WITO umetolewa kuwataka polisi waache kuwafanyia raia vitendo vinavyoweza kuamsha hisia za kujitetea dhidi ya chombo hicho cha dola.
Aidha Jeshi hilo likiwa chombo cha Dola chenye wajibu wa kulinda usalama wa raia wote, limetakiwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na malalamiko mengi dhidi ya jeshi hilo kwamba limekuwa chombo cha kuwaonea na kuwadhulumu raia badala ya kuwalinda.
Malalamiko hayo ni pamoja na kutumika ovyo risasi za moto ambako kumesababisha mauaji ya raia wasio na hatia.
Aidha raia wamekuwa wakikamatwa, kuteswa na kurundikwa mahabusu kwa muda mrefu kisha kuachiwa huru.
Waliokumbwa na mikasa hiyo ni pamoja na vijana wapiga debe katika mabasi ya daladala, Waumini wa dini ya kiislamu, wafuasi wa vyama vya upinzani na vijana wanaodaiwa kuwa ni wazururaji.
Wimbi hilo la ukiukaji wa sheria na kanuni za jeshi hilo, limesababisha polisi kuonekana adui wa raia kinyume na madhumuni ya kuwepo kwao kijamii.
Ukiukaji huo wa sheria hivi sasa unaonekana kuchukua mkondo ambao huenda ukasababisha machafuko siku za usoni iwapo mtindo wa kupongezana na kulindana unaodhaniwa kuwepo ndani ya jeshi hilo hautakomeshwa.
Matukio ya hivi karibuni Jijini na kule Zanzibar wananchi wengi wameyaeleza kuwa ni matokeo ya uonevu wa jeshi hilo dhidi ya baadhi ya raia ambao sasa inaonekana wanalazimika kujitetea.
Akielezea tukio lililotokea Kurasini Jijini, Mzee mmoja anaeishi eneo la Kariakoo, amesema vurugu iliyotokea ilisababishwa na maaskari wawili wa usalama barabarani ambao alisema waliyasimamisha magari yaliyowachukua wafuasi wa chama cha CUF waliokuwa wakielekea mkutanoni.
Mzee huyo aliendelea kueleza kuwa maaskari hao baada ya kuyasimamisha magari hayo walichukuwa leseni za madereva wake wakidai magari hayo yalibeba abiria wengi.
"Hizi hazikuwa daladala ni magari yaliyochukuwa wanachama kuwapeleka mkutanoni kama ambavyo watu hujazana katika magari kwenda mazikoni au kwenye sherehe", alidai mzee huyo na kuongeza kwamba chama tawala kimekuwa mara zote kikibeba wakereketwa wake toka eneo moja hadi jingine.
" Hatujasikia CCM ikiulizwa leseni na kujaza watu katika mgari, iweje kwa CUF iwe nongwa, lipi la ubaya kwao kama si woga wa kisiasa, alihoji kwa mshangao Mzee huyo.
Vitendo kama hivyo vimekuwa vya kawaida kufanywa na polisi kwa visingizio vya kutekeleza majukumu yao.
"Kama chombo kinachopaswa kuwalinda raia na mali zao kinageuka kuwanyanyasa na kuwaonea, wakimbilie wapi kama si kuamua kujitetea wenyewe, amehoji Afisa mstaafu wa jeshi hilo ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.
Akizungumza na maafisa wa polisi katika ukumbi wa FFU mjini Zanzibara juzi, Inspekta Generali wa polisi Omar Mahita aliripotiwa kutoa onyo dhidi ya raia wanaoamua kupambana na polisi.
Bwana Mahita alitoa vitisho hivyo kufuatia kujeruhiwa kwa polisi watatu waliotaka kufanya kazi zao kwa kuvamia mkutano wa ndani wa chama CUF.
Hata hivyo katika hotuba yake bwana Mahita hakugusia chochote juu ya watendaji wa jeshi hilo wanaokiuka sheria hali ambayo huenda ikachochea uonevu zaidi dhidi ya raia.
Wananchi wengi waliohojiwa na gazeti hili
kufuatia matamshi ya Kamanda Mahita, wamesema huenda ni dalili kuwa chama
tawala kinajenga mazingira ya kutumia nguvu ya dola kudhibiti wapinzani..
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |