Ahadi hiyo imetolew katika maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislamu zilizofanyika mjini humo jumapili iliyopita.
Maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislamu hufanyika kila mwaka katika mwezi Muharramu kwa mujibu wa kalenda ya kiislamu ambapo Waislamu hukumbuka tukio muhimu la Hijra.
Hijra ni hatua ya Waislamu wakiongozwa na Mtume Muhammad(s.a.w) kuhama mji wa Makka kwenda Madina miaka 1421 iliyopita.
"Hapa hatuwezi kuhama, bali Hijra yetu tutasafisha uovu uliopo", wamedai Waislamu wa Mwanza.
Akizungumza katika Hafla hiyo, Ustaadh Ilunga Kapungu alisema Waislamu popote walipo hawana budi kuitafsiri kivitendo falsafa ya Hijra.
Ustaadh Ilunga aliuambia umati mkubwa uliokuwa ukimsikiliza kuwa Masahaba walihajiri Makkah kwenda mji mwingine wa Madina si kwa sababu nyingine ile ila kujiweka sawa kimapambano dhidi ya dhulma iliyoshamiri katika jamii yake.
Akioanisha tukio la Hijra na hali inayowakabili raia waislamu hapa nchini, Ustaadh huyo alisema kwa kiwango kikubwa madhila yanayowakuta Waislamu yanatokana na utawala mbaya wa dola na taasisi zake.
"Dereva akiendesha gari vibaya huondolewa akawekwa dereva mwingine, hasusiwi gari", alisisitiza.
Aidha aliwataka Waislamu kusimamisha haki kwa kushiriki kuweka uongozi uliosafi.
Alisema Hijra ilikuwa hatua katika harakati za kusimamisha haki.
Hata hivyo alisema katika mazingira waliyomo Waislamu hivi leo hawawezi kuhajiri bali kuendesha harakati za kuisafisha jamii na uovu hapo hapo walipo.
NIMESOMA orodha ya waratibu wa uchaguzi na wasimamizi iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuchapishwa na gazeti hili toleo lililopita. Orodha hiyo ilimshtua kila aliyeifuatilia, kwani si tu kwamba ilionesha ubaguzi wa kidini uliokithiri katika sekta mbalimbali za serikali bali pia ulionesha kudumaza misingi ya demokrasia.
Pamoja na kuwa na athari mbaya hasa kwa Waislamu, lakini pia orodha hiyo ni ushahidi wa kisayansi unaotafutwa na Mheshimiwa Rais Mkapa ili kuwashughulikia wanaofanya kazi za serikali kwa upendeleo wa kidini. Tutashindwa kuamini kauli ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa Januari 19, 1999 pale Diamond Jubilee alipopewa malalamiko ya Waislamu likiwemo la kubaguliwa katika idara mbalimbali za serikali.
Mhe. Rais Mkapa akijibu risala hiyo alisema: "...serikali itayapa uzito unaostahili masikitiko yenu, hakuna hata moja litakalopuuzwa. Kila moja litafanyiwa utafiti na uchambuzi wa kina...".
Sasa utafiti na uchambuzi wa kina anaotafuta Mhe. Rais tofauti na ubaguzi wa wazi kama huu ni upi? Mimi naamini Rais Mkapa hawezi kuwaacha watu wanaotaka kubomoa umoja, upendo na ushirikiano wetu waendelee kutugawa kwa misingi ya dini.
Orodha hiyo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatia wasiwasi hasa kwa Waislamu. Aliyepanga hivyo hatujui kama alikusudia nini katika timu yake hiyo. Uwiano wa majimbo 109 (Wakristo 99 na Waislamu 10) mikoa 20 (Wakristo 18 na Waislamu 2) inawezekana ukawa na lengo la kuunufaisha Ukristo na kuudidimiza Uislamu kupitia uchaguzi. Wasiwasi wetu mkubwa unatokana na ushirikiano wa Kanisa na serikali kama anavyoainisha Dk. Sivalon kwamba: "Ni dhahiri kuwa hakuna nchi yoyote katika Afrika ambako Kanisa limepewa nafasi bora kama Tanganyika. Uhusiano kati ya kanisa na serikali unawaweka viongozi wa Kanisa katika nafasi nzuri ya kuonesha muelekeo wa kisiasa. Uhusiano huu ulitiwa nguvu zaidi na shughuli za viongozi muhimu wa Kanisa ambao walimsaidia Mwalimu Nyerere katika masuala ya (kiserikali) na hivyo kumpa muda wa kuongoza TANU".
Wasiwasi wetu Waislamu unatokana na historia inavyojionesha kama anavyoeleza Dk. Sivalon na kwamba kumbe mizizi ya ubaguzi ndiyo kwanza inamwagiwa maji ili ilichupue na kutoa matunda yatakayoneemesha Kanisa katika kipindi kijacho. Ni matunda hayo yatakayokwenda bungeni, halmashauri na hata Ikulu huku tukiimba nyimbo za usawa na kuheshimiana kwa dini zote.
Historia ya Kanisa inaonesha kwamba lilikuwa mbele katika kuhodhi utawala. Papa Pius wa X alisema tarehe 9, Novemba 1903 kwamba "Tutawakasirisha watu wengi tunaposema kwamba ni muhimu kwetu kujishughulisha na siasa. Lakini kila anayelituhumu suala hili kwa haki lazima atambue kuwa Papa mwenye mamlaka aliyepewa na Mungu, hukumu ya juu haina haki ya kutenganisha mambo ya kisiasa kutoka uwanja wa imani na maadili". [Peter de Rose "Vicars of Christ" Corg Books London 1984).
Papa Leo XIII alisema: "Wakatoliki wanawajibika kuwapigia kura wale ambao wanaahidi kuendeleza maslahi ya Ukatoliki na kamwe wasimchague mwingine asiyependa dini (ya Ukatoliki) badala yake ... kuna kura ya jumla, kura ya jumla ya Wakatoliki kwa ajili ya wagombea wa Kikatoliki".
Baada ya vita ya pili ya dunia, Papa Pius wa XII alikuwa tayari kumfukuza Mkatoliki yeyote kwenye Kanisa ambaye alimpigia kura Mkomunisti badala ya Mkatoliki [Uk. 208 Vicars of Christ].
Sasa ukiiangalia historia ilivyo ya Kanisa na ulinganishe na mazingira ya Tanzania leo hayana utofauti na zama hizo za giza. Mkomunisti wa sasa ni Muislamu. Hatuwezi kushangaa Waziri Kapuya akizomewa bungeni na watu walioingia huko ili kuendeleza maslahi ya Kanisa.
Lakini mimi siamini kama ubaguzi huu Mheshimiwa Rais Mkapa aliyeapa kulinda usawa na haki bila ubaguzi wa aina yoyote anaweza kuuridhia ufanye kazi katika mazingira ya Tanzania ya leo.
Ramadhani Amri L. Nkobokobo,
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |