Kodi katika mafuta imevuka mipaka

KABLA ya kuingia kwa sera za ubinafsishaji na mambo ya soko huria, Serikali ilikuwa inajitahidi kudhibiti mfumuko wa bei kwa bidhaa muhimu.

Katika utaratibu huo, mafuta yangeweza kupanda bei pengine mara moja tu kwa mwaka. Na mara nyingi ongezeko hilo lilikuwa likitangazwa wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti.

Haina maana kuwa kama bei ya mafuta ilisalia bila kuongezeka kwa mwaka mzima, bei haikuwa ikipanda katika soko la dunia. Wala haina maana kuwa Serikali ilikuwa ikitoa fedha zake kufidia ongezeko ili mlaji asiumie.

Kama bei ya kuagiza mafuta pamoja na kodi zote ilikuwa Sh. x, makampuni ya mafuta yalikuwa yakiuziwa kwa y shs. y Kwa bei hiyo ilikuwa ikipatikana faida, y-x = z shs.

Faida hii ilichukuliwa na serikali na ilijulikana kama 'wind fall profit'Bei ya mafuta ikiongezeka katika soko la dunia, y ilikuwa haiongezeki ila x iliongezeka na faida z kupungua.Lakini wakati mwingine bei ya mafuta ilipungua pia na y kubakia pale pale kwa hiyo z kuongezeka.Mfano mafuta yalishuka sana bei Februari 1999 katika soko la dunia,hivyo wind fall profit ikawa kubwa sana.Lakini ilipofika Julai mwaka huo huo bei ya mafuta ikapanda sana hivyo z kupungua.

Kutokana na kazi hiyo ya kudhibiti mfumuko wa bei na yenyewe kupanda ikishuka ndio ikaitwa wind fall profit.Lakini katika Bunge la Bajeti mwaka jana,faida hii ilifanywa kuwa kodi iliyowekewa kiwango maalum(fixed).Kutoka wind fall profit ikawa wind fall profit tax.Sasa kinachoamua bei ya mafuta ni soko la dunia. Ule mchango wa wind fall profit haupo tena.

Mwakilishi wa Benk ya Dunia nchini Bw.James Adams,hivi karibuni amenukuliwa na vyombo vya habari akisema,ongezeko la bei ya mafuta ni la kimataifa,hivyo serikali haiwezi kulaumiwa.

Bw. Adams amesema, sekta ya mafuta imebinafsishwa, hivyo serikali haihusiki tena na upangaji wa bei.

Ni katika mtizamo huo huo, wananchi wanaweza kuuliza hii 'wind fall profit' ambayo ilikuwa inadhibiti mfumuko wa bei, serikali inachukua ya nini wakati haipangi bei?

Laiti serikali isingeing'ang'ania 'faida' hii bei ya petrol kwa sasa isingezidi sh. 462 na dizeli ingekuwa kiasi cha sh. 390.

Baadhi ya maofisa wa serikali wameeleza kuwa serikali haiwezi kuiacha kodi hiyo kwani imekuwa ni kitega uchumi kikubwa sana.

Mafuta yanayotumika nchini si chini ya lita 650 Milioni kwa mwaka. Kila lita ya petroli ikilipiwa sh. 98.50 na sh 120 kwa dizeli ni takriban sh 70,850,000,000 zinakusanywa kutokana na kodi hii ya windfall profit/Tax. -

Hiki si kiwango kidogo cha fedha japo mwananchi anaweza asiione katika huduma za maji, akienda hospitali, huko mashuleni; mishahara ya waalimu; polisi na hali za barabara huko vijijini.

Kabla ya zoezi la ubinafsishaji yalikuwepo mashirika na makampuni ambayo yalikuwa yakiingizia serikali faida. Mfano ni kampuni ya sigara.

Hivi sasa kila kitu kinauzwa ikiwa ni pamoja na machimbo muhimu ya madini. Mali [madini] serikali imewapa wawekezaji wa nje yenyewe inapewa kodi kidogo.

Kwa mujibu wa tarifa zisizo rasmi kila dhahabu ya thamani ya Sh.80,000 serikali inaambulia Sh. 2400 tu; sawa na asilimia 3. Zaidi ya hivyo, serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi kwa wawekezaji wa nje kwa kile kinachoitwa kuwavutia wawekezaji.

Katika mazingira hayo, haielekei kuwa, mwananchi mlaji atahurumiwa aepukane na mzigo huu wa kodi ya "wind fall profit".

Hata hivyo muhimu hapa kufahamika ni kuwa, kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, sio inayomuathiri zaidi mwananchi, bali mfumo wa kodi kwenye bidhaa hiyo.


Afisa upelelezi Moro ashutumiwa

BAADHI ya waumini wa Kiislamu wa mjini Tanga wameishutumu vikali kauli ya Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Morogoro (RCO), Steven Ngowi aliyetaka wasomaji, wachapishaji na wauzaji wa kitabu kitukufu cha Qur'an wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Waumini hao wamedai kuwa kauli ya Bw. Ngowi imekashifu na kudhalilisha Waislamu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti hivi karibuni, waumini hao wamesema hawakutegemea kiongozi wa chombo cha serikali kutoa kauli kama hiyo kwa vile imelenga kuwakashifu Waislamu.

"Tunashangaa kuwa Ngowi amewashitaki wale waliosema Yesu si mwana wa Mungu kwa madai ya kufanya kashfa wakati yeye anatoa kauli ya kashfa vile vile dhidi ya Waislamu", alisema mmoja wa waumini hao aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Mwakuruzo.

Muumini huyo alisisitiza kuwa kauli ya kutaka wasomaji, wachapishaji na wauzaji wa Qur'an wakamatwe na kushitakiwa kwa madai kuwa kitabu hicho kinakashifu imani za wengine ni kashfa kwa Waislamu.

"Hatutaki kuongea mengi kwa vile kesi hii ipo mahakamani, lakini Bw. Ngowi aelewe kuwa kauli yake haiwezi kuachwa hivi hivi bila kujibiwa...".

Muumini mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema licha ya Bw. Ngowi kukashifu Uislamu inaonesha upendeleo wa kidini hasa kwa kuzingatia kuwa imetolewa na kiongozi wa chombo cha serikali inayodai kuwa haina dini.

"Kama Qur'an na Biblia zinatofautiana kuhusu Yesu kuwa au kutokuwa mwana wa Mungu, kwanini wakamatwe wachapishaji wa Qur'an tu na isiwe wa Biblia. Ngowi anataka kutuambia kuwa Ukristo ndio dini pekee?", alihoji.

Hoja ya kutaka wasomaji wachapishaji na wauzaji wa Qur'an wakamatwe ilitolewa na Afisa huyo wa polisi mjini Morogoro wakati akitoa ushahidi katika mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Morogoro katika kesi ya kufanya mihadhara bila kibali na kunukuliwa na gazeti hili hiki iliyopita.

Kesi hiyo inawakabili wahubiri wa kikundi cha AL-MALLID tawi la Morogoro.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook