UTAJIRI wa nafsi ni ile hali ya nafsi kukubali kuwa dunia hii ina Muumba ambaye ndiye anayemiliki neema zote na ndiye mtoaji na mgawaji wa neema hizo. Yeye pekee ndiye mwenye uweza wa kuruzuku na kudhikisha na ni yeye tu awezaye kutajirisha na kufakirisha.
Kwa ujumla imani hiyo hutakasa nafsi na mambo yote yanayochafua moyo, au kwa maana nyingine, huponya maradhi yote ya kiroho (moyo). Kwa hali hiyo nafsi hiyo huepukana na husuda, choyo, chuki, majungu, fitna, ubinafsi, ubakhili, majivuno, kujionesha, kujidai, kibri, dharau na dhulma kwa ujumla wake.
Nafsi iliyosalimika na maradhi au maovu hayo mara zote huridhika hutosheka na kushukuru unapopata neema yoyote iwe kubwa au ndogo kwani ina yakini kwamba kila neema anayopaswa mja inakadiriwa na Muumba japo ni wajibu kwa kiumbe kufanya jitihada kutafuta fadhila za Mola wake.
Vile vile nafsi ya aina hiyo inapofikwa na shida huwa na subira na uvumilivu kwani ina yakini kwamba yote hayo ni mitihani ya Mwenyezi Mungu. Nafsi hii huweza kutoa na kuwapa viumbe wenzie neema yoyote iliyo katika miliki yake kwa kiasi cha uwezo wake kwa kuwa ina hakika kwamba Mwenyezi Mungu ana hazina kubwa isiyopungua wala kwisha, hivyo aweza kumrejeshea na hata kumzidishia kile alichotoa ama hapa duniani au akhera au kote.
Zaidi ya hivyo, nafsi hiyo hupendelea viumbe wote wapate hali bora ya maisha hapa duniani na huko akhera. Kwa ajili hiyo nafsi hiyo hufanya harakati kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinagawanywa kwa viumbe wote na wakati huo huo ujumbe wa Allah (s.w.) unawafikia watu wote. Kwa maneno mengine roho na mwili vina nawirishwa sambamba.
Katika kufanikisha harakati hizo nafsi iliyokuwa tayari kujitoa muhanga kwa hali na mali ili kuondoa dhulma ya aina yoyote katika ardhi. Nafsi hiyo huwa tayari kwa mapambano ya kisiasa, kwa silaha ya kura na hata kivita dhidi ya dhalimu yoyote kulingana na wakati au mazingira. Dhalimu huyo aweza kuwa mtu binafsi, chama au serikali ili kusimamisha haki kwa wote.
Umasikini wa Nafsi
Ni hali ya nafsi kukosa imani sahihi juu ya Muumba na uweza wake. Nafsi hii maskini huwa na dhana potofu kwamba ama ulimwengu umetokea tu kwa bahati mbaya au unae Muumba lakini Muumba huyo ana wasaidizi au washirika katika utendaji kazi wake. Au pia nafsi hii hudhani kuwa yupo Muumba lakini hashughuliki na maisha ya viumbe.
Kwa ujumla nafsi hii ama haiamini au ina mashaka juu ya kuwepo kwa Muumba na maisha baada ya kifo.
Kwa hali hiyo, nafsi hiyo hukabiliwa na maradhi mengi yanayosumbua moyo. Kutokana na maradhi hayo nafsi hii ama huona neema zilizopo mbinguni na ardhini hazina mwenyewe au zinamilikiwa na Muumba mwenye washirika. Au zina mwenyewe lakini hazifuatilii.
Nafsi hiyo hudhani kuwa riziki au utajiri hupatikana kwa bahati nasibu au kwa jitihada pekee za mja au kwa kuwaomba washirika waliomfanyia Muumba wakiwemo wapiga ramli, wasoma nyota, waganga wa tunguli, washona hirizi na waandika makombe, mizimu na mababu na kadhalika.
Kwa imani hiyo, nafsi hiyo hutafuta mafanikio ya kidunia kwa njia zozote, ziwe za halali au za haramu ikiwa ni pamoja na unyonyaji, unyang'anyi, rushwa, ulaghai, utapeli, kamari, riba, wizi na kadhalika.
Mara nyingi nafsi hiyo hughafilika na maisha ya dunia tu. Kwa wale matajiri wanaona wamepata utajiri kwa ujanja na jitihada zao huulinda utajiri wao kwa kulimbikiza na hufanya ubakhili siku zote wao huhofia kufilisikika na hivyo badala ya kuwainua na kuwasaidia wasio na uwezo wao husherehekea adha wanayoipata wenzao au hushiriki kuwakandamiza na kuwabeza kwa kudhani wamekuwa mafakiri kwa uzembe wao.
Hata wanapotoa, hutoa kwa ria, ili waonekane kuwa ni matajiri au wakati mwingine hutoa ili kuwafurahisha watawala au hutoa katika mambo ambayo yatachangia kuongeza soko la bidhaa zao hata kama mambo hayo ni ya kishetani. Wengine hutoa baada ya kufikwa na majanga ya kimali.
Katika hali ya shida, nafsi maskini husononeka mno kwa kudhani kuwa, waliopata wana bahati. Kwa hiyo nafsi hii hushikwa na maradhi ya chuki, husuda, fitna, kijicho na kadhalika. Hufikia mahali nafsi hiyo kupendelea mwenye nacho wapatwe na matatizo ili nayo ifarijike kutokana na maradhi hayo mabaya.
Wakati wa operesheni ya kilichoitwa uhujumu uchumi, Bwana mmoja alirukaruka kwa furaha aliposikia mali yote ya mfanyabiashara mmoja maarufu imesombwa na polisi na yeye mwenyewe kakamatwa.
Aidha, mtu mwenye nafsi hiyo hutamani vile walivyoruzukiwa wengine angeruzukiwa yeye. Na kile au vile alivyoruzukiwa yeye wengine wasipate.
Mara kwa mara nafsi hiyo huteseka na donge moyoni kwa nini yule kapata na mimi nikose. Binti mmoja alifurahia mwenziwe kufiwa na mchumba wake. Kana kwamba moyoni alisema 'bora wote tukose. Au nafsi hiyo huumia moyoni kwa nini yule yuko vile nami niko hivi'.
Nafsi hii huwa tayari kufanya fitna na kila jitihada kuhakikisha fulani hafaulu kupata kitu fulani au aondokewe na neema fulani. Na huwa tayari kufanya hata maovu ili kupata inachotamani. Kwa watu wengine, nafsi hii huwa hairidhiki hata na umbile la asili alilomuumba Muumba. Ndio maana huhangaika kubadilisha ngozi au nywele ili ikidhi tamaa yake ya kufanana na wale inaowaona 'wameumbika vizuri".
Kwa wengine nafsi hii huwapelekea kukosa uadilifu katika ndoa au kushindwa kudumisha ndoa kwa kushindwa kuvumilia kukosa vile wanavyotamani. Wengine wenye maradhi au ugonjwa huu wa nafsi hukubali kutenda uovu kwa matarajio ya kupata kitu fulani iwe mali au mume, wengine hukubali kuolewa na tajiri twaghuti kuliko fakiri mcha Mungu. Akina dada au mama wengine wenye nafsi hii hupinga hata ruhusa ya waume zao kuongeza mke au wake. Wengine wenye nafsi hii huridhia talaka kuliko ukewenza.
Ikiwa madarakani nafsi hii hujali maslahi yake binafsi. Pamoja na mshahara mnono na marupurupu, nafsi hii hula rushwa. Huwa tayari kuangamiza roho za watu ili kulinda madaraka bila kujali kuwa kukaa kwake madarakani kunawaumiza wengi.
Nafsi za namna hii zinapokuwa madarakani, haki huadimika, badala yake dhulma hushamiri. Rasilimali za dunia humilikiwa na wao wachache huku walio wengi wakiishi kwa shida hata kufa njaa.
Wengine wanapofanya harakati za kutafuta haki kwa wote, nafsi hizo huchukia kwa kuona kuwa harakati hizo zinalenga kuwanyang'anya vile wanavyovipata kwa dhulma. Hudhani kuwa wapigania haki hao wanatamani "ulaji wao".
Na pia wanajua kuwa dhulma ikikoma, wao watakosa au watapungukiwa na maslahi. Hivyo nafsi hizo maskini hutumia nguvu, propaganda, urubunifu na vitisho ili kuwadhibiti watetezi wa haki.
Umaskini wa nafsi humfanya mtu asiridhike, asitosheke, asikinai awe
limbukeni, asisubiri wala kuvumilia. Kwa ujumla, nafsi maskini ni nafsi
inayoondoka duniani na mzigo wa madhambi.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |