Huku mbio za urais zikianza:
Lipumba atonesha Wananchi Tabora
KOSA lao nini, wananchi wa Tabora wameomba serikali ya CCM iwaeleze.

Mkoa ulikuwa kitovu cha harakati za kupigania uhuru na kituo cha "kutotoa" viongozi. Lakini sasa umefanywa hame na kielelezo cha umasikini.

Pamoja na mkoa kutelekezwa hata vile vizuri vilivyokuwepo umenyang'anywa.

Huo ni mlolongo wa hoja na maswali yanayoulizwa na baadhi ya wananchi wa Tabora baada ya hotuba ya Profesa Lipumba hivi karibuni.

"Mkoa ulishiriki kikamilifu kutafuta uhuru. Viongozi wote wa siasa tuliwapokea tukakaa nao kwa wema wakisoma 'Tabora School'. Hawakuona mahali palipofaa kwa mkutano wa TANU wa 1958 uliopitisha uamuzi wa Busara isipokuwa Tabora. Lakini fadhila tunayorejeshewa ni kunyang'anywa hata kile tulichokuwa nacho, amesema Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mussa Msabila.

Manung'uniko na hoja kama hizo, imekuwa ndio gumzo mjini Tabora toka Prof Lipumba amalize ziara yake mkoani hapo.

Akiwahutubia wananchi wa Tabora Prof. Lipumba alisema, baada ya uhuru kupatikana kila kilichokuwa kizuri mkoani hapo kimehamishwa.

Amesema, karakana kuu ya shirika la Reli(Loco shed) ilikuwa Tabora. Ikitoa ajira kwa Wananchi wa mkoa huo na huduma muhimu.

Lakini amesema, karakana hiyo ilihamishiwa Morogoro ambapo ilijulikana kama Diesel Shed.

Aidha amesema kiwanda cha Tumbaku ilikuwa kijengwe Tabora inayolima tumbaku kwa wingi, lakini kilipelekwa Morogoro.

Katika hali hiyo Tabora imenyimwa unafuu wa ajira na mzunguko wa fedha unaotokana na mishahara ya wafanyakazi.

Wazee kadhaa katika wazee wa CCM walioongea na gazeti hili wamesema, hotuba ya Lipumba imewaweka njia panda.

"Anachoongea Profesa ni ukweli mchungu kwa CCM na changamoto kwa wanaTabora", amesema mmoja wa wazee hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

"Tukieleza shida zetu kama wazee wa CCM hakuna anayetujali sasa hoja kama hizi (za Profesa Lipumba) zimezidi kutuchanganya", aliongeza.

Lakini hakutaka kufafanua shida gani na walizipeleka kwa nani na lini.

Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kiasi miezi miwili nyuma wazee waliilamikia CCM juu ya hali zao ngumu za kimaisha kiasi kwamba hawawezi kumudu hata gharama za matibabu.

Risala hiyo waliisoma mbele ya kada mmoja wa CCM aliyekwenda kumpa Kadi Mzee Fundikira.

Inasemekana kiongozi huyo wa CCM aliwashushua wazee hao kwa kuwaambia kuwa yeye hakwenda kutatua matatizo yao. Aidha aliwaambia, risala yao inaonekana imetoka kwa wapinzani.

Chama cha CUF kilifanya mkutano wa Baraza lake mjini Tabora ambapo pia ulifanyika mkutano ya hadhara.

Mkutano huo ulifanyika katika uwanja wa Chipukizi

Wakati huo huo, Wanafunzi 12 wa shule ya Sekondari Milambo wamesimamishwa shule kwa kile kilichodaiwa kuwa kumshabikia Lipumba.

Wanafunzi wengine kadhaa wamechapwa viboko kwa kosa hilo.

Wanafunzi waliosimamishwa wametajwa kuwa ni Frederick William, Mohamed Ally, Edward Uforo, Dismas Juma na Renatus Peter.

Wengine ni Bikwa Zuberi, JumaTwahiru, Hussein Shaaban, Mrisho Mihehe, Marko Fidelis, Maarifa Muyomba na Salim Almasi.

Taarifa za baadhi ya vyombo vya habari zimeeleza kuwa uongozi wa shule utatumia mikanda ya video kuwatambua Wanafunzi wengine walioonesha kumshabikia Profesa Lipumba.


Msamaha wa deni ulaghai


MSAMAHA wa 'madeni' haujaiongezea serikali hata senti moja wala kujinasua na kitanzi cha deni.

Hivyo kauli kwamba, iutumie msamaha huo kuboresha hali za wananchi ni za kupotosha na kuichonganisha serikali na wananchi.

Hayo yameelezwa na mtaalamu mmoja wa mambo ya benki na masuala ya fedha ya Kimataifa.

"Nchi hakuna inachopata kwa kuambiwa imesamehewa deni la shilingi trilioni 1.6. Kwanza hicho kiwango hakiwakilishi thamani yoyote halisi, bali ni zao tu la mchezo wa namba", amesema mtalaamu huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Amesema kama nchi inadaiwa shilingi trilioni 3.2 ikasamehewa trilioni 1.6 hakuna kinachoongezeka katika uwezo wake wa kiuchumi.

Awali ya yote, amesema, msamaha huo hauna maana hiyo 1.6 trilioni itageuka kuwa fedha taslimu na kuingia katika hazina ya serikali.

Pili, bado serikali inawajibika kuendelea kulipa deni lililosalia.

Tatu, deni lililosalia hakuna tamaa litamalizika.

Maadhali deni linaendelea kuwepo, amesema, na serikali inawajibika kuendelea kulipa, utumwa wa deni linalokuzwa kwa riba bado upo pale pale.

"Misamaha hii ni kiini macho, wananchi wasipewe tamaa ya kupata unafuu, vinginevyo watakuwa wamechonganishwa na serikali yao watakapokosa kuona huo unafuu", amesema.

Akizungumzia dhana ya mikopo, madeni na misamaha katika mashirika ya fedha ya Kimataifa, amesema kinachofanyika ni utapeli na wizi.

Amesema, ukiambiwa deni lako ni trilioni 4 yaweza kuwa deni halisi lilikuwa bilioni 800 tu kutegemea umri wa deni na kiwango cha riba.

Kwa hiyo, ziada ya trilioni 3.2 (3,200,000,000,000) ni zao tu la mchezo wa namba. Ndio maana ni rahisi kwa wanaodai kutamka wamesamehe 1.6 trilioni kwa vile wanajua namba hiyo haiwakilishi mali yoyote.

Aidha, wanajua vyovyote iwavyo deni hilo halilipiki mpaka mwisho wa dunia. Bali wanachofanya ni kukushikilia uendelee kukopa na kusalia mtumwa wao.

Amesema, ni bora wananchi wakaelimishwa kuhusu ujambazi huu wa mashirika ya fedha ya kimataifa na nchi wahisani kuliko kuwapa tamaa hewa.

Mtaalamu huyo wa masuala ya fedha alikuwa akitoa maoni yake juu ya taarifa za msamaha wa sehemu ya madeni ya Tanzania kwa nchi wahisani.

Akizungumza na gazeti hili, amesema, anaona uchungu jinsi wananchi wasivyoelezwa ukweli juu ya masuala haya ya mikopo, madeni na misamaha yake. [Soma makala hii]

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook