INAVYOELEKEA Tanzania ikiongozwa na Serikali ya CCM ilikumbwa na wimbi la mageuzi bila kutazamia, kwa hali hiyo ililazimika kuikubali demokrasia ya vyama vingi kwa shingo upande.
Takwimu zilionesha zaidi ya asilimia 80 ya watanzania walitaka mfumo wa chama kimoja uendelee na ilikuwa asilimia 20 tu iliyotaka mfumo wa vyama vingi.
Kutokana na wimbi la mageuzi ya kisiasa la wakati ule ilionekana ni busara kufuata uamuzi wa "wachache " hivyo mfumo wa vyama vingi ukarudi kwa mara nyingine nchini.
Haraka haraka "Wapinzani" waliungana na kuanzisha chama cha upinzani dhidi ya CCM. Hata hivyo wengi wa wapinzani hao walikuwa ama wastaafu wa serikali au watu waliokuwa na " kazi maalum" wakijitokeza kama wapinzani.
Haikupita muda chama hicho cha upinzani kikakumbwa na migogoro ya uongozi hatimaye baadhi ya viongozi wakaamua kujitoa. Baada ya mgawanyiko huo ndipo wananchi waliposhuhudia kuibuka kwa utitiri wa vyama.
Harakati za kisiasa chini ya mfumo wa vyama vingi zilishika kasi mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu, baadhi ya vyama vikisaidiwa na wakongwe wa siasa au wanasiasa waliojiengua toka chama tawala vilielekea kubadili hali ya kisiasa ya nchi yetu.
Hata hivyo, ukongwe na uzoefu wa chama tawala katika medani ya siasa ulimudu kuwasambaratisha wapinzani ambao baadhi waliihama dunia muda mfupi mara baada ya kutangaza kuwania nafasi ya juu ya uongozi.
CCM ilikuwa na kila sababu ya kuvitaka vyama vya upinzani hasa upande wa bara vijiandae zaidi kuweza kupambana nayo na ilidhihirika hivyo kwa vyama fulani ambavyo vilishindwa hata kueleza vingefanya mambo gani mapya ambayo CCM hainayo, badala yake vilinadiwa na umaarufu wa mtu ua watu ambao kwa hakika walistahili kugutukiwa na wananchi kutokana na uwezo au muelekeo wao kisiasa.
Hivi sasa uwanja wa siasa unaelekea kuchukua mkondo mpya
Kuwania ruzuku au kubebana kisiasa hakuna nafasi tena. Wananchi wameanza kuelewa umuhimu wa kuwa na uongozi makini wenye kujua shida na mahitaji yao sambamba na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Kwa sababu hiyo vyama hewa vimetupwa mkono na vile vyenye sera au ilani(manifesto) za ulaghai vimeanza kujishuku.
Wananchi wameanza kupima kauli na matendo ya wale wanaosimama kuomba uongozi. Hawako tayari kuwapa fursa nyingine wanaoendelea kuwadhulumu kiuchumi na kijamii. Hawako tayari kuyumbishwa na sheikh au askofu, RTD, TvT au TvZ, mbinu zote iwe hotuba au mikopo ya kuanzishia biashara, zinazolenga kuwalaghai wamezibaini.
Huu ndio mwamko unaoelekea kufichua ukweli wa mambo juu ya hatima ya Tanzania katika demokrasia ya vyama vingi. Kwa kuliona hili watawala wameanza kutaharuki wakionesha sura halisi za kutokuwa tayari kuyapa fursa mabadiliko ya kidemokrasia.
Kutokuhiyari huko kumekuwa kukijidhihirisha katika kuvizuia baadhi ya vyama kufanya mikutano ya hadhara, vyombo vya dola hutumika kutishia wafuasi au kuingilia kati harakati za kisiasa za vyama hivyo.
Mwezi mmoja uliopita, waziri mkuu akiwa ziarani kanda ya ziwa aliripotiwa kuwaonya wafanyibiashara wanaosaidia vyama vya upinzani wakati huo huo akitoa matumaini kwa wale wanaopeperusha bendera za CCM mbele ya biashara zao.
Kule Zanzibar hali ni mbaya zaidi ambapo viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani hususan chama kikuu cha upinzani nchini CUF, wamekuwa wakiishi kwa wasi wasi mkubwa kutokana na vitisho na unyanyasaji wa serikali ya chama tawala.
SMZ imekuwa ikijitokeza wazi wazi kuzuia harakati na shughuli za chama hicho kwa visingizio ambavyo kwa hakika vimekuwa vikiidharaulisha nchi yetu mbele ya mataifa mengine.
Wakati mwingine kukandamizwa kwa wapinzani kumekuwa kukihalalishwa na hata na vyombo vya sheria. Kesi ya uhaini iliyofunguliwa dhidi ya wanachama 18 wa CUF ni mfano hai wa namna madhila ya kisiasa dhidi ya wapinzani yanavyopata baraka za vyombo vya sheria Zanzibar.
Kesi ya watuhumiwa hao imekuwa kitendawili kikubwa ambapo hivi sasa haifahamiki hatima yake baada ya Jaji anayesikiliza shauri hilo kuwaona watuhumiwa wanashitaka la kujibu baada ya kutupilia mbali hoja ya upande wa utetezi.
Ile kudhaniwa tu ni mfuasi wa CUF Zanzibar inaelekea kuwa ni "kosa" la jinai mbele ya watawala ambalo huweza kumgharimu muhusika kazi yake, nafasi yake kazini, makazi au biashara yake!
Ipo mifano mingi inayoonesha watu kubomolewa nyumba au makazi yao kwa sababu za kisiasa, wapo waliofukuzwa kazi au kuhamishwa na wapo waliobomolewa vibanda vya biashara au kuwekewa vikwazo kadhaa wa kadhaa.
Kilele cha kukandamizwa upinzani visiwani humo kimejitokeza hivi majuzi kwa kukamatwa katibu mkuu wa CUF bwana Seif Sharrif Hamad na wenziwe saba wakidaiwa kuwapiga polisi na kupora mali!
Tukio hili linadhahirisha zaidi kutokutakiwa mfumo unaohalalisha upinzani kwa chama tawala.
Mfululizo wa propaganda zinazoendeshwa dhidi ya baadhi ya vyama vilivyodhamiria kufanya mageuzi ya kweli ni hali nyingine inayotishia demokrasia nchini.
Baadhi ya vyama vimedaiwa kuwa vya kidini, vya kikabila au kuwa na ajenda zenye lengo la kuwagawa Watanzania!
Matamshi yasiyo na ushahidi yamekuwa yakitolewa kupitia vyombo vya habari dhidi chama fulani. Lengo likiwa ni kukifitinisha kwa wananchi. Mara nyingi vyombo hivyo vimeshindwa kuripoti hata mikutano ya hadhara kama inavyofanywa kwa vyama vingine.
Kwa upande mwingine zipo jitihada za makusudi zinazofanywa na watawala zinazoashiria kutaka kudhibiti maamuzi ya kidemokrasia.
Suala la waraka namba moja lililozaa mabadiliko ya 13 ya katiba ya jamhuri ya muungano, halina tafsiri nyingine kinyume na ile ya kukandamizwa demokrasia nchini.
Mtiririko wa yote hayo hauna ishara njema kwa wapiga kura wa nchi hii. Huenda gharama za uchaguzi Mkuu Oktoba matokeo yake yakawa hadithi za Esopo.
Kwa hali hiyo ni bora zaidi ingetamkwa kwa
niaba ya wananchi kuwa mfumo wa vyama vingi hautakiwi nchini kwetu, CCM
ni muungano wa vyama vilivyoleta uhuru, kwa hiyo ndio chama pekee chenye
haki ya kuongoza nchi hii daima dumu!
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |