Pumbao la kisiasa lililokuwa limewazuga Waislamu kuwa dini ni mbali na siasa ukurasa wake unatazamiwa kufungwa, Uislamu kama
itikadi isiyowachelea watawala wanaodhulumu raia utakapofafanuliwa na wahadhiri.
Aidha, Salamu 'zitapelekwa' kwa Rais Mkapa kuhoji udhalimu wanaofanyiwa Waislamu.
Damu ya Waislamu iliyomwagwa Mwembechai itakuwa moja ya nukta muhimu katika salamu hizo.
Taarifa zinaeleza kuwa, kauli za baadhi ya maaskofu kuhusiana na uchaguzi wa mwaka huu pia zitafafanuliwa.
Mmoja wa waandalizi wa hafla hiyo Bw. Mussa amesema, baadhi ya viongozi wa makanisa, wameshatoa maelekezo kwa waumini wao wachague watu gani oktoba.
Bwana Musa amesema mmoja wa viongozi hao amenukuliwa na vyombo vya habari akisema:
" Katika uchaguzi ujao tunataka kuona tunapata viongozi toka ndani ya Kanisa, tunataka Ma DC na wakuu wa mikoa wawe watu wa kanisa, hata Rais na uongozi mwingine.
Kauli kama hiyo inapotolewa na Askofu, si ya kupuuzwa amesema Bw. Mussa.
"Itabidi Waislamu watakapokutana Jumapili Msikiti wa Tungi waitafalkari", alisisitiza.
Aidha amesema yapo makundi ya akinamama kutoka makanisani jijini ambayo nayo yameanza kampeni za Oktoba kwa misingi ya dini.
"Yote hayo lazima waislamu wayajadili, amesema.
Ni kwa ya pili katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja Waislamu nchini wanakutana kujadili hali yao kisiasa na kijamii, safari hii ikiandamana na maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu. Jijini Dar es Salaam waumini watajumuika kwa wingi katika Msikiti wa Tungi ulioko wilaya ya Temeke.
Mjini Morogoro wanawake wa Kiislamu watakusanyika kesho (Jumamosi) katika Msikiti wa Mafiga kutafakari mambo mbalimbali yaliyojitokeza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa msemaji wa kamati ya maandalizi, sherehe za jijini zinatazamiwa kutanguliwa na dhafa ambayo waumini hao watazunguka mitaa mbalimbali ya Jiji kuelekea Msikiti wa Tungi kuhitimisha shughuli alasiri ya siku hiyo.
Msemaji huyo amelifahamisha gazeti hili kuwa mambo yatakayojadiliwa sehemu zote mbili ni pamoja na tukio la hivi karibuni ambapo Afisa Upelelezi Mkoa Morogoro Bwana Ngowi alidai mbele ya Mahakama kuwa waandishi wa Qur'an wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwa kuwa kitabu hicho kinakashifu imani za wengine.
Akiungana na Afisa huyo, naye Hakimu alidai kuwa hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa Qur'an ni kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Tofauti na ilivyokuwa mwaka jana wakati wa maadhimisho haya, mwaka huu jumuiya na taasisi zote za Kiislamu zimeungana katika kuandaa hafla hiyo.
Wawakilishi wa jumuiya hizo wamelieleza gazeti hili lengo la hatua hiyo ni kuimarisha mshikamano wa Waislamu katika kipindi hiki ambapo nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
"Tungependa Waislamu wawe na uamuzi wa pamoja juu ya nani ambao wangefaa kuwapa kura zao ili waongoze nchi hii", amedai Bwana Yasin Idd mwakilishi wa jumuiya moja yenye makao yake wilaya ya Ilala Jijini.
Aidha, imeelezwa kuwa madhila mbalimbali yanayosemekana kwa hufanyiwa Waislamu yatajadiliwa kwa urefu na wale watakaopata fursa ya kuzungumza siku hiyo.
Katika madhila hayo, limo suala la Mwembechai ambalo hadi leo serikali iliyoko madarakani imeshindwa kulipatia ufumbuzi.
Kushindwa huko kwa serikali kumekijengea chama cha CCM udui ambao huenda ukakigharimu katika uchaguzi ujao.
Viongozi wa shughuli hizo wamesema wamedhamiria
kuwapa maelekezo waumini wa dini hiyo ya namna ya kuondokana na madhila
yanayowakuta kwa kutumia fursa ya demokrasia mwezi Oktoba mwaka huu.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |