Morogoro:
Kielelezo cha ufukara na sera za kibalakala nchini - 4

AIDHA, pamoja na matatizo mengine, viwanda kadhaa vya Morogoro vimekuwa vikiendeshwa kwa kusuasua na vingine kufa kabisa, jambo ambalo limechangia kuathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa mkoa huu.

Tikiutupia macho kwa maneno machache sana uwanja wa biashara mkoani, tunapata picha kuwa sekta binafsi inayoongoza katika eneo hili kama ilivyo katika viwanda hususan baada ya taasisi za biashara za umma kama vile RTC kufa.

Ukiacha wafanyabiashara wakubwa wengi wao wakijali maslahi binafsi zaidi kuliko utu katika utendaji wao wa kila siku iwe kwa wateja au wafanyakazi wao, wafanyakabiashara wadogo wadogo walioko katika sekta isiyo rasmi ndiyo wanaoongoza kwa wingi mpambano wa biashara huria.

Wengi kati ya hawa ni wale walioachishwa kazi kama si kustaafishwa katika sekta ya umma kufuatia sera ya ubinafsishaji, na wengine ni wanafunzi na hata wahitimu waliokosa kazi za kuajiriwa au kujiajiri zinazoona na taaluma zao.

Watu wote hawa licha ya kujiita kuwa "wamejiajiri" lakini kile wakifanyacho ama hawana ujuzi nacho, au hakioani na taaluma walizonazo, kutokana na serikali kutowawekea mazingira mazuri ya kujiajiri.

Kiuhakika kundi hili la wafanyabiashara ndogo ndogo, mama ntilie na "mafundi mchundo" limekuwa kama kundi la kondoo wasio na mchunga, au watoto wasio na mlezi (watoto wa mtaani) kwa kifupi hili ni kundi la watu wasiojua mustakabali wa maisha yao mbeleni.

Hawa ni watu ambao hawafanyi biashara kwa kutafuta faida itakikanayo.

Je, uchumi wa mkoa utanawili kwa stahili ya biashara na wafanyakazi wa aina hiyo?

Mamlaka husika badala ya kuwawekea Morogoro hawa miundo mbinu watu wao wanawahujumu kwa njia moja au nyingine, jambo ambalo ni sawa kabisa na kuhujumu mkoa kiuchumi. Na mazao ya hujuma hizo ni ufisadi wa aina zote.

Tukitazama tija katika uwanja wa viwanda na biashara kimkoa, Morogoro bado kabisa haijaonesha kile kipatikanacho katika sekta hiyo kwa uhalisia wake wala kule kinapokwenda.

Je, sekta hiyo inaunufaisha mkoa au faida yake inaishia katika 'mifuko mipana' ya serikali kuu huku ikiwaacha wakazi wa Morogoro wakipiga miayo ya njaa?

Maliasili:

Kama kuna eneo tajiri kabisa la maliasili duniani basi eneo la mkoa wa Morogoro ni mojawapo.

Tukianza na misitu kwa mfano, tangu Desemba 31 mwaka 1988, Morogoro ilikuwa na eneo la misitu lenye kilometa 36,964, misitu ya hifadhi ikiwa ni kilometa za mraba 14,015.

Zaidi ya hapo mkoa ukaotesha miche 583,218 na kuipanda katika eneo lisilopungua hekta 277.

Rekodi zinaonesha kuwa tokea wakati huo hadi hivi leo wastani wa zaidi ya kilomita 9,561.6 za mbao na magogo huvunwa kila mwaka ambazo huingiza mamilioni ya shilingi yasiyounufaisha kwa lolote mkoa huo.

Maliasili hiyo pia hufujwa mno kwa kukatwa kiholela nishati kwa matumizi mbalimbali ya majumbani na viwandani kwa mfano, kati ya mwaka 1985 hadi 1988 zaidi ya kiubiki mita 77,180 za kuni zilivunwa. Na magunia 89,579 ya mkaa yalizalishwa kati ya mwaka 1986 na 1987.

Kibaya zaidi ni kwa serikali kutopanga mkakati wowote wa kuokoa hujuma hiyo mbaya kabisa dhidi ya misitu yetu kwa kuhakikisha kwamba nishati mbadala kama vile ya upepo au nishati ya jua (solar energy) inapatikana kwa urahisi na gharama nafuu zaidi.

Hujuma nyingine mbaya mno ni ile ya "mashindano yasiyo rasmi" ya kuchoma moto misitu yanayofanywa kila mwaka, hivyo kuteketeza aina kadha wa kadha za miti iliyobebwa na ardhi ya Morogoro.

Miongoni mwa aina hizo ni pamoja na Mgunga (Acacia Senegal kwa jina la kitaalamu) unaopatikana Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo - Magadu. Aina nyingine ya Mgunga (Acacia torulosa) unapatikana huko Kiroka, Mshanga (Adenanthera pavonina) unapatikana huko wilayani Morogoro, Mkora (Afzelia quanzensis) unaopatikana Mahenge wilayani Ulanga, Mliende (Albizia lebbeck) unaopatikana kwa wingi kiasi wilayani Morogoro na uwanda wa Wami Dakawa. Na Msambu au Mkani (Allan bleckia Ulugurensis) unaopatikana kwa wingi katika milima ya Uruguru ambayo imegeuzwa kipara kwa kwa kufyekwa misitu yake na kuchomwa.

Miti mingine inayovinjari katika ardhi nzuri ya mkoa huu huu ni Mwarobaini (Azadirachta Indica).

Aidha, ardhi ya Morogoro imebeba mkarangamtiunaopatikana Mahenge, Myombo iliyopo katika hifadhi ya wanyama ya Mikumi ambayo mapato ya uendeshaji wake pia hayako wazi kwa wakazi wa Morogoro.

Pia kuna mkababu ulioko Morogoro Hotel, mfudufudu iliyoko karibu na kiwanda cha kusindika tumbaku Morogoro, mjakaranda unaopatikana Kingolwira na aina nyingi nyinginezo ambazo bei ya mbegu zake ni kati ya shilingi 4000 na 40,000 kwa kilo.

Nyuki:

Nta na asali ni mazao muhimu ya nyuki ambayo yana bei nzuri katika soko la kimataifa. Kama Morogoro ilivyokosa viwanda vya kusindika vyakula na vinywaji, vivyo hivyo imekosa kiwanda cha asali.

Hata hivyo, tangu mwaka 1988 Morogoro kama mkoa ulikuwa na mizinga 4,292 ya kisasa na ya jadi zaidi ya 11,265, idadi ambayo ni ndogo mno ukilinganisha na ukubwa wa mkoa kijiografia na mwitu ilionao.

Kufuatia hali hiyo, mazao yanayozalishwa na fedha inayopatikana pia huwa si ya kuridhisha. Kwa mfano, takwimu zinaonesha kuwa mwaka 1985/86 mkoa ulizalisha kilogram 1,602 tu zilizoingiza shilingi 215,000 tu!! Aidha, ukazalisha nta kilogram 2,552 na kuingiza shilingi 127,000 tu!

Pia mwaka 1986/87 ilizalisha nta kilogramu 650 iliyoingiza shilingi 39,000 tu. Na asali ilizalishwa kilogramu 9,240 zilizoingiza si chini ya shilingi milioni tatu tu za Kitanzania! Hakuna mabadiliko yoyote hivi leo juu ya nyuki, nta na asali yake!!

Uvuvi:

Miongoni mwa neema zilizopo Morogoro ni kupitiwa na mito mikubwa kama vile mto Wami, Ruaha na Ruvu, mabwawa kadhalika.

Hata hivyo, hakuna mpango wowote wa makusudi wa wazi kabisa wa kuzifanya maliasili zilizomo humo kama vile samaki na mamba ziwe sehemu mojawapo muhimu za uchumi wa Morogoro.

Hakuna hata kituo kimoja chenye sifa ya kuitwa "kituo cha uvuvi" wala mito husika haijasanifiwa kabisa kuwa sehemu muafaka kwa shughuli za uvuvi na usafirishaji wa mazao ya sekta hiyo.

Kwa serikali yenye mipango inayotekelezeka na viongozi wabunifu, mto Ruaha ambao ni shina la Mto Rufiji mbeleni kwa mfano, wafaa kabisa kuwa 'kiunga' cha uvuvi na ufugaji wa 'mazao ya maji baridi. Lakini, kwenye miti hakuna wajenzi.

Aidha, ni eneo muafaka la kuwekewa boti ndogo ndogo za uvuvi na viwanda vidogo vidogo vya kusindika minofu ya samaki wa maji baridi na mazao yake hususan miiba, hivyo kuinua uchumi wa mkoa na taifa kiujumla ikiwa ni pamoja na kuingiza fedha nyingi za kigeni.

Mipango mibovu na ukosefu wa uongozi bora imepelekea sekta ya uvuvi Morogoro kuendeshwa shaghalabaghala.

Itaendelea toleo lijalo
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook