Nini cha kushangaza, mwizi kukatwa mkono au kibaka kuchomwa moto!
Ndugu Mhariri
HIVI karibuni Jimbo moja la Nigeria lilietekeleza sheria ya Kiislamu ya kumkata mwizi mkono. Hukumu hiyo ilitekelezwa baada ya mtuhumiwa kuthibitika kisheria kuwa alikwiba ng'ombe.
Licha ya wizi huo, mtuhumiwa alipewa nafasi ya kujitetea. Isitoshe hata hukumu yenyewe ilitekelezwa kwa misingi ya kibinadamu. Ukataji wa mkono ulifanywa kisayansi ambapo daktari alihusishwa moja kwa moja katika shughuli hiyo.
Muhalifu alidungwa sindano ya ganzi ili asiteseke kwa maumivu na bila shaka baada ya hapo alipata huduma za matibabu.
Pamoja na ubinadamu huo uliofanywa kwa muhalifu, bado wametokea watu waliochukizwa na hukumu hiyo, wakidai imekiuka haki za binadamu.
Mimi nawauliza watu hao, hivi kumkata mkono mwizi wa ng'ombe na kumchoma moto kibaka kwa kuiba shilingi mia mbili, ipi adhabu ya kinyama?
Ningependa kuwajuza wapinzani wa sheria za Kiislamu kuwa sheria za Kiislamu haikukusudiwa kuwakomoa watu bali zimekusudiwa kuihifadhi jamii na uhalifu wa makusudi. Nasema hivyo kwa sababu sheria hizo hutumika kwa kuzingatia mazingira ya jamii.
Kwa mfano, kama hali ya uchumi wa nchi si nzuri sheria husitishwa. Ilitokea wakati wa Ukhalifa wa mmojawapo wa Masahaba wa Mtume (s.a.w.), nchi yake ilikumbwa na baa la njaa, ikabidi Khalifa asitishe sheria ya kukata wezi mikono, hii ni kwa sababu hali ile ya dhiki ingewalazimu watu kupoteza uadilifu.
Hata katika mazingira ya nchi kama Tanzania, sheria hiyo haiwezi kutumika kwa sababu watu wengine wanalazimika kufanya uhalifu kwa sababu ya hali halisi.
Hakuna Muislamu anayeweza kufanya ukatili wa kumuadhibu anayeiba kwa sababu ya njaa. Lakini inastaajabisha kuwa, licha ya hali hiyo watu wanaoiba mafenesi hivi leo wanavishwa matairi na wengine kumwagiwa petroli au mafuta ya taa na kisha kupigwa kiberiti. Huu sasa ndio unyama wenyewe!
Hivi karibuni Bwana mmoja alishambuliwa kwa mapanga hadi kufa baada ya kufumwa akichimba viazi vitamu kwenye shamba la mtu.
Hata huko magerezani waliojaa ni walalahoi. Lakini watetezi wa haki za binadamu kimya! Sio kama tunatetea wahalifu bali ni jumuku la serikali kuboresha maisha ya wananchi ili isiwepo sababu ya kumfanya mtu aibe.
Tofauti na mifumo mingine ya maisha, mfumo wa maisha wa Kiislamu unajali sana ustawi wa maisha ya wananchi ili jamii isalimike na maovu.
Uislamu haurusuhu kabisa watu kuishi kwa tabu hata kulazimika kuiba. Ndio maana umeweka utaratibu wa kutoa zaka, sadaka na Infaq ambapo wenye uwezo kuwasaidia wasiojiweza. Isitoshe serikali yenyewe huwa na hazina (Baitul mal) ya kuwasaidia wananchi kwa kuwapa mitaji ya kuendeshea miradi yao huku mazingira ya biashara yakiwa yameboreshwa kutokana na mzunguko wa fedha kupitia zaka, sadaka na mishahara bora ya wafanyakazi.
Aidha, mbali ya kumpatia mfanyakazi mshahara unaokidhi mahitaji yake, serikali ya Kiislamu hufikia hata kugharamia malezi ya idadi fulani ya watoto katika familia mbalimbali za wananchi wake. Pia hutoa motisha maalumu kwa vijana ili waoe na kuolewa ili kuihifadhi jamii dhidi ya uovu wa zinaa.
Kwa ujumla, Uislamu unaondoa kabisa yale mazingira yanayomfanya mtu atende dhambi iwe wizi, zinaa, rushwa, ulevi na kadhalika.
Mtu akifikia hatua ya kutenda dhambi yoyote kati ya hizo basi ni nafsi yake tu imemtuma na kwa hiyo astahiki kuadhibiwa. Pamoja na hivyo, mtu akituhumiwa kwa wizi, lazima uchunguzi ufanyike ili kubaini sababu zilizomfanya mtu huyo aibe.
Ikithbitika kisheria kuwa ameiba kwa makusudi ndipo sheria inapofanyakazi. Jukumu la serikali za mitaa siku zote ni kuhakikisha watu hawana matatizo yoyote yale iwe chakula, mavazi, ajira na mengineyo.
Sheria hubakia tu kuchunga murua wa jamii lakini watu hawana sababu ya kuikiuka. Mtu yeyote anayepinga au kushutumu sheria za Kiislamu ama hazijui au ana chuki tu na Uislamu.
Mama Akili,
Morogoro.
Ndugu Mhariri
KATIKA tangazo la kukitambulisha kipindi cha Mulika husemwa kwamba katika jamii kuna ndoa za aina nyingi zikiwemo zile za kimila, Kidini na zile za mkeka.
Baada ya maelezo hayo limekuwa likiulizwa swali je ndoa hizi ni halali kwa mujibu wa sheria? Yaani kwa maneno mengine uhalali au uharamu (ubatili) wa ndoa yoyote ile hata zile zifungwazo kwa mujibu wa sheria za kidini, hutegemea sheria zitumikazo mahakamani.
Kisha hudaiwa katika tangazo la kipindi hicho ambacho huoneshwa saa tatu usiku wa kila Alhamisi kuwa wanasheria watatufafanulia uhalali wa ndoa hizo!
Katika moja ya vipindi hivyo mwanasheria Mulika alionesha ubatili wa taratibu za ndoa kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.
Mwanasheria huyo alisema talaka yoyote itolewayo nje ya mahakama si talaka halali. Yaani ili talaka iwe halali lazima ithibitishwe na mahakama.
Akitoa mfano, mwanasheria huyo alitaja "talaka tatu" zitolewazo ndani ya ndoa ya Kiislamu kuwa ni moja ya mambo yaliyo batili kwa mujibu wa sheria. Aidha talaka nyingine yoyote itolewayo kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu ni batili kwa mujibu wa sheria.
Alipoulizwa na mwanahabari Asha Mtwangi je kuna jitihada yoyote kwa wanasheria kujua sheria ya dini ya Kiislamu inaeleza nini kuhusu masuala ya ndoa na talaka, mwanasheria huyo alisema huwa wanawauliza Bakwata kuhusu sheria za Kiislamu!
Kwa mujibu wa Uislamu anayestahiki kuhalalisha au kuharamisha jambo ni Mwenyezi Mungu na Yeye ndiye mwenye haki ya kuwawekea wanadamu sheria na taratibu za kufuata.
Kwa maana hiyo yeyote anayejipa mamlaka ya kutunga sheria akawalazimisha wengine wazifuate au yule anayejipa mamlaka ya kuhalalisha na kuharamisha jambo anakuwa amejipa mamlaka ya uungu!
Ningependa kuwasihi wanasheria wa kipindi cha Mulika na wengineo ambao hujifaragua kuisemea sheria ya kiislamu bila ya kuijua wakiwa wataalamu wenye kujua miiko ya kitaaluma waanze kujifunza sheria ya Kiislamu ili wafahamu kwa kina inasemaje badala ya kuegama kwenye "kusikia sikia" yale yasemwayo mtaani.
Nachukua fursa hii pia kuitahadharisha serikali juu ya ile sheria yake ya ndoa na talaka ya mwaka 1971. Sheria hiyo inapingUislamu na Waislamu hawako tayari kutii jambo linalokwenda kinyume na maamrisho ya Muumba. Kwa hiyo kwa nujibu wa Uislamu sheria hiyo ya ndoa (Marriage act 1971) ni batili na Muislamu kuifuata ni ukafiri.
AbdulWahab Bashir Ali,
Dar es Salaam.
Ndugu mhariri,
KATIKA siku za hivi karibuni umejitokeza msemo wa kuwekeza hasa hasa ukiwa na maana ya kuwaalika watu kutoka nje waje na makampuni yao au wanunue makampuni ya hapa nchini ili wawekeze katika sekta mbali mbali.
Kwa ajili hiyo viongozi wetu hasa wanapofanya ziara za nchi nyingine hutamka kwa vinywa vipana kuwataka wafanyabiara wa huko wafanye haraka kuja nchini.
Kwa mtazamo wangu huu ni "umatonya" wa kimya kimya unaofanywa na viongozi chini ya kivuli cha uwekezaji.
Unapomwita mtu aje kutoka huko anakotoka kuwekeza nyumbani kwako lazima kwanza uwe umewaandaa wananchi wako kuikabili hali hiyo, usipofanya hivyo ni dhahiri utakuwa umekubali wawe watumwa wa wageni.
Ni sawa na wale makaburu walionunua benki yetu kwa bei poa kisha wakatoa masimango kuwa wameacha wake zao wakaja hapa ili kuwasaidia watanzania waondokane na uhohe hahe uliowazingira.
Kauli hiyo, chambilecho cha Profesa Lipumba kuwa hata wakoloni walikuja kuchota utajiri wetu na kutukandamiza wakiwa wamewaacha wake zao makwao, ni ya kashfa kubwa kwetu watanzania.
Kwa nini viongozi wetu washindwe kuwa na mipango makini ya maendeleo badala yake wende kuinadi nchi kwa wafanyabiashara wakubwa wa mataifa mengine, je huku sio kutangaza kushindwa kuongoza? Je Watanzania tunaonekanaje kwa mataifa hayo kama sio kudharaulika?
Waziri mkuu alipokuwa nchini China mwandishi wake aliripoti kushangazwa kwake na jinsi jimbo moja la nchi hiyo lilivyoweza kulifanya eneo lenye ukame unaofanana na ule wa Singida na Dodoma kutoa chakula cha kutosheleza jimbo hilo na kuhangaika kutafuta soko la kuuza ziada.
Kushangazwa huku kwa mmoja wa viongozi wetu wakuu wa kitaifa kunatupa wasi wasi wananchi wa kawaida. Je wataalamu wa kilimo wa hapa nchini wameshindwa kumuonesha waziri mkuu jinsi ardhi kame inavyoweza kugeuzwa ikatoa mazao. Inashangaza zaidi waziri mkuu akiwa mtu aliyesomea masuala ya kilimo na aliyepata pia kuwa waziri mdogo wa kilimo kutokujua namna ardhi kame inavyoweza kurutubishwa.
"Umatonya" wa kuchekelea kila tutakachooneshwa na mabwana wakubwa ili wakidhi haja zetu, unaidhalilisha nchi.
Sera ya uwekezaji kutoka nje inayopewa sura ya "mgeni njoo mwenyeji apone" ni ukoloni mwingine tunaoukaribisha kwa mikono miwili kwa kushindwa kwetu kuwa na mipango makini ya kuendesha nchi.
Abu Hafsa
Dar es Salaam
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi katika gazeti lako ili niwajulishe wasomaji kuwa Dar es Salaam ndio chemchem ya kila jambo.
Linaloundwa Dar lipokelewe mikoani iwapo ni zuri.
Watu wa Dar ndio walioanzisha michezo kukutanisha mikoa kwa ajili ya mpira wa miguu mwaka 1944. Ndio walioanzisha harakati za kudai uhuru mwaka 1954.
Wakaanzisha mihadhara na sasa wameanzisha "tusikubali kuonewa au kudhulumiwa".
Macho na masikio ya mikoani yawe Dar.
Khamis Alawi (Madema),
S.L.P 2607,
Soko Kuu Lindi Mjini.
Ndugu Mhariri
MACHI 26, mwaka huu, Chama Cha Wananchi (CUF) kilifanya mkutano mkubwa Jangwani Jijini Dar es Salaam.
Jambo la kushangaza vyombo vyote vya habari (ukiacha gazeti moja la wiki) havikuripoti kabisa mkutano huo.
Baada ya mkutano wa CUF, CCM wakafanya mkutano kushutumu yale yaliyozungumzwa katika mkutano wa CUF.
Mkutano huu wa CCM ukaripotiwa na kupewa uzito katika magazeti, RediO na TV.
Sasa jambo linalotushangaza ni vipi vyombo vya habari viripoti shutuma wakati yale yanayoshutumiwa havikuripoti?
Huu ni mtindo mpya wa habari tunaoushuhudia hapa Tanzania.
Mwashamba Ramadhani,
Manzese,
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |