KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI


1970 uwe mwaka wa ngumbaru


UHURU, Alhamisi, Januari 1, 1970.

RAIS NYERERE jana usiku aliutangaza 1970 kuwa mwaka wa Elimu ya Watu Wazima na kusema kuwa shabaha ya kwanza itakuwa shughuli ya kuwaelimisha watu wazima katika kutimiza ahadi moja ya TANU isemayo: "Nitajielimisha kadri ya uwezo wangu wote na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote".

Katika salamu za Mwaka Mpya zilizotangazwa kwa njia ya redio, Mwalimu alisema kuwa ingawa tumezungumza sana habari ya elimu ya watu wazima, na ingawa watu wengi wamelishughulikia jambo hili, hatujapata bado kujiandaa hasa ili kuushambulia ujinga.

"Kamati Kuu ya TANU sasa imeamua kwamba lazima tuifanye kazi hiyo katika mwaka 1970. Miezi kumi na mbili ijayo lazima iwe na lengo la kuwaelimisha watu wazima", alisema.

Mwalimu aliendelea: "Sisi ni maskini na tuko nyuma. Na watu wengi mno miongoni mwetu wanaikubali hali hi tuliyo nayo kana kwamba ni amri ya Mungu na wanadhani kuwa hatuna la kufanya kuondoa hali hiyo".

Shabaha ya kwanza ya elimu ya watu wazima, alisisitiza Mwalimu, lazima iwe kujiondoa katika kuikubali hali ya maisha ambayo watu wa Tanzania wameishi karne nyingi zilizopita.

Hatuna budi kufahamu kuwa si lazima tuishi katika vibanda vibovu, au tulime kwa vijembe vibovu na katika hali ya udhaifu wa afya. Hatuna budi kutambua kwamba sisi wenyewe tunaweza kuyakabili mambo hayo. Kazi ya kwanza ya elimu ya watu wazima itakuwa kutufanya tukatae vitu hivyo na kwamba sisi wenyewe tunao uwezo wa kupata nyumba nzuri zaidi, vyombo vizuri zaidi vya kufanyia kazi na afya nzuri zaidi.

Tujifunze kubadili maisha

Shabaha ya pili ya elimu ya watu wazima ni kujifunza jinsi ya kuyabadili maisha yetu. Kwa hiyo hatuna budi kujifunza jinsi ya kuongeza mazao katika mashamba yetu, katika viwanda vyetu na katika ofisi zetu na kula chakula bora ambacho kinahitajiwa katika miili yetu, alisema.

Mwalimu aliongeza, hatuna budi kujifunza habari za mipango yetu ya maendeleo ya uchumi, ili tuweze kuhakikisha kwamba wote tunatimiza wajibu wetu katika kuifanya mipango hiyo ifanikiwe na kuhakikisha kwamba wote tunafaidika kutokana na mipango hiyo.

Elimu ya watu wazima ni kujifunza jambo lolote lile ambalo litatusaidia kubadili na kutumia mazingira hayo ili kuinua maisha yetu. Aliongeza: "Elimu si muujiza fulani unaotokea darasani tu. Ni kujifunza kutoka kwa watu wengine na kujifunza kutokana na mafanikio na makosa yetu wenyewe ya siku zilizopita".



SHAMRA ZA IDI:
Kachukua mtoto siye wake


Ngurumo, Jumatano Aprili 6, 1966
 

SHAMRA za Iddi kuwa zimeleta mkasa kidogo huko kwenye hospitali ya wazazi Ocen Road mjini Dar es Salaam.

Wazazi walikwenda kujifungua, kama kawaida yao baada ya hapo hurudi tena kwao. Sasa wakina mama nafikiri hapa walikuwa na haraka ya kwenda kula Iddi majumbani mwao, wakiwa na furaha mbili, ile ya Iddi na ile ya mgeni yaani mtoto.

Katika shamra shamra hizo, mama mmoja alijifungashia mtoto ambaye kazaliwa na mwenzake. Kwa ajili ya makosa kidogo.

Hapo jana, Bwana Mganga Mkuu wa hospitali hiyo ya wazazi amewaomba wazazi wote warudi tena hospitali ili nafikiri watoto wakapimwe na yule aliyechukua mtoto siye wake atapewa mali yake.

Wazazi hao wanaotakiwa ni wale ambao wamejifungua tarehe mosi na pili. Nauli zao watarudishiwa wasiwe na shaka.


Marikani ajenga kituo cha vita Sudan


Ngurumo Jumatano, Februari 16, 1966

HABARI kutoka Khartum, Sudan zimeeleza kwamba serikali ya Amerika itajenga kituo cha kivita katika sehemu ya kusini ya Sudan, kituo hicho ni badala ya kile kituo kilichokuwa Unguja ambacho kilibomolewa mara tu baada ya mapinduzi.

Habari nyingine zinasema serikali ya Sudan imefikisha mapatano ya kisiri na Amerika. Kwa kufuata mkataba huu wa kisiri, Amerika itaipa serikali ya Sudan pesa za dola milioni 40, vile vile itapeleka Sudan kiasi kikubwa cha silaha pamoja na vitu vingine vya kivita.

Serikali ya Sudan imekwisha pata ndege maalum zinazoitwa "Helicopter". Ndege hizo zinaendeshwa na wanahewa Wamerika waliopata ujuzi wa vita kupinga wananchi huko Vietnam.

Utawala

Mojawapo ya masharti ya msaada huo yaliyowekwa na Marikani ni madai kwamba serikali ya Sudan ipige marufuku Chama Cha Kikomunisti cha Sudan, ianzishe utawala wa chama kimoja tu nchini, vile vile iwaruhusu Waamerika kujenga kituo cha kivita katika sehemu ya kusini ya Sudan kitakachowawezesha kuikagua sehemu nzima ya kati ya Afrika.

Matokeo yaliyotokea majuzi yashuhudia kuwa serikali ya Sudan imekubali masharti hayo ya Marekani. Zaidi ya hayo, kwa kusudi la kuwashambulia Wakomunisti serikali ya Sudan iliomba serikali ya Amerika "msaada wa wataalamu".

Kwa kufuatia ombi hili, mwaka uliopita maofisa wa Idara ya Upelelezi ya Amerika (C.I.A.), Major Luter Lloyd, Captain Perry Robert, vile vile makamu wa Director wa ofisi ya C.I.A. inayoshughulika na mambo ya Near East , Allen Adams wote walikwenda Khartum.

Mwandishi mmoja wa habari wa Sudan jina lake Mohammed Abbas, anayejulikana kwa kushirikiana kwake na C.I.A. pia alifika Khartum kutoka Cairo.

Kuwashambulia Wakomunisti huku Sudan kulianzishwa na hatua ya kuchochea iliyochukuliwa na mwanafunzi Shangwi chini ya uongozi wa Marekani.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook