Waislamu mjini Moro wiki hii walizuia Karandinga lisiwapeleka rumande wenzao baada ya Hakimu aliyesema Qur'an si kitabu cha Mungu, kufuta dhamana yao.
Hakimu John Nganya aliingia mahakamani na kusema, "ujumbe wenu nimeupata na kwa upumbavu wenu dhamana zimefutwa. Mtakwenda rumande mpaka tarehe 3/5/2000", imeelezwa.
Baada ya shura fupi, Waumini hao waliamua kumuona Hakimu mkuu Mkazi.
Kesi ilipitiwa upya ambapo Mwendesha mashitaka alieleza kuwa hapajakuwa na tatizo la kuwafutia dhamana washitakiwa.
Wakati hayo yakiendelea, polisi walianza kuwapakia watuhumiwa kwenye karandinga.
Hata hivyo Waislamu walikuja juu na kuzuia gari hilo kuondoka.
Mjadala mkali ulifanyika kati ya Hakimu Mkuu Mkazi, Mwendesha mashitaka na karani wa mahakama. Hakimu John Nganya aliitwa ajieleze.
Hakimu Mkuu baadae aliwaambia watuhumiwa dhamana yao inaendelea na kuwataka waondoke wakiwa huru kuendelea na shughuli zao.
Utenguzi huo wa amri ya hakimu John uliitikiwa kwa kivumo cha Takbiira huku Waislamu wakitoka mahakamani.
Washitakiwa katika kesi hiyo na. 416/99, awali waliandika barua kumkataa hakimu John.
Barua hiyo ya kumkataa imetajwa kuwa ndiyo iliyomchochea hakimu John kuwafutia dhamana watuhumiwa.
Katika barua yao ya kumkataa Hakimu huyo, walisema hakimu kwa dhahiri amekuwa akionesha hisia za imani yake dhidi yao.
Aidha wamedai japo shitaka ni kufanya mhadhara bila kibali, lakini Hakimu kwa makusudi amekuwa akiwatupia shitaka la kukashifu dini ya kikristo.
Sababu nyingine waliyoitoa ni kuwa, hakimu Nganya amekuwa akitoa maneno ya kuchokoza hisia za Imani yao pasi na sababu za Msingi.
Walitoa mfano kuwa, alidiriki kusema Biblia ni Neno la Mungu na Qur'an si andiko la Mungu jambo ambalo wamedai limefanya kesi iendeshwe bila ya kuzingatia madai.
Barua hiyo ya washitakiwa kwenda kwa hakimu Mkazi wa mahakama na nakala yake kupewa Bwana Nganya imedai Hakimu huyo amekuwa akitumia muda mwingi kujibu Hoja za washitakiwa badala ya mashahidi wa upande wa mashitaka.
Aidha washitakiwa walidai Hakimu Nganya amekuwa akiwatisha mara kwa mara.
WIMBI la kuisaidia serikali ya CCM iepukane na dhulma, limetikisa mji mkuu Dodoma mwishoni mwa wiki.
Imedaiwa udhalimu unaofanywa dhidi ya Waislamu hauvumiliki tena. Na namna pekee ya kuisaidia CCM isiendelee kudhulumu ni kutoipa kura Oktoba.
Wanawake Waislamu wameweka wazi kuwa, wao hawana hamu tena na siasa za CCM. Wamesema wao walivamiwa wakiwa Msikitini wakapigwa sana na kudhalilishwa wakiwa mikononi mwa polisi na askari Magereza.
Mauaji ya Mwembechai wameyataja kama kilele cha dhulma na ukandamizaji. Wamesema Damu ya Waislamu imemwagwa bila ya haki na vikao rasmi vya CCM vikatoa pongezi kwa wauaji.
Wakitoa salamu zao katika sherehe za Mwaka Mpya, wameishutumu serikali ya Rais Mkapa kuhusika na kudhalilishwa kwao kwa vile amekataa sheria kutumika kulihukumia suala hilo.
Sherehe hizo zilifanyika Aprili 15, katika uwanja wa Jamhuri, waandaaji wakiwa Bakwata na kikundi cha Bi Khadija.
Baada ya kutolewa salamu hizo, Sheikh wa wilaya wa Bakwata alijikuta akizomewa na umati wa wahudhuriaji pale alipojaribu kuponda salamu hizo zinazoiasa CCM na serikali yake.
Hatua hiyo ya Sheikh Aburabi ilipingana na ile ya Mbunge wa Dodoma mjini Mhe. Hashim Saggaf aliyekuwa mgeni rasmi. Yeye alisema, kila mtu ana uhuru wa kueleza maoni yake.
Habari tulizozipata tukienda mitamboni zimeeleza kuwa Bakwata wameandika barua polisi kuomba radhi na kujieleza kuwa wao hawahusiki na salamu zilizoisema CCM na serikali yake.
Juhudi za gazeti hili kuwasiliana na uongozi wa Bakwata juu ya habari hizo hazikuweza kufanikiwa.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |