Mashairi


Chechnya

Haya maafa mazito, wenzetu wamefanyiwa,
Chechnya kuna ‘mbito’, nduguzetu wauliwa,
Wafa wakubwa watoto, tena kwa kudhulumiwa,
Ni yetu sote makiwa, mauaji ya Chechnya.

Islamu ndugu moja, ni rehema tumepewa,
Anapotendwa mmoja, mabaya akifanyiwa,
Kwa pamoja yetu hoja, sote tumedhulumiwa,
Ni yetu sote makiwa, mauaji ya Chechnya.

Islamu wa dunia, mno tumeshachezewa,
Adui kutuingia, kutendwa yasiyo sawa,
Bora mwisho kufikia, kwa visasi kutolewa,
Ni yetu sote makiwa, mauaji ya Chechnya.

Fika tunajua fika, Islamu twachukiwa,
Vitimbi vinafanyika, kote tunabughudhiwa,
Ni hila zinatumika, umoja kuvurugiwa,
Ni yetu sote makiwa, mauaji ya Chechnya.

Uvamizi wa Urusi, Chechnya kuhujumiwa,
Waislamu tuhisi, ni sote tumevamiwa,
Tuwalaani waasi, kwa nguvu si kuchekewa,
Ni yetu sote makiwa, mauaji ya Chechnya.

Mauaji wafanyayo, pasipo kulaaniwa,
Ni jeuri yawapayo, Urusi wajishauwa,
Bali tusivunje nyoyo, kuungana twatakiwa,
Ni yetu sote makiwa, mauaji ya Chechnya.

Umoja wa Mataifa, umeshakununuliwa,
Upo kama umekufa, hako palipokemewa,
Ya Chechnya maafa, kimya yamenyamaziwa,
Ni yetu sote makiwa, mauaji ya Chechnya.

Tuuona unafiki, kiasi kilofikiwa,
Wanakufa halaiki, kwao roho zatolewa,
Na ‘UNO’ haisikii, kulikoni “mnajuwa”?
Ni yetu sote makiwa, mauaji ya Chechnya.

Hapa Umoja wa kweli, ndicho chasisitizwa,
Amehimiza Jalali, adui kukabiliwa,
Tuondoshe mushkeli, vyovyote itavyokuwa,
Ni yetu sote makiwa, mauaji ya Chechnya.

Ya Illahi ya Rabana, tunaomba kwako dua,
Wape nguvu Ikhwana, wasije kutawaliwa,
Mashahidi “Firjana’, nafasi waje patiwa,
Tama ni yetu makiwa, mauaji ya Chechnya.

Mshauri Mkuu
Dk. Kassim M.P. Haumotile ( wa Sungwi)
S.L.P. 2116,
Amani- Zanzibar.


Kadhi

Ikiwa twataka Kadhi, aishike Qur’an,
Awe ndiye wa kukidhi, sharia za Rahmani,
Si vema kuwakabidhi, watu wasio na dini,
Hao wasio na dini, wasitakwe ushauri.

Ili haja ikidhiwe, tuhusishwe waumini,
Suala lijadiliwe, penye ovu tubaini,
Kishae tulienguwe, tubai na lilowini,
Tuhusishwe waumini, viongozi tuchaguwe.

M.M. Mkola,



AN-NUUR 1999 Wapi lilipofikia?

Mhariri ANNURU, suali ninaulizia,
Nijibu nipate nuru, pamoja na muangaza,
Na fikira ziwe huru, nyingine kuziingiza,
Wapi lilipofikia, hili suala la Kadhi?

Kwa kuwa ni yetu haki, kuwaza na kuuliza,
Zapita siku lukuki, pasipo na kutujuza,
Vipi Kadhi hatakiki, katika zetu Baraza?
Wapi lilipofikia, hili suala la Kadhi?

Ikiwa kina fulani, mbele wamejitokeza,
Tujulishwe waumini, mambo yalivyojing’aza,
Kama si hivyo yakini, ni lipi hilo tukwaza?
Wapi lilipofikia, hii suala la Kadhi?

Hoja tuliichangia, ili tuondoe giza,
Pale ilipoingia, kwetu Kadhi kuongoza,
Wengi tukafurahia, mada tukasisitiza,
Tunapo lianza jambo, twende nalo hadi mwisho.

Tama hapa nafikia, waraka naufupiza,
Ni vema kuzingatia, haya tulo zungumza,
Hili jambo ni huria, si hekima kunyamaza,
Somo hili nilosoma, kwa kupitia ANNURU.

Ustadh M. Mkolamasa,
Darulhijra,
Box 984,
Morogoro.


koroga!

Changanya ikorogeni dini ndani ya siasa
Muwazime wajivuni wale akina Bokasa
Wababe nambari wani vifutike vyao visa
Weka dini na siasa koroga tusalimike

Nasema bandika chungu korogeni hivi sasa
Wanywe wapate uchungu ulimi wakitikisa
Yawatoke kama rungu mwcho wakijipapasa
 Weka dini na siasa koroga tusalimike

 Koroga tupate uji uwe moto hasahasa
Tuwanyweshe wauwaji tena wasije kutesa
Wale vigogo magwiji wakubwa wakunyanyasa
Weka dini na siasa koroga tusalimike

 Ushahidi nakupeni zingatieni darasa
  Mfanowe uigeni kwake  Haruni na Mussa
 Dhidi yake Firauni hawakuhofu mikasa
Weka dini na siasa koroga tusalimike

Koroga tuwamwagie wakija kujitakasa
 Usoni uwababue tuwajuwe nani hasa
Wasije watuzuzue wakatula kibubusa
 Weka dini na siasa koroga tusalimike

Wale wote wahaini wakija tutawanasa
Watuvishao uhuni pale tulipowaasa
 Tukatupwa gerezani,vipigo na kututesa
 Weka dini na siasa koroga tusalimike

Koroga tuwafilisi beti nafunga kitasa
Walotupiga risasi bila haki wala kosa
Katiba walioasi mwisho wakose furusa
Weka dini na siasa koroga tusalimike
 

Idd Kikong’ona,
 Morogoro



Vyama vya Siasa

Umetimia wakati; vyama tuvichambueni,
Tuviweke katikati, cha kweli tukibaini
Sote pamoja kwa dhati, kuratukipigieni,
Tunga tungo zitungeni’ tuvichambueni vyama.

Tuanze na CCM, wakongwe nambari wani,
Ziseme zetu kalam, sifaze ziwe hewani,
Wajuwe Dar es Salaam, na pembe zote nchini,
Tunga tungo zitungeni, tuvichambueni vyama.

Bila upendeleo, tunga kimefanya nini]
Yataje maendeleo, tangu kiwepo kitini
Taja na mafanikio, ya miji na vijijini,
Tunga tungo zitungeni, tuvichambueni vyama.

Sema toa na mifano, maji, umeme mijini,
Shule, madawa, sindano, tiba hospitalini,
Njia mawasiliano, barabara mikoani,
Tunga tungo zitungeni, tuvichambueni vyama.

Viwanda nayo ajira, biashara mitaani,
Kimefuta ufukara, aula umasikini?
Chama hiki zake sera, zimetupa afuweni?
Tunga tungo zitungeni, tuvichambueni vyama.

Tuvichambueni vyama, tunga tungozitumeni
Wazi tajeni dhuluma, kama kiliturubuni,
Tukihoji wote umma, kwenye zake kampeni,
Tunga tungozitungeni, tuvichambueni vyama.

Mwisho tuchambue CUF, kama kina sera gani,
Kina sera makinifu, za kushika usukani?
Viongozi watiifu, weledi tuwadhamini?
Tunga tungozitungeni, tuvichambueni vyama.

Mhariri An-nuur
Box 55105, Dar es Salaam.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook