BARUA


Mahita cheo ni dhamana, tekeleza wajibu

Ndugu Mhariri,

KAMANDA wa polisi nchini bwana Omar Mahita juzi alitoa matamshi mazito ambayo bila shaka yatakuwa ni maagizo kwa makamanda wa jeshi la polisi nchini.

Matamshi hayo yalifuatia purukashani iliyotokea katika ofisi za CUF eneo la Magomeni mjini Zanzibar baada ya polisi kuvamia na kutaka kuzuia mkutano wa ndani wa chama hicho.

Ningependa kumnukuu kamanda Mahita kama ifuatavyo"Tendo hili iwe mara ya mwanzo na mwisho, atakaerudia hili jambo basi litakalomfika basi asilie na mtu isije ikalaumiwa polisi kwa hatua hizo na yeyote, hata wakienda kwa mabwana zao wanaodai Human Rights, Human Rights, maana wao jambo dogo tu wanakimbilia kwa mabwana zao".

Waliodaiwa kuwapiga na kuwazuia polisi wasifanye kazi zao ni pamoja na Bwana Seif Sharrif Hamad Katibu Mkuu wa chama cha CUF na wanachama wengine saba wa chama hicho.

Matamshi ya kejeli ya Kamanda Mahita yana tafsiri gani, anataka kutuambia akiwa kiongozi wa jeshi la polisi hayatambui mashirika ya haki za binadamu duniani? Yaani kwake yeye AMNESTY, ARTICLE 19 si lolote si chote zaidi yakuwa mabwana wa vyama vya upinzani.

Na kama kuomba msaada fulani nje ya nchi ni kwenda kwa mabwana zetu, basi tuko wengi wenye mabwana huko ikiwa ni pamoja na viongozi wetu wakuu wa nchi ambao baadhi yao wamerudi hivi karibuni kutoka kwa nchi rafiki kuomba misaada.

Mabwana wengine hivi sasa wanatujengea mabarabara wakati huo huo wakitupa misaada ya chakula tusife njaa!

Kamanda Mahita sio mwanasiasa ambaye tungedhani anachukizwa na harakati za wapinzani, yeye ni Kamanda wa chombo cha Dola anaepaswa kutekeleza wajibu wake kama msimamizi wa usalama asiye na upande.

Kama ni kujeruhiwa polisi ndiko kulikomkasirisha je amesahau vitendo vya kinyama viliyofanywa na vijana wake dhidi ya raia Jijini Dar es Salaam mwezi februari mwaka wa juzi. Kujeruhi na kuua lipi jambo baya zaidi. Au unataka kutuambia uhai wa askari polisi una umuhimu zaidi kuliko wa raia wa kawaida.

Alisema nini baada ya mauaji ya raia wale wasio na hatia au amechukuwa hatua gani hadi hivi sasa kuwarudi waliovamia jengo la ibada na kulinajisi.

Amechukuwa hatua gani dhidi ya watendaji wake waliowadhalilisha vikongwe na wazee ambao wengine wana umri sawa na Mzee Mahita au kumzidi.

Bwana Mahita aelewe cheo ni dhamana tu, kabla yake kulikuwa na waliokalia kiti hicho, wakaondoka. Ni vizuri kama Historia itamkumbuke kama msimamizi wa kweli wa haki.

Salum Kilakale
Mafiga
Morogoro



Mahakimu na polisi acheni jazba za udini

Ndugu Mhariri

KATIKA habari zilizoandikwa kwenye gazeti lako la toleo namba 247 ulieleza kwenye kichwa cha habari juu ya Qur'an na kesi inayoendelea mjini Morogoro, dhidi ya wahadhiri waliofunguliwa kesi ya makosa mawili mojawapo likiwa la kutamka "Yesu si Mungu" kama ilivyonukuliwa katika Qur'an takatifu.

Hakimu wa kesi hiyo aliingilia kati baada ya ushahidi wa Qur'an kwa kusema kuwa hakuna ushahidi kuwa Qur'an ni kitabu cha Mwenyezi Mungu. Kutokana na hayo hapo ningependa kuhoji:

Serikali hii ya Tanzania awamu ya tatu ni ya Kikatoliki au Ukristo wa aina gani? Kwani serikali nyingi zilizotamka wazi ni za Kikristo kama vile Uingereza, Ujerumani na kadhalika hazijaweza kupeleka kesi za kipuuzi kama kesi hii mahakamani. Mbali na Waislamu wachache katika jamii zao. Waislamu ambao wako huru kutangaza dini na kuelezea imani zao katika nchi hizo bila ya kusumbuliwa na polisi au serikali za nchi hizo. Je! Tuseme serikali hii ya awamu ya tatu ndio mihimili ya Ukristo katika dunia nzima?

Sisi Watanzania hususan tunaopenda haki na amani hustushwa sana na kesi za namna hii ambazo huonesha wazi jazba ya watendaji wa serikali wakiwemo polisi na mahakimu badala ya kutumia busara na akili.

Pia huonesha wazi kiwango cha usomi na mawazo ya ubinafsi na ubwanyenye (partisan) wa hali ya kusikitisha. Watu kama hawa wakiendekezwa ndio watageuza nchi hii kuwa Rwanda ya pili.

Naongeza pia kusema serikali hii ya awamu ya tatu ya CCM imeshika hatamu katika jambo hili. Bila shaka Watanzania wote watakuwa mashahidi wa yatakayotokea mbeleni.

Pia kwa barua hii nawaomba ndugu zangu Watanzania wote wapenda amani wakiwa Waislamu na Wakristo wakatae kata-kata kuburuzwa katika jazba za kidini.

Mwisho, polisi na mahakama zimeanza kuonesha mifano mibaya katika kuleta mfarakano katika nchi hii wakati wanasiasa na wakuu wa serikali wakikaa kimya na kuonesha kukubalika kwa jazba hizo. Tunawapa usia serikali ya awamu ya tatu kuwa hata wakiwafunga Waislamu wote Tanzania miaka yote bado "Yesu hatakuwa Mungu" kwao.

Kinachotakiwa ni kuvumiliana na kuishi kijamii moja na kukubaliana wewe wasema huyu ni Mungu, mimi nasema si Mungu. Msipoteze pesa, muda na gharama nyingi za walipa kodi (wakiwamo Waislamu) kusimamisha kesi ambazo hazitaleta faida yoyote kwa wananchi kiujumla. Wakati wa kulazimisha hoja umekwisha.

N.A. Ally,
P.O. Box 4354,
Dar es Salaam.


Kweli hawa ni Wakristo wenye siasa kali

Ndugu Mhariri

NAOMBA nafasi katika gazeti letu ili niweze kutoa wasiwasi wangu uliniopata kufuatia Wakristo huko Uganda kujiua kwa kujilipua moto na wengine kwa kukatwakatwa na mapanga.

Habari za vifo zimemshtua kila aliyesikia taarifa hizo mbaya na hasa aliyejionea kupitia vituo vya televisheni. Habari hizo zilidisha simanzi hasa baada ya kueleweka kwamba waliojiua na kuuawa ni wafuasi wa dhehebu fulani la dini ya Kikristo.

Tumekuwa tukisikia mahubiri ya Wakristo wakisema eti amri ya sita ya Mungu inasema "usiue" Kutoka 20:13

Tukiwa bado hatujasahau machungu ya Rwanda, Padri mwingine Joseph Kibwetere wa Kanisa la Kurejesha Amri Kumi za Mungu amefanya mauaji ambayo hatutoyasahau katika historia.

Ni kweli kwamba Kibwetere analaaniwa japo kidogo, lakini sijasikia chombo chochote kikilaani dini ya Kikristo kwamba ndiyo inayolinda imani za kibubusa (dogma) za kuambiwa hili na kukubali bila kuhoji.

Lazima tulaani kwa nguvu zote hawa watu wanaotumia dini kwa maslahi yao ya utajiri na kujinufaisha kisiasa. Waislamu jiulizeni kama waliojiua wangekuwa Waislamu vyombo vya habari tungeviambiaje?

Ramadhani A.L. Nkoboko,
Dar es Salaam.



Katiba ya Tanzania inabagua Waislamu?

Ndugu Mhariri

KATIKA toleo la Machi 31- Aprili 6, 2000 Mkuu wa Polisi Upelelezi mkoa wa Morogoro (RCO), Steven Ngowi ametaka walioandika Qur'an, wachapishaji na wauzaji wake wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Madai haya ameyatoa kwa sababu kuwa Qur'an inakashifu imani ya wengine. Kauli hii haina mantiki na hazingii akilini. Kwa sababu katika nchi yetu ya Tanzania tuna katiba na katika vifungu vifuatavyo vinasema:

19(1) Kila mtu atakuwa na haki na uhuru wa mawazo (fikra), imani na haki ya kuchagua kuhusu dini aitakayo, pamoja na uhuru wa kubadili dini au imani yake.

10(2) Bila kuathiri sheria zilizoko za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, shughuli za dini, za kuabudu na kueneza dini zitakuwa huru na ni jambo la khiari ya mtu nafsi yake na uendeshwaji, uendelezwaji shughuli za dini na vyombo vya dini kamwe hazitakuwa sehemu za serikali.

Ikiwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema hivyo kwa nini RCO Steven Ngowi atoe madai hayo? Je, Waislamu wanabaguliwa katika katiba hiyo?

Naye Hakimu Bwana Mganya bila hata aibu anasema kuwa hakuna ushahidi kuwa Qur'an ni kitabu cha Mwenyezi Mungu. Je! Wao wapo madarakani kwa ajili ya kuwatumikia watu wa dini fulani?

Kutokana na kauli za viongozi hawa wawili Waislamu tunapaswa kutambua kuwa viongozi hawa wanatunyima haki yetu kama raia wa Tanzania na hii iwe sababu ya kukipigia kura ya hapana chama tawala.

Mama Khairat,
Dar es Salaam.



Hongera Prof. Lipumba kutufungua macho wananchi

Ndugu Mhariri

HOTUBA iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba kwa kiwango kikubwa imetufungua macho Watanzania.

Hotuba hiyo aliyoitoa katika mkutano mkubwa (ambao unakadiriwa kuhudhuriwa na watu wengi kuliko mkutano wowote hapa nchini tangu karne hii ianze) uliofanyika katika viwanja vya Jangwani Machi 26, mwaka huu ulikuwa na mvuto wa aina yake kutokana na uzito wa maudhui uliojikita katika hotuba ya Mwenyekiti wa CUF Taifa.

Mwenyekiti wa CUF aliitahadharisha CCM kama chama tawala kisithubutu kuiba kura ili kujirahisishia ushindi, kikifanya hivyo kitasababisha umwagaji damu katika nchi yetu.

Hongera Profesa Lipumba kutupatia mwamko huu wa maana wenye lengo la kutusaidia katika maisha yetu ya kila siku.

Mashaka A. Lonka,
S.L.P. 90402,
Dar es Salaam.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook