Tatizo ni Dhulma
IMEKUWA ni kawaida kwa viongozi wa serikali na CCM kuwashutumu Masheikh kuwa wanachanganya dini na siasa.
Aidha, shutuma hizo zinaongeza kuwa Misikiti imekuwa ikitumika kwa shughuli za kisiasa.
Jambo moja ni wazi. Huu utakuwa ni mjadala wa viwizi. Shutuma hizi zitaendelea kutolewa lakini Waislamu hawatasita kuisema serikali na CCM hata ndani ya khutba za Ijumaa.
Tanzania si nchi inayotawaliwa kidikteta wala kibaguzi kwa misingi ya kikabila.
Kikatiba na kisheria, ubaguzi wa kidini pia haukupewa fursa.
Hata hivyo, Waislamu wanaushahidi unaoweza kusimama kwenye mahakama yoyote huru na ya haki kuthibitisha kuwepo ubaguzi, ukandamizaji na uonevu dhidi yao.
Maadhali wanaonewa na kubaguliwa kwa ajili ya imani yao, watazungumza kama Waislamu, Msikiti ukiwa ndio ofisi yao kuu na kitovu cha umoja na mfungamano wao.
Waislamu walifitiniwa kuwa wawapo ndani ya Misikiti yao wanamtukana Mungu wa Wakristo.
Viongozi wa CCM na serikali yake wakaidaka fitna ile na kuamrisha polisi wawavamie misikitini kwao.
Misikiti ikanajisiwa, Masheikh wakakamatwa, wanawake wakadhalilishwa na baadhi ya Waislamu kuuliwa.
Kitovu cha kuieleza dhulma hii hakiwezi kuwa sokoni kwa sababu si suala la wachuuzi na City. Wala Feri (Kivukoni) kwa sababu si suala la wavuvi.
Litazungumzwa Misikitini ndipo liende mitaani na maofisini.
Bwana Yusuf Makamba anashangaa iweje watu watumie Misikiti kuwaambia waumini wasiipigie CCM kura.
Tunadhani Bw. Makamba angepaswa awashangae wale ambao watatokea wawashawishi Waislamu waipende CCM.
Ni binadamu wa aina gani ambaye atakuwa na mapenzi na mtu aliyechochea kuuliwa kwa ndugu zake kisha akashangilia mauaji hayo!
Anas (r.a.) anaelezea kuwa Mtume wa Allah amesema: "Msaidie ndugu yako ikiwa amedhulumiwa au ni dhalimu. Mtu mmoja akauliza: Ee Mtume wa Allah! Ninaweza kumsaidia mtu aliyedhulumiwa, lakini nitawezaje kumsaidia dhalimu? Akasema Mtume: "Unaweza kumsaidia kwa kumnasihi/kumzuia asifanye vitendo vya dhuluma. Huo utakuwa ni msaada wako kwake". [Bukhari na Muslim].
Waislamu watakuwa hawajatekeleza wajibu wao wa kidini, iwapo hawataisema CCM na serikali yake kwa yale maovu wanayoona inayafanya.
Maadhali dini yao inawaamrisha wasiikubali dhulma, wataendelea katika msimamo wa kuikataa dhulma na kupambana na kila dhalimu.
Na suala hapa si siasa au kampeni nani au chama gani kitawale.
Bali suala la msingi ni kupiga vita dhulma. Huo ni msimamo wa Uislamu
iwe ni kwa CCM au yeyote aliye madarakani.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |