwa mujibu wa kanuni za kimataifa, alama ya senti ni c, kwa lugha zote hata kwa Kiswahili, kwa hiyo kifupisho cha sentimita ni cm na sio sm. Kwa vile s ni alama ya sekunde, sm itamaanisha sekunde mita, ambayo ni tofauti na maana inayokusudiwa.
Aidha, wakati mwingine waandishi hawatofautishi kati ya herufi kubwa na herufi ndogo. Kwa mfano, alama ya kizio nyumbufu za masi, kilogramu ni kg, yaani k ndogo na g ndogo. Lakini bila shaka wengi mtakuwa umeshaona moja kati ya alama hizi Kg, Kgs, KGS zikitumika kuwakilisha kilogramu, kwa mujibu wa jedwahili 1 na 2, Kg itaamaanisha kelvini gramu, KG ina maanisha kelvin giga, ambapo KGS ina maanisha kelvin giga siemeni.
Kuandika Kiasi kwa Kutumia Alama na Namba
Pia kuna kanuni inayotawala namna ya kuandika kasi kwa kutumia namba pamoja na kizio. Kanuni hii inasema kuwa wakati wote namba ianze ikifuatiwa na kizio. Kwa mfano kilogramu ishirini inapoandikwa kwa namba na kizio inatakiwa iandikwe 20 kg na sio kg 20 na kadhalika.
Hitimisho
Katika makala hii tumeona kuwa matumizi ya Kiingereza kufundishia sekondari na elimu ya juu nchini Tanzania huwafanya walengwa wasielewe wanachofundishwa. Matokeo yake ni kushuka kwa kiwango cha elimu. Hali imekuwa mbaya zaidi katika elimu ya sayansi na teknolojia kwa vile wahitimu hushindwa kuwa wabunifu na watundu wa kutumia elimu waliyoipata mashuleni kwa maendeleo ya taifa hili.
Aidha, tumeona kuwa kumekuwepo vikwazo vingi vilivyosababisha kuyumba kwa sera ya lugha nchini, moja ya sababu iliyochangia ni ubishi wa wasomi wetu ambao wenye ujuzi mkubwa katika taaluma zao lakini hawana ujuzi juu ya masuala ya lugha na elimu.
Kwa bahati nzuri mawazo yao yanafanana sana na ya wasomi wa nchi nyingine zilizoendelea kama vile Kiingereza waliopinga Kiingereza kisichukue nafasi ya Kilatini kama lugha ya kufundishia au wasomi wa Kijerumani waliopinga Kijerumani kisichukue nafasi ya Kifaransa kama lugha ya kufundishia.
Lakini kwa bahati nzuri wataalamu wasiopenda lugha zao walishindwa huko Uingereza na huko Ujurumani. Walishindwa pia huko India na nchi nyinginezo ambazo ni pamoja na China, Japan, Korea na kadhalika. Ni matumaini yetu kuwa wasomi wenye kupinga maendeleo ya Kiswahili kwa sababu ya kwenda na mazoea ua kwa kutokujua nao pia watashindwa na historia haitawasahau kamwe.
Ni muhimu tukajikumbusha kuwa tumo vitani. Vita hivi vinapiganwa katika medani ya kitamaduni ambayo mhimili wake mkuu ni Kiswahili. Historia ya nchi hii inadhihirisha namna kilivyotumika kama silaha kubwa, kama vile kuleta uhuru na umoja wa kitaifa. Sasa basi huu ni wakati muafaka wa kukienzi Kiswahili na kukipa ile dhima muhimu ya kulela maendeleo ya sayansi na teknolojia, yaani kukifanya lugha ya taaluma kwa ngazi zote za elimu nchini.
Namalizia kwa kusema kuwa ni matumaini yangu kuwa uamizi wa sasa wa kukifanya Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia sekondari, kuanzia mwaka 2001, kama ulivyoamuliwa hivi karibuni na Wizara ya Elimu na Utamaduni, utatekelezwa bila kusita.
Hata hivyo, ni muhimu kwa vyombo vinavyohusika kufanya matayarisho muhimu, kama vile kuandaa semina kwa walimu, kwani si sahihi kuamini kuwa kwa vile walimu wengi wanafahamu Kiswahili, basi wanaweza kufundisha kwa Kiswahili. Watunzi wanahtaji kuhamasishwa ili waanze kuandika vitabu vya taaluma zao kwa Kiswahili. Wachapishaji nao wanahitaji msukumo ili waanze kufikiria uwezekano wa kuchapa vitabu vya taaluma vilivyoandikwa kwa Kiswahili.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |