Bakwata Tanga yadaiwa kuzorotesha maendeleo

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Bibi Salma Kauli amewashutumu viongozi wa Baraza hilo kwa kusababisha kuzorota kwa maendeleo ya wanawake kielimu hapa nchini.

Akizungumza na viongozi wa kidini na wazee wa mji wa Pangani mkoani Tanga hivi karibuni, Mwenyekiti huyo aliwataja viongozi wa BAKWATA kuwa na ubinafsi na ukiritimba, jambo ambalo limekwamisha maendeleo ya wanawake wa Kiislamu kielimu.

"Kuwa nyuma kielimu kwa wanawake wa Kiislamu kumechangiwa na ubinafsi na ukiritimba wa viongozi wa BAKWATA ambao wameshindwa kuwahamasisha na kuwashirikisha Waislamu katika mambo mengi ya maendeleo", alisema.

Alisema kwa vile chombo hicho ndicho kinachotambuliwa na serikali kuwa ni cha Waislamu, mipango mingi ambayo ingeleta maendeleo kwa Waislamu imekuwa ikifikishwa kwenye Baraza hilo lakini kutokana na ubinafsi wa viongozi wake imekuwa ikikaliwa bila kufanyiwa kazi.

Ametoa mfano kuwa nafasi nyingi za masomo kwa wanawake zimekuwa zikitolewa kutoka nchi za Uarabuni na Ulaya na zinapofikishwa kwenye Baraza hilo viongozi huzifungia makabatini.

Akizungumza mbele ya Sheikh wa Bakwata wa Mkoa wa Tanga, Sheikh Juma Luwuchu, Bibi Salma aliwashutumu viongozi wa Baraza hilo kuwa wamekiuka haki ya wanawake kujiendeleza licha ya Uislamu kutoa kipaumbele kikubwa kwa wanawake kupata elimu.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook