MTUME hakuacha Masheikh kuwa ndio kigezo cha Uislamu sahihi.
Bali alichoacha ni Qur'an na Sunnah yake.
Hayo yamesemwa na baadhi ya Waislamu kufuatia kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Yusuf Makamba kuwa "Mtume hajawatuma Masheikh kuhubiri siasa Misikitini".
"Mtume hajatuma watu wanaoitwa Masheikh, bali alichowaambia Waislamu wote ni kuwa amewaachia kitabu cha Allah na Sunnah yake", amesema Sheikh Ali Abbas na kusisitiza kuwa hiyo ndiyo miongozo pekee Waislamu wakiifuata hawatapotea na wala sio Masheikh.
Mhe. Yusuf Makamba amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, baadhi ya Masheikh wanaacha kuhubiri dini misikitini na badala yake wanawashauri waumini wasiichague CCM katika uchaguzi ujao.
Akasema huko ni kuhubiri siasa na kuagiza Masheikh hao wahojiwe hayo ndiyo Mtume aliyowatuma?
Kufuatia kauli hiyo, Ustadh Mustafa amesema, kuwanasihi waumini waiepuke CCM ni kufuata mafunzo ya Mtume (s.a.w.).
Amesema, Mtume (s.a.w.) ameagiza watu wakiona uovu wauondoe kwa mikono yao, wakemee au wachukie na kuongeza, "maadhali Waislamu wametosheka kuwa CCM inawadhulumu, ni wajibu wao wakidini kuipiga pande".
Amesema, Qur'an imewaagiza waumini wasisaidiane katika uovu na udhalimu, kuongeza "maadhali Waislamu wanahisi kudhulumiwa na CCM, aya zinazowakemea madhalimu zitaendelea kusomwa misikitini na CCM kutajwa katika sherhe na maelezo ya aya hizo.
"Tukisoma aya zinazowalaani wauaji, tutawataja walioua Mwembechai na CCM iliyopongeza mauaji yale", amesema.
Naye Mama Fatmah Mussa amesema, Allah (s.w.) amewaonya waumini wasipokee habari na kuziamini bila kuzifanyia uchunguzi.
Akanukuu aya isemayo: "Enyi mlioamini kama fasiki akikujieni na habari (yoyote ile msimkubalie tu) bali pelelezeni (kwanza) msije mkawadhuru watu kwa ujahili na mkawa wenye kujuta juu ya yale mliyoyatenda". [49:6]
Amesema, Waislamu waliuliwa pale Mwembechai kwa sababu baadhi ya viongozi wa CCM walipokea habari wakaziamini bila ya kuzifanyia uchunguzi huku wakitamba hawashindwi na kitu.
Kwa jazba kubwa wakaamrisha nguvu kubwa ya vyombo vya dola iwakabili Waislamu.
"Kuogopa kuundwa Tume huru ya uchunguzi na kukataa kuwafikisha wauaji mahakamani ni CCM na serikali yake kukiri udhalimu iliofanya", amesema.
"Viongozi hao waliowadhuru watu kwa "ujahili" na chama chao kilichowapongeza hawatoacha kutajwa kwa ubaya wao misikitini aya hiyo isomwapo", amesema.
Aidha, amesema, suala si kutajwa tu lakini na kuwatahadharisha waumini wawaepuke.
KUMEKUWA na wimbi kubwa la watoto wenye umri wa kwenda shule kuzurura mitaani bila kwenda shule. Aidha, wengi wao wanaonekana kutokuwa na wazazi au walezi wa karibu.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia watoto wenye umri kati ya miaka tisa na 14 wakiwa wameshika chekecho wakipembua mchanga kutafuta madini ya kuuza.
Walipoulizwa na mwandishi kama kazi hiyo wanaifanya kwa agizo la nanin, walisema, ni kwa faida yao na hakuna mtu aliyewatuma kuchekecha mchanga.
Wengi wameeleza kwamba wazazi wao waliwafukuza na wengine wakidai hawana baba wala mama na wala hawakuwahi kuwaona tangu wanakuwa na akili.
Mkuu wa shule ya msingi ya kijijini hapo Bwana Raphael Clemence alipoulizwa kama watoto wanaoonekana mitaani ni wanafunzi wake, alikataa na kusema kuwa wanafunzi wake wanahudhuria shule kama kawaida na hawana tabia za utoro.
Aidha, Bwana Raphael alisema kuwa, uchunguzi unaonesha kuwa watoto hao si wenyeji wa kijiji hicho ambacho kimejaa utajiri wa madini. "Watoto wote uliowaona ni kutoka nje ya Mirerani", alisema Mwalimu.
Naye Mratibu wa elimu kata ya Mirerani, Bwana Urio amethibitisha kauli ya Mkuu wa shule kwa kusema kuwa huo ni uchunguzi wa kisayansi. Wengi wa watoto hao ni kutoka vijiji jirani vya Arumeru, Mikunguni, Makiba na kwingineko.
Viongozi wa serikali hawakupatikana ili kuzungumzia suala hili. Lakini Afisa Elimu Bwana Urio aligusia kuwa serikali ya kijiji tayari imeshachukua hatua za awali.
Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na uongozi wa mkoa, serikali ya kijiji ikishirikiana na ILO kitengo cha kuzuia ajira za watoto tayari wamefanya vikao kuzungumzia suala hilo.
Baadhi ya wazazi walioongea na mwandishi wa habari hizi wameiomba serikali kuwaondoa watoto hao kwa kile walichokiita ni aibu kwa watu wa Mirerani ambao ni matajiri kutokana na madini.
Pamoja na maelezo yaliyotolewa na viongozi wa elimu, lakini bado kuna watoto wengine ambao ni wenyeji wa Mirerani nao wameungana na wenzao katika kutafuta chochote pasipo kwenda shule.
Huenda hili linachangiwa na vishawishi wanavyoweza kupata toka kwa wenzao wasiokwenda shule.
Aidha, yawezekana likasababishwa na shule yenyewe kuwa ni moja na watoto ni wengi kupita uwezo wa shule.
Kwa maelezo ya Mkuu wa shule takriban kila darasa lina idadi ya wanafunzi 130 jambo ambalo si rahisi kwa mwalimu kudhibiti utoro na matatizo mengine ya nidhamu kwa watoto.
Baadhi ya wazee wa Mererani wamezilaumu sera za chama tawala ambazo wamesema zimedumaza elimu hivyo vijana wengi kuipuuza badala yake kuamua 'kujitafutia' maisha wangali wadogo.
"CCM imeshindwa kuandaa mazingira mazuri ya elimu hasa elimu ya msingi, vijana hawavutiwi na mfumo huu wa elimu wa kujua kusoma na kuandika", amedai mzee mmoja.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |