Tusielekee walikozama Wakongo

JAMII yetu inapiga hatua kusogelea ilikofikishwa Congo wakati wa utawala wa Mobutu ambapo sheria na haki zilikuwa "bidhaa adimu" kwa mwananchi wa kawaida. Mwandishi Hussein Ahmad anajaribu kulinganisha mambo yaliyoizamisha nchi hiyo na yale yanayotendeka hapa nchini.

Kwa wafanyibiashara au wasafiri kutoka Tanzania waliobahatika kufika miji ya Bukavu, Kivu na Kalemii Congo(Zaire) zama za utawala wa Mobutu Sesseseko Kukung'wendo wa Zabanga, watakubaliana nami kuwa Zaire ilikuwa kana kwamba ni nchi isiyo na serikali , kwa sababu hakuwepo aliyeweza kumdhibiti mwingine, kila mmoja alishughulishwa na ulaji wake. Kuanzia Rais, mawaziri, wakuu wa mikoa na watendaji wote wa vyombo vya Dola kila mmoja alijali nafsi yake.

Walichokijua watawala hao ni kudhulumu na kuonea Wananchi, kiasi kwamba kiongozi aliweza kwenda sokoni akajizolea bidhaa bila malipo. Makamanda wa Polisi na watoza ushuru walikuwa kama miungu watu walioweza kuchukua chochote kutoka kwa raia. Hapakuwa na utawala wa sheria. Bunduki zilikuwa ofisi binafsi za maaskari, vituo vya polisi vilikuwa ngome za wadai rushwa.

Jeshi nalo halikuwa nyuma katika vurugu hili, lenyewe liligawanyika, kilikuwepo kikosi maalum kilichomlinda Rais Mobutu na familia yake, kikosi hicho kilipata huduma zote; na lilikuwepo jeshi la kawaida ambalo maaskari wake walilazimika kujitafutia namna nyingine ya kuishi. Kwa hiyo mara kwa mara walivamia vijiji kupora mali za raia, makamanda walivizia majahazi kuwatisha wafanyabiashara na kupora mali zao. Kushitakia uovu polisi ilikuwa ni kujitafutia usumbufu na gharama. Watu walilazimika kununua haki zao kwa watendaji wa serikali.

Wananchi waliumia sana lakini mazingira ya vitisho na mabavu ya vyombo vya Dola hayakuruhusu kuhoji.

Kwa ufupi hiyo ndiyo hali ya nchi iliyokuwa ikiitwa Zaire ambayo sasa ni kinyang'anyiro cha wanasiasa baada ya kutumbukizwa kwenye machafuko makubwa yanayowaweka wananchi katika mapigano wasiyojua hatima yake. Kwa hali iliyofikia Congo hivi sasa ni kibarua kigumu kumaliza maasi ili kuijenga upya nchi hiyo.

Hayo ni matokeo ya ulafi wa watawala wasiojali utu na uzalendo ambao kwa kushirikiana na mataifa makubwa wamekuwa wakitumia rasilimali za nchi kwa manufaa yao binafsi wakiwaacha wananchi katika umasikini. Zaire au Congo kama inavyofahamika sasa imefikishwa kuwa moja ya mataifa masikini licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali ilionao.

Mara nyingi tumekuwa mafundi wa kuhadithia maangamizi yanayowafika wenzetu sambamba tukijivuna kudumu kwa amani na utulivu uliopo nchini, lakini ukweli usiotakiwa kusemwa ni kwamba nchi yetu inapita mkondo ule ule uliowazamisha wenzetu.

Katika matoleo ya nyuma ya gazeti hili mwandishi mmoja alitoa taswira ya hali ya maisha ya idadi kubwa ya wananchi wa nchi hii inayoitwa ya amani na utulivu. Sambamba mwandishi huyo alionesha matendo ya kusikitisha wanayofanyiwa wananchi hao madhalili na vyombo vya Dola wanapojitafutia riziki zao.

Tanzania hivi sasa imegawika kimatabaka, lipo tabaka la wenye nacho ambalo wengi wao ni viongozi wa nchi waliojilimbikizia mali kupitia nafasi walizo nazo. Na lipo tabaka la wanyonge waliowengi.

Viongozi wa serikali iliyoko madarakani wamekuwa mahodari kunadi amani ya Tanzania mbele ya mataifa mengine lakini wakipuuzia hatari ya mgawiko huo wa kitabaka

Hatari nyingine ni uendeshaji wa nchi usioridhisha ambapo watendaji wa serikali wamekuwa wakitumikia zaidi nafsi zao bila ya kujali wananchi.

Tunaambiwa serikali hii imefanikiwa kukusanya kodi lakini hatuelezwi wala kuona inatumikaje, maji ya kubahatisha, mahospitali hayana madawa, umeme kukatika ovyo, barabara na reli sehemu kubwa ni zile tulizorithi kutoka kwa wakoloni. Miundo mbinu kusini mwa nchi hii bado ni kitendawili miaka arobaini sasa.

Bunge nalo halionekani kufanya kazi yake ipasavyo wengi hivi sasa wanaliona ni mahali pa mavuno ya wanasiasa waliojipa uwakilishi wa Wananchi. Kama wapo wabunge wanaojali maslahi ya nchi na wapiga kura wao basi ni wachache, wengi wao ni wale wapokea posho. Vikao vya Bunge havina maana tena kwa mwananchi mnyonge hasa baada ya kupitishwa marekebisho ya 13 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Mahakama zilibaki kuwa matarajio ya wananchi kupata haki zao. Lakini yameingia mashaka kutokana na mazingira ya rushwa, uchelewashaji wa kesi, kukosekana uhuru wa mahakama, uduni na uhaba wa vitendea kazi.

Jeshi la polisi nalo linaonekana kupoteza maana yake kwa jamii, polisi wengi hivi sas si walinzi wa kweli wa wananchi na mali zao. Mtazamo waWananchi wengi hivi sasa ni kwamba kumwita polisi akusaidie ni kujitafutia makubwa na usumbufu wa bure, lazima kama unaweza ujipigepige ili upate haki yako.

Ni mazingira hayo ambayo yameyafanya magereza kufurika watuhumiwa ambao wengi wao haijulikani kesi zao zitasikilizwa lini na cha kusikitisha zaidi wengine hawajui hata makosa yao.

Kwa hiyo kama ilivyokuwa Zaire ya Mobutu, jamii yetu inaelekea mahali pasipotabirika, inaonekana kana kwamba anasubiriwa nani amfunge paka kengele, ili kila mtu ajue la kufanya.Viongozi wetu hawaonekani kuliona hilo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook