JAPO umaskini limekuwa vazi la wananchi wengi lakini, kwa hakika hakuna anayeupenda. Basi tu mtu afanyeje! Maisha ya umaskini hutawaliwa na dhiki, huzuni na unyonge siku hadi siku. Kufuatia uzoefu unaoambatana na utafiti, makala haya yanaielezea hali hiyo ya maisha katika nyumba za wanyonge.
BABA Shida akiwa na familia yake wanaonekana wamesawajika. Baba amejiinamia akionekana mwenye lindi la mawazo, Mama ameshika tama, watoto wamekaa chini hapa na pale wakiwa wamechoka.
Hiyo ndiyo hali niliyokuta nyumba moja eneo fulani.
Baada ya kusabahiana nao, nilijitambulisha kuwa ni mwandishi ninayetokea gazeti fulani na nilikuwa katika shughuli za kikazi.
"He! Nyie mnaoandika magazeti mnafika mpaka huku, mnatafuta nini?" alihoji mama Shida.
Hata hivyo, wote walinikaribisha vizuri, alianza Baba Shida karibu kwenye kigoda, nikaketi. Akaendelea karibu sana mwanangu, naye mama akaongeza karibu mwanangu. Nikawauliza habari za hapa, wakajibu "salama hivyo hivyo baba mradi kunakucha". Nikauliza kwanini mama. Baba we acha tu alijibu kwa masikitiko bi mkubwa yule.
Akaendelea kusema, mwanangu maisha yanatuelemea. Hivi unavyotuona, baba, hatujapata chochote cha kutia tumboni tokea jana usiku. Ndio maana unawaona wadogo zako wapo hapa saa hizi.
Kwa kawaida muda huu wanakuwa mchezoni. Lakini leo wameshindwa. Hivi navutia vutia muda ili baadaye niende hapo mashineni nikapete pumba za mpunga ili tupate vichenga vya kuchemsha. Na pumba zenyewe ni za kubahatisha maanake tuko wengi huko mashineni. Inabidi uwahi kama saa kumi na moja hivi la sivyo utakuta wenzio wamekwishazoa zote.
Natazama saa, ni saa tisa na nusu alasiri, huku mama akiendelea kusema, huyu mdogo wako hapa miguuni amelia mpaka amelala. Hivi akiamka sijui nitambebea mbeleko gani. Hawa wakubwa wanaweza kuvumilia njaa lakini haka bado kadogo sana, hakawezi.
Hao wakubwa wana wiki ya pili sasa hawajaenda shule, pesa za kulipa ada hatuna. Baba yako ndio kama unavyomuona, maarifa yote yamemwisha, kazi kasimamishwa, mafao yake hajapata. Na shambani mwaka huu, mwanangu hatukuambulia chochote, tulitegemea kijishamba cha mihogo, lakini nacho kimeshambuliwa na nguruwe, aa! wanyama hawa wametufanya kazi safari hii!
Haya, nilikuwa na biashara ya vitumbua, mgambo wamenimwagia, mtaji umekufa, Basi shida moja kwa moja baba, akamaliza mama Shida. Baba Shida, ambaye muda wote alikuwa kimya, akitikisa kichwa, ana familia ya watoto watatu, Sikitiko ambaye ni binti wa miaka kumi na minne, Dunia mwenye miaka tisa na Jaribu, kitindamimba anayekaribia miaka saba. Hata hivyo, Baba na mama Shida waliwahi kuwa na watoto wa tatu wakubwa ambao walikufa baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba. Miongoni mwao alikuwa Shida.
Baada ya maelezo ya mama Shida yaliyonitia simanzi nzito iliyonilazimu kupapasa mifuko licha ya ukata nilionao, mazungumzo yetu hayakauendelea sana. Sikuweza kuwa na ukavu wa kuhoji kile kilichonipeleka. Tukaagana na huku wakisikitika kuwa mgeni sikuandaliwa chochote.
Siku nyingine nilipata wasaa wa kutembelea nyumbani kwa marehemu mzee Matatizo aliyefariki kwa ugonjwa wa kipindupindu uliosababishwa na maji machafu baada ya serikali kushindwa kuwapatia wananchi wa eneo husika huduma ya maji safi na salama.
Lahaula! Hapo nyumbani nikakuta watu wanaanua tanga. Nilipouliza, nikajibiwa kuwa mtoto wa pili wa kiume wa hayati mzee Matatizo aitwaye Mateso, alizikwa siku kadhaa zilizopita. Aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kujaribu kuiba mkungu wa ndizi.
Nikazunguka uani nionane na mama Mateso. Nikamkuta yu taabani kwa kuondokewa na dume lake. Kwa uchungu mkubwa wa uzazi, mama Mateso alinisimulia kuwa siku ya kifo cha mwanae, yeye na marehemu waliongea sana nyumbani tokea asubuhi hadi mchana.
Maongezi yao zaidi yalihusu maisha. Akikariri maneno ya mwanawe, mama Mateso alinieleza kuwa marehemu kwa masikitiko makubwa alimwambia , "mama, mimi naona maisha yamezidi kuniwia magumu baada ya kibanda changu cha biashara kubomolewa na Tume ya jiji. Na mimi ndio mtoto wa kiume kwako niliyebaki hapa nyumbani hivyo lazima nihangaike kukusaidia wewe mama, vinginevyo nani atakusaidia.
Huku akibubujikwa na machozi, mama Mateso aliendelea kusema, kauli ya mwisho aliyonitamkia mwanangu ni kuwa mama naona leo hatuna kitu kabisa hapa nyumbani, ngoja nitoke nikahangaike. Kumbe masikini mwanangu ndio alikuwa ananiaga.
Huku akizidi kulia kwa kwikwi na macho yake yakiwa yamevimba kwa kilio, mama Mateso alisema, ee! Yarabi, ninusuru mie, huyu ni mwanangu wa pili nazika sasa. Dada yake Huzuni alikufa kwa uzazi mwaka jana, baada ya kukosa huduma hospitalini kwa kushindwa kutoa shilingi elfu tatu.
Nimebakiwa na mtoto mmoja wa kiume Masumbuko ambaye yuko gerezani baada ya kukamatwa kwa kosa la uzururaji. Kwa hiyo baba, mama yako nimebaki mkiwa. Hii nyumba japo ni kibanda lakini naiona kubwa kwa upweke.
Sasa sijui huyo Masumbuko atafungwa miaka mingapi huko jela, huzuni ilioje mwenzenu mimi. Mwanangu Masumbuko hajui kuiba cha mtu jamani. Mwenyewe shughuli yake ni kuitilia abiria kwenye mabasi, wenyewe wanasema sijui kupiga debe. Akipata visenti, analeta nyumbani, tunanunua unga, tusonge ugali wetu, tunakula. Lakini sasa nasikia serikali inazuia wapiga dege.
Mwanangu, uchungu wa mwana aujua mzazi. Ukikumbuka uzazi halafu ufikwe na haya yaliyonifika mimi, dunia yote unaona inakuelemea wewe. Tumewazaeni wanetu kwa matarajio kuwa mje kuwa na maisha bora kuliko yetu, mtulee na kutuzika lakini ndoto hiyo kwangu mie mama Mateso imetoweka. Nimekuwa mama Mateso kweli jamani!
Baada ya kumsikiliza mama Mateso kwa majonzi nikamuhani na kumuaga. Akaniambia asante baba, safari njema, uzidi kunikumbuka mama yako.
Kutoka hapo, sasa naelekea nyumbani kwa baba Tabu. Kufika hapo, nikakuta yeye, mkewe na mtoto wake mkubwa wa kike wakitoa nje vifaa vyao vya kulalia na kuvianika juani kufuatia mvua iliyonyesha usiku wa jana yake. Mvua hiyo mbali ya kupenya ndani kutokana na uchakavu wa paa, pia iliangusha upande mmoja wa nyumba hiyo ya miti.
Baba Tabu ana familia ya watoto wanne, Tabu, Mwanjaa, Vumilia na Mashaka ambaye wenyewe wamezoea kumwita Mziwanda. Ingawa Mziwanda ambaye ndiye mtoto wa pekee wa kiume, anasoma shule darasa la tano, lakini ameshindwa kwenda shule na badala yake amekwenda kuuza mahindi ya kuchemsha ili hela zitakazopatikana zisaidie nyumbani na pesa nyingine "zidundulizwe" ili apate ada na nguo za shule.
Kuvuja na kubomoka kwa nyumba kumewafanya baba na mama Tabu wasiende shambani. Ndio maana nimewakuta nyumbani. Baada ya kumaliza kutoa vitu ndani sasa wanapata nafasi ya kuongea nami. Nikaanza kwa kuwapa pole, wakajibu tumeshapoa baba.
Anaendelea kusema baba Tabu, jana hatukulala mwanangu mvua imetunyeshea kucha mpaka pale ilipokoma. Sasa afadhali sisi wazima, tabu ilikuwa kwa huyu dada yako mdogo Vumilia ambaye ni mgonjwa mgonjwa. Wakati huo binti huyo alikuwa amelala kwenye gunia.
Pamoja na hali yake mbaya ya afya, wazazi wameshindwa kumpeleka hospitali kwa ukosefu wa fedha au wengine husema ukata. Kabla ya kupata ugonjwa, Vumilia ambaye ni msichana anayekaribia miaka kumi na mitano alikuwa msaidizi wa ndani katika nyumba ya bosi mmoja mjini.
Nilipouliza kwanini Vumilia afanye kazi badala ya kwenda shule. Mama Tabu alijibu aa! Baba mwanangu tuseme nini sijui. Kibarua chake kilikuwa kinamsaidia na kutuokoa kweli hapa nyumbani. Tunapenda mno mdogo wako asome lakini hali hairuhusu baba.
Hizo ajira za watoto hata zisingekuwepo kama hali ya maisha ingekuwa nzuri. Hakuna mzazi mwenye kujua uchungu wa kuzaa anayependa kinda lake kama hili likatumikishwe. Huyu hata harufu ya maziwa hayajesha mdomoni lakini tufanyeje mwanangu.
Sasa wakipiga marufuku hizo ajira za watoto sio kwamba watawasaidia watoto bali watawaweka katika hali ngumu zaidi kama hivi unavyoona mwanangu. Hapa tegemeo letu ni mwanangu Mziwanda Mashaka ambaye amepeleka biashara mjini. Hivyo akirudi ndio tujue kula. Mlo wetu hapa baba hauna ratiba maalum. Wakati mwingine joni hadi jioni kama hivi tukila jioni ya leo, basi mpaka jioni ya kesho panapomajaaliwa.
Nilipoulizia maendeleo ya kilimo, mama Tabu alijibu, mwanangu wee! Kilimo cha jembe la mkono nacho kilimo. Ni kilimo cha kuvunja uti wa mgongo. Miaka yote tunalima, na huyu baba yako ni hodari kweli kulima lakini wapi baba.
Mavuno tunayoyapata ni hafifu mno hapo ndio shamba likikubali, likikataa tena ndio usiseme. Kidogo hicho hicho tunachovuna inabidi tuuze ili tupate pesa za kukidhi mahitaji mengine nayo kama vile kununua nguo na hata kwa ajili ya matibabu.
Wakati tunaongea, mara alitokea msichana mwembamba hivi. Mama Tabu akanitambulisha kuwa huyo ndiye Mwanjaa na akaongeza kuwa mwaka jana msichana huyo alifiwa na mtoto wake. Mtoto huyo alikufa kwa utapiamlo.
Hali ngumu ya maisha imesababisha binti huyo atalikiwe na mumewe. Ndio sababu binti huyo sasa amerudi kwa wazazi wake. Mama Tabu akaniambia kuwa, kama ningekuwa tayari, wangeweza kuniozesha binti huyo hata bure, kwani anaadhirika tu pale nyumbani.
Nilitabasamu na kumuangalia baba Tabu ambaye jina lake hasa ni mzee Majuto. Yeye akasisisitiza yale yaliyosemwa na mkewe. Akaongeza kusema, umaskini mwanangu ni adui mkubwa sana wa binadamu. Umasikini unatia unyonge na kushusha thamani ya mtu.
Leo hii mimi ninathamani gani mbele ya hawa wanangu. Wakati mtoto wa mwenye nacho au mtoto wa kiongozi wa serikali anamuonea fahari baba yake, mimi nina faida gani kwa wanangu. Kila wanachohitaji, mimi sina uwezo wa kuwapatia. Wananijali na kunipenda kwa kuwa tu wametokana na mgongo wangu, alisikitika mzee Majuto na mimi nikamliwaza.
Baada ya mazungumzo na mzee Majuto, nikaona sasa niwaage wenyeji wangu. Wakasikitika sana kwa kutoweza kuniandalia chochote.
Wakati natembea njiani, nikakuta watu wamejaa sehemu fulani, wakiangalia juu ya mti wa Zambarau au mzambarau. Nilipotupa macho juu ya mti huo, nikaona mwili wa binadamu unaning'inia.
Mama mmoja wa makamo akawa anamwambia mwenzie kuwa bwana huyo ni jirani yake anaitwa Mawazo. Akasema hilo ni tukio la tatu mtu kujinyonga. Baada ya pilikapilika za wananchi kwa ushirikiano na polisi, mwili wa mtu huyo ukashushwa. Katika upekuzi ikakutwa barua iliyosomeka hivi:
"Nimeamua kujiua kutokana na hali ngumu ya maisha, tafadhali asisimbuliwe mtu yeyote kuhusiana na kifo changu".
Kwa mujibu wa wananchi waliokuwepo hapo, hata wale waliojinyonga awali waliandika ujumbe kama huo. Mwanadada mmoja alisikika akisema, "haya maisha magumu yatatutamaliza jamani, halafu bado tu mtu anaipigia kura CCM jamani, Miaka arobaini sasa iko madarakani hali zetu zinazidi kuwa mbaya".
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |