Rufiji: Bonde lililopo kati ya huzuni na tabasamu


BONDE la mto Rufiji linajumla ya kilomita 177,000 za mraba, sawa na asilimia 20 ya eneo zima la nchi hi inayopigania "ukiriri" wa ufakara.

Bonde la Rufiji lenye uwezo wa kulisha Afrika Mashariki nzima endapo litatumiwa vizuri na mamlaka husika limetandawaa katika mikoa ya Pwani, Lindi, Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Dodoma na Singida!

Bonde hili lina utiriri wa rasilimali ambazo ni chachu ya uchumi wa nchi hii. Kwa mujibu wa taarifa za shirika la Chakula na Lishe (FAO) kuna hekta zisizopungua 622,622,400 zifaazo kwa kilimo cha kiangazi (cha umwagiliaji) katika bonde lote la mto Rufiji. Ambapo bonde la Usangi limemega hekta 208,000 kati ya hizo, Ruaha napo pakameza hekta 5,800 huku Kilombero paliichukulia hekta 329,600 na Rufiji chini yakiwa na hekta 70,000.

Cha kusikitisha na kushangaza ni kuwa bonde hilo bado kabisa halijaguswa itakikanavyo kwa madai kuwa eti uwezo wa Taifa wa kugharamia "miradi mikubwa" ya umwagiliaji ni mdogo hasa ikizingatiwa kwamba miradi hiyo inahitaji "fedha nyingi" za kigeni kununulia zana za kilimo.

Aidha, hoja nyingine inayotolewa na mamlaka husika (Rufiji Basin Development Authority - RUBADA) ni kuwa eti, nchi hii ina upungufu wa wataalam wenye ujuzi na uzoefu wa muda mrefu wa kuendesha mashamba ya umwagiliaji! Hata hivyo, mamlaka hiyo inakiri kwamba tatizo hilo linazidi kupungua jinsi miaka inavyokwenda lakini haioneshi kivitendo ukweli wa kauli hiyo.

Cha kujiuliza zaidi juu ya hoja hizo mbili ni kuwa endapo serikali inaweza kuikarabati Ikulu kwa mabilioni ya shilingi, kununua magari ya anasa na kuwajengea makasri ya kifahari "waheshimiwa" vipi ikose fedha za kuendeleza kilimo cha kiangazi katika bonde hilo ambalo sehemu zake nyingi hazihitaji mitambo yoyote ya gharama kubwa, kwani umwagiliaji wake ni wa nguvu za mtiririko wa maji?

Kuhusu hoja ya wataalamu haikubaliki kwa kuzingatia kuwa moja ya maeneo yaliyopitiwa na bonde hilo kuna Chuo Kikuu cha Kilimo chenye wataalamu wa kutosha "eneo husika" wenye uzoefu wa kutosha na ujuzi wa hali ya juu na bila shaka wanafahamu vilivyo mazingira halisi ya bonde la mto Rufiji.

RUBADA pia inatoa hoja ya mafuriko ya mara kwa mara yanayoyakumba maeneo makubwa ya bonde hilo hususan Rufiji chini kuwa ni kikwazo kingine cha kuendeleza kilimo cha kiangazi bondeni hapo ukizingatia kuwa uzuiaji wa mafuriko ni kitu cha lazima katika kuasisi na kuendeleza kilimo cha kisasa cha umwagiliaji maji, uzuiaji ambao unahitaji matuta makubwa chini ya vifaa vya gharama kubwa toka ng'ambo!

Aidha, mamlaka hiyo inaongeza kwamba njia za usafiri nazo ni tatizo lingine linalokwaza uendelezaji wa kilimo katika mabonde hayo na pia kukifanya kilimo cha kiangazi bondeni Rufiji kuwa cha gharama kubwa ukilinganisha na maeneo mengine!

Pia hoja nyingine inayokwaza kilimo hicho katika eneo hilo inatajwa kuwa ni pamoja na ndege na wanyama waharibifu hususan nyani, viboko, tembo na nyati ambao ni wengi katika maeneo ya bonde hilo lililokusanya misitu minene na hifadhi za wanyama za Selous, Rungawe na Ruaha zenye vivutio kadha wa kadha vya utalii vyenye uwezo wa kuingiza maelfu kila uchao yatakayowezesha kugharamia uendelezaji wa sekta nyingine katika bonde la mto Rufiji.

Tukiziangalia kwa kifupi hoja zote hizo kengeza zilizotolewa ambazo zinadaiwa kukwaza kilimo cha kiangazi bondeni Rufiji tunagundua kwamba msingi wa kudumazaa maendeleo ya bonde hilo pamoja na mambo mengine ni ukosefu wa mipango bora endelevu ya kilimo nchini na uchache wa ubunifu wa viongozi husika. Kwani rasilimali zilizoko katika bonde hilo pekee kama vile uvuvi, mbuga za wanyama, misitu na mazao yake, vivutio vya kihistoria zinatosha kabisa kugharamia sekta ya kilimo cha kiangazi katika bonde hilo.

Rasimali nyingine ni maeneo yafaayo kabisa kuzalisha umeme utokanao na nguvu za maji kwa nchi nzima.

Katika eneo hilo kuna vituo visivyopungua tisa viwezavyo kutoa umeme mwingi kama vile Stiegler's Georger kiwezacho kutoa Megawati 1,400, Ruhudji megawati 685, Mnyera megawati 485, Kilombero megawati 464; Kihansi megawati 288, Mpanga megawati 160, Lukose megawati 130 an Iringa megawati 87.

Vingi kati ya vituo hivyo vipo katika bonde la Kilombero.

Tangu miaka 10 iliyopita kuna miradi michache tu ya umwagiliaji ambayo ulianzishwa kwa jazba na kuendeshwa kwa vishindo katika bonde hilo, miradi ambayo sasa kama si baadhi yake kufa iliyobaki ingali inasuasua isipokuwa michache tu ndiyo inayokwenda vizuri.

Miradi hiyo ni pamoja na shamba la mpango la Mbalali lenye ukubwa wa hekta 32,000 na shamb la Mwakilombero lilomeza hekta 8,400 tu. Zaidi ya hapo katika kipindi hicho pia kulikuwa na mipango ya kuanzisha mashamba huko Kapunga hekta 5,700, Madibira hekta 7,890 na Ikwiriri 15,000. Mipango ambayo hadi hivi leo haijulikani ilipoishia, zaidi ya kuendesha miradi midogo midogo ya umwagiliaji hasa katika maeneo ya Usangu na Kalenga mkoani Iringa iliyokusanya hekta 300 tu!!

Itaendelea toleo lijalo.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook