Kuporwa kwa shule ya Moshi Muslim:
Manispaa yazua uzushi


UZUSHI hauwezi kuinasua CCM kutokana na kitanzi ilichojitia shingoni.

Hayo yamesemwa na waumini kadhaa mjini Moshi kufuatia propaganda inayopigwa dhidi ya juhudi za kuihami shule ya msingi Mwenge.

"Wamezoea kutudhulumu kisha walete visingizio. Mwembechai waliua, wakasingizia Balozi za nje, wakamtia kilema Chuki Athumani wakamsingizia kuwa na makaratasi ya uchochezi, sasa wanapora shule yetu wanasingizia Cuf" amesema Bw. Shuayb Msechu.

"CCM na serikali yake isijidanganye. Inatambua dhulma inazowafanyia wananchi.

. Kuleta uzushi wa kuisingizia Cuf hakutawafanya Waislamu waache kuipigania shule yao", amesema Bw. Hashim Hassan wa Maboghini;na kuongeza, kama ni 'kuhongwa wao ndio wamezoea kutumiwa na Kanisa Katoliki kuzuia ujenzi wa misikiti'.

Imeelezwa kuwa uongozi wa manispaa, unadai; yapo mapesa yaliyomwagwa kuzuia shule hiyo isifanywe "English Medium School".

Katika maelezo hayo imedaiwa kuwa uongozi wa manispaa umetuhumiwa na Mkuu wa Mkoa Mh. Philemon Sarungi kutaka kuiangusha CCM kwa kuleta agenda zisizokuwa na ridhaa ya wananchi.

Imeelezwa katika kujitetea mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa manispaa alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa wananchi walishirikishwa "ila tatizo ni kuwa Cuf imemwaga fedha nyingi.

Wakati huo huo imeelezwa kuwa, Waislamu walikutana Masjid Riadha mwishoni mwa wiki ambapo walipitisha azimio la kutoyumba katika kudai shule yao ikiwa ni pamoja na ukumbi wa mikutano. Wamesema, maadhali ukumbi huo ulijengwa kama Wakfu hautouzwa wala kubadilishwa.

Imefahamika kuwa, Mkurugenzi wa Manispaa Moshi alikuwa amepeleka hundi ya Sh. Milioni nne kwa Bakwata kumalizia malipo ya ununuzi wa ukumbi huo. Hata hivyo Katibu wa Bakwata Bw. Rashid Malya amewaeleza waumini kuwa alikataa kuipokea hundi hiyo.

Halmashauri Kuu ya Bakwata Mkoa inatarajiwa kukutana kesho kujadili pamoja na mambo mengine, hatma ya suala hili.


Waanzisha umoja wa kusaidiana

WAISLAMU kadhaa mjini Dar es Salaam wameanzisha umoja wa kusaidiana wakati wa neema na matatizo ili kujikwamua katika umaskini na matatizo.

Habari zilizopatikana mapema wiki hii zilieleza kuwa umoja huo unaitwa United Muslims Brotherhood na ofisi zake ziko huko Kinondoni Ananasif ambako taratibu za kusajili umoja huo zipo katika hatua ya mwisho.

Imeelezwa kwamba madhumuni ya kuwa na umoja huo ni kusaidia Waislamu wanachama wenye matatizo ya kifedha, kufarijiana (kifedha) mwanachama anapopata msiba au majanga yoyote yasiyokuwa ya kawaida.

Aidha, umoja huo umeelezwa unajishughulisha na kuwapatia misaada na mikopo Waislamu wanachama wanapokwama katika kuanzisha miradi ya kujitegemea na kuwatafutia nafasi za kujiendeleza wale ambao wanahitaji kusaidiwa.

Imeelezwa kwamba Waislamu wenye nia ya kujiunga na umoja wanakaribishwa bila masharti ili kujipatia maendeleo ya maisha.

Mmoja wa viongozi wa umoja huo Bwana Mahmoud amesema kwamba wanatarajia kuanzisha maktaba ya kujisomea taaluma za Kiislamu na kutafuta eneo maalum la kujenga ukumbi ambako Waislamu watautumia kufanya mambo ya kheri na kubadili mawazo, sherehe na michezo ya halali.

Amefafanua kuwa Makao Makuu ya muda yapo Kinondoni Ananasif karibu na shule ya msingi Ananasif jijini. Katiba ya chama hicho imeshawasilishwa kwa Kabidhi Wasii kwa usajili.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook