MOTO ni rasilimali muhimu mno kwa maisha ya wanadamu. Kimsingi, mojawapo ya kanuni za uhai wa viumbe ni mwanga ambao unatokana na jua ambalo, kihalisia ni moto. Kitabu kitukufu cha Waislamu kinaliita jua "taa ing'arayo na yenye joto kali yaani siraja kwa lugha ya Kiarabu. Sayansi imekiri kuwa neno au jina hilo ndilo hasa linalowakilisha umbile la jua kwa uhalisi wake. Mwandshi S. Husein anafafanua
Pamoja na ukali wa jua, bado kiwango cha mwanga na joto kianchopatikana hapa duniani kinawiana na mahitaji ya viumbe vilivyopo. Hii inatokana na ukweli kwamba kiwango hicho kimekadiliriwa na Muumba kwa manufaa ya viumbe.
Haiyumkini kabisa kuwa jua liwe limejikadiria lenyewe kiasi hicho cha mwanga na joto kwa maisha ya viumbe vya duniani. kijiografia, zipo sayari nyingine ambazo zinapata joto au mwanga ambao haufai kabisa kwa maisha ya viumbe waliopo duniani.
Kama mpango wa maumbile ungekuwa wa bahati nasibu kama wanavyodai makomredi wa itikadi ya kimaksi, basi viumbe vya dunia hii visingekuwepo kama hali ya hewa ya sayari yetu ingekuwa kama ile ya sayari ya Mekyuri. Au kama, "kwa bahati mbaya" Baba yetu Adam na mama yetu Hawa wangeangukia kwenye sayari hiyo, basi ulimwengu wa wanadamu usingelikuwepo.
Wataalamu wanatuambia, laiti jua lingesogea mbali kidogo tu kutoka pale lilipo basi tungeganda kwa barafu na laiti lingekaribia kidogo tu, sote tungeyeyuka kwa joto.
Kwa hali hiyo, jua halipo pale kwa bahati nasibu kama inavyodaiwa na nadharia za Kimarx , bali limewekwa pale kwa mahesabu ya uhakika kwa ajili ya uhai wa viumbe.
Aidha, jua ndilo linalotupatia nuru kupitia mbalamwezi. Qur'an inauita mwezi 'Nur' kwa maana ni 'chombo' kinachoakisi mwanga au nuru. Pamoja na kazi nyingine nuru hiyo ya jua kupitia mbalamwezi husaidia macho yetu kuona nyakati za usiku.
Kimaumbile, macho yetu hayawezi kufanyakazi gizani. Mtu anapokuwa gizani hulazimika kupapasa kama kipofu japo yu anamacho. Ni kwa sababu hii watu wanahoji kama mwanga usingekuwepo maisha yetu yangekuwaje?
Watu wanaotumia akili zao wakiwemo wanasayansi wanahoji kuwa, macho yalijuaje kuwa duniani kuna mwanga utakaoyawezesha kuona. Na mwanga nao ulijuaje kuwa duniani kuna macho yanayohitaji mwanga ili yaweze kufanya kazi na huo mwanga uliwezaje kujikadiria kwa kiwango kinachowafikiana na macho.
Kwanini haukuwa mkali kiasi cha kuathiri macho au kwa nini haukuwa hafifu kiasi cha kutoyawezesha macho kuona?
Vile vile nishati ya jua ni muhimu mno kwa maendeleo ya teknolojia. Kuna vifaa mbalimbali vinavyotegemea nishati hiyo.
Kwa ujumla rasilimali ya moto kupitia vyanzo mbalimbali imechukua sehemu muhimu katika maisha na shughuli zetu za kila siku. Vifaa vya nyumbani kama taa, jiko, redio, feni, friji, jokofu, pasi, televisheni na kadhalika vyote vyahitaji moto.
Vifaa vya hospitali, maofisini na katika sehemu mbalimbali za kazi kama mashine, mitambo, x-ray, viyoyozi, kompyuta na vinginevyo vyote vyahitaji moto. Halikadhalika vyombo vya usafiri kama gari, treni, ndege, meli, boti, pantoni, pikipiki, skuta na trekta vyote vinatumia moto. Kwa hiyo, kila binadamu kwa namna moja au nyingine lazima atumie moto.
Hata hivyo, pamoja na manufaa yake, moto ni moja ya vyanzo vikuu vya maangamizi ya mali na maisha ya wanaadamu. Moto umekwishamletea mwanadamu hasara kubwa kwa namna nyingi. Mbali na majanga ya mioto ya umeme, mkaa, kuni, gesi, stova, mchina, pia majeshi ya nchi mbalimbali duniani yameangamiza mali na maisha ya watu kwa kutumia moto ima kwa mabomu, makombora au risasi.
Kutokana na manufaa na hatari ya moto ndio maana Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'an:
"Je, mnauona moto ambao mnauwasha, je, mti wake mmeumba nyinyi au sisi ndio tuliouumba? Sisi tumeufanya kuwa ukumbusho wa moto wa Akhera na manufaa kwa viumbe". (56:71-73).
Hakuna binadamu asiyejua moto mijini na vijijini. Kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu katika aya hiyo anatutaka tuuchukulie moto huo tunaoutumia kila mara kama ukumbusho wa moto wa Jahanamu.
Jinsi tunavyojihadhari na moto wa dunia ndivyo hivyo tunavyotakiwa tujihadhari na moto wa Akhera. Sote kwa namna moja au nyingine tumekwishashuhudia au kupata madhara ya moto.
Hivi karibuni yametokea matukio ya kutisha yaliyohusisha moto. Moja limetokea katika nchi jirani ya Uganda ambako mamia ya watu wameteketezwa kwa moto katika Kanisani la wana maombi.
Na lingine limetokea mkoani Mbeya ambako makumi ya watu wamekufa kwa kuteketezwa na moto na wengine kujeruhiwa vibaya.
Matuko yote yamepewa uzito maalum na vyombo vya habari. Ni hakika ya kimaumbile kuwa yeyote aliyeona au kusikia maafa hayo alizidi kupata hisia za kuuogopa moto.
Watu wa kijiji kilichofikwa na msiba wa moto Mbeya ndio waliopata maumivu zaidi ya kihisia kwani wameshuhudia wenzi wao waliowajua kwa majina na viwiliwili wakiitwa majivu pasipo kutambua nani alikuwa nani. Ilibidi mazishi yashirikishe watu wa imani zote.
Aidha, mtu asiye na moyo wa ujasiri asingeliweza kuwatazama wale majeruhi jinsi walivyoungua. Na hata mtu mwenye moyo mgumu kwa vyovyote aliathirika kihisia kwa kuiona miili ya watu namna ilivyobabuka ngozi. Mkuu wa Wilaya alitoa hotuba iliyokuwa na hisia kali kutokana na janga lile la moto.
Madaktari huwa mahodari sana wa kuficha ukweli juu ya uhai wa mgonjwa lakini hawakusita kusema kuwa, kwa kiwango walichoungua baadhi ya majeruhi hao, ambacho ni zaidi ya asilimia sitini, isingewezekana kwao kuendelea kuishi.
Kwa mujibu wa aya ya Qur'an tuliyoinukuu, ule moto wa betri uliolipua lori la mafuta, ulikuwa muhimu kwa lori hilo. Kutokana na betri, gari hufanya kazi na kumpatia faida mmiliki wake. Pia wafanyakazi hunufaika.
Isitoshe yale mafuta yaliyobebwa na lori hilo yalikuwa muhimu kwa matumizi mbalimbali. Laiti yangefika kule yalikokusudiwa yangewanufaisha wahusika kwa njia mbalimbali.
Lakini madhara ya moto ule wa betri hilo tumeyaona na mwenye lori kapata hasara, mwenye bidhaa kapata hasara na waliotaka kuiba wao wamepata hasara kubwa zaidi.
Kwa hiyo, waliofikwa na janga hilo (ukiacha waliokufa), walioona na tuliosikia kwa pamoja tumepata ukumbusho wa madhara ya moto. Japokuwa moto twautumia kila siku lakini mwanadamu ni kiumbe anayejisahau sana. Hivyo matukio kama haya yatusaidie kukumbuka adhabu ya moto wa Akhera.
Ifahamike kuwa huu moto tunauouna duniani haulingani kwa ukali na moto wa Akhera. Ukali wa moto wa Akhera hauna kifani. Tangu hapo huu moto wa duniani haukukusudiwa uwe adhabu bali kama aya ilivyobainisha umeumbwa kwa manufaa yetu.
Moto wa Akhera wenyewe umeumbwa makhususi kwa adhabu. Adhabu ya chini sana ya moto wa Akhera ni kali mno kuliko ile ya moto uliowateketekeza watu Mbeya. Tofauti na moto wa dunia ambao mwisho wake ni kumuua mtu na kumfanya majivu, moto wa akhera ni wa kudumu. Mtu hafi na hawi jivu.
"Na wale waliokufuru watakuwa na moto wa Jahanamu, hawatahukumiwa kufa wala wahawatapunguziwa adhabu ... (35:36)
Ikiwa tunapata maumivu kwa kuungua na njiti tu ya kiberiti au kuna misimu, huwa tunalalamika kuungua na jua kwa nini basi tusijihadhari na moto wa milele wa Jahanamu?
Kuna watu wanaojidanganya kuwa hakuna moto na pepo bali ni imani tu. Hawa jibu lao ni fupi tu kuwa Mwenyezi Mungu aliyeumba jua kama nilivyokwishaeleza awali, ndiye huyo huyo aliyeumba moto. Kama Mungu angetaka, basi angelishusha jua chini, lingetosha kuwa Jahanamu.
Au angetaka, angewatupa waovu kwenye sayari ya Mekyuri ambayo tayari wanadamu wamekwishaiona, ingetosha kuwa 'Jahanamu', lakini jua, pamoja na ukali wake, haliwezi kufananishwa na moto wa Jahanamu. Mbali na moto ndani ya jahanamu kuna adhabu nyingine.
Mwanadamu anapohisi ukali wa jua, hukimbilia kivulini. Sasa aliyeumba kivuli ndiye huyo huyo aliyeumba pepo. Lakini pepo ni tofauti na kivuli kwani kivuli mtu anaweza kupumzika bila kustarehe lakini peponi kuna starehe zisizo na mfano na aingiae lazima apate starehe "Hakuna tabu wala kuchoka" (35:35).
Vile vile Mungu aliyeumba joto na ubaridi ni sahali kwake kuumba moto na pepo. Hii ni mifano tu ya kumsaidia mtu kutanabahi. Mara nyingi binadamu huwa mbishi kuamini kitu mpaka akione kwa macho. Lakini mbona kuna vitu vingi ambavyo hatuvioni kwa macho yetu. Nani anaiona Oksijeni.
Lakini tofauti na vitu hivyo ambavyo twaweza kuviona au kuvihisi kwa kutumia nyenzo za kisayansi, moto umefichwa na tutauona baada ya kifo, siku y siku ikifika, Mungu atasema:
"Basi hii ndiyo jahanamu mliyokuwa mkiahidiwa. Ingieni leo kwa sababu ya ukafiri wenu". (36:63-64)
Baada ya kuingia humo, wahusika watalia wakisema:
"Mola wetu! Tutoe motoni (uturejeshe duniani) tutafanya vitendo vizuri visivyokuwa vile tulivyokuwa tukifanya. (Mwenyezi Mungu awaambie): "Hatukukupeni umri wa kuweza kukumbuka mwenye kukumbuka?"
Kwa hiyo, tusisubiri kuuona moto ndipo tuamini bali tujihadhari nao kabla ya kifo.
Wapo wengine wanaoulizia kuwa itawezekanaje ule mwili unaozikwa kaburini ambamo unaoza na kuliwa na wadudu uje ufufuke siku moja. Vivyo hivyo wengine huuliza kuwa wale watu walioteketezwa kwa moto hadi kuwa majivu watawezaje kufufuliwa? Wapo hata wanaodhani kuwa kwa kuzichoma moto maiti zao, basi wao wamekosa na Mungu kakosa.
Hawa wote wanashindwa kuelewa jambo moja kuwa mtu sio kiwiliwili. Kiwiliwili ni jumba tu linalomfunika mtu kama bodi la gari linavyofunika injini.
Hebu mtu ajiulize kwa nini watu husema fulani hayupo nasi tena duniani wakati mwili wake upo yaani haujazikwa. Hii ni kwa sababu yule mtu ameondoka wao wanabaki na gamba tu lililokuwa limemuhifadhi "yule mtu".
Ndio maana ndugu na jamaa, pamoja na mapenzi makubwa waliyokuwanayo kwa ndugu yao, bado anapokufa, humfukia ardhini au wengine ndivyo hivyo humchoma moto. Yote ni kwa sababu waliyekuwa wakimpenda ameondoka na laiti angalikuwepo wasingethubutu kumfukia au kumchoma moto.
Au kwa nini watu wamlilie fulani wakati mwili wake wako nao mikononi. Kwanini wasifarijike kwa kuutazama mwili huo na badala yake wanahuzunika zaidi wanapouona!
Hiyo maana yake ni kwamba, ule mwili sio mtu, bali unamilikiwa na mtu. Mtu ajiulize kwamba anasema "kichwa changu, mguu wangu au tumbo langu". Huyu anaemiliki viungo hivi ni nani wakati kila kiungo mwilini kina haki ya kujimiliki chenyewe kulingana na umuhimu wake.
Mkono unapovunjika hausemi "mimi mkono nimevunjika bali "mwenyewe" ndiye anayesema "mkono wangu" umevunjika. Au badala ya tumbo kusema "ninaumwa, "mmiliki" husema "tumbo linaniuma" au kichwa kinaniuma. Sasa tumtafute huyu anayemiliki kama kweli tutampata, maana yake hatujui mahali anapokaa mwilini!
Itaendele toleo lijalo
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |