Uchaguzi 2000 somo toka Z'bar



HALI ya Zanzibar kabla ya 1995

INAFAHAMIKA kwamba historia ya Zanzibar ni ndefu lakini cha msingi ni kuwa uongozi wa Sultani ulipinduliwa na kuwa na uongozi wa wananchi ukiongozwa na hayati Aman Karume kama Rais wa kwanza. Baadaye pakawa na Muungano wa Zanzibar na Tanganyika kufanya Tanzania.

Wakati wote chama tawala Zanzibar kilikuwa Afro Shiraz na kwa upande wa Tanganyika TANU. Mwaka 1977 TANU na ASP zikaungana kufanya CCM. Na kuanzia wakati huo, kukawa na CCM - Bara na CCM - visiwani katika misingi ya uamuzi ijapokuwa maamuzi ya pande mbili hizi zinawasilishwa katika CCM Taifa. Si nia ya makala hii kuonesha mafanikio au udhaifu katika serikali ya Zanzibar zilizopita chini ya Alhaj Aboud Jumbe, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Alhaj Idrisa Abdul Wakil na baadaye Rais Salmin Amour.

Hata hivyo, inaeleweka pamekuwa na mawimbi na tufani katika mvutano wa hali ya muungano kati ya Zanzibar na Bara, hata nafasi ya uongozi katika muungano. Hali hii itakumbukwa sana ukizungumzia kwa mfano: "Kuchafuka kwa hali ya hewa", "Zanzibar kumezwa na bara", "Zanzibar kuwa mkoa au wilaya","Rais wa Zanzibar ni mkuu wa mkoa".

Haya yalizungumzwa na wananchi katika vipindi mbalimbali vya Marais tofauti. Hali hii watu walihisi yaliweza kudhibitiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere na baada ya kuondoka mambo yangekuwa magumu. Picha tutakayozungumzia baadaye inaonesha kuwa sio hivyo kwani nguvu alizokuwa nazo Mwalimu bado ipo mpaka sasa hivi. Ila swali ni kuwa nani yupo nyuma ya nguvu hii?
 

Hali ya Zanzibar baada ya 1995

Kabla ya 1995 pamekuweo na mfumo wa chama kimoja cha siasa Tanzania. Mfumo wa vyama vingi kiutekelezaji na kiuchaguzi ulianza kufanya kazi mwaka 1995. Matayarisho yake yalianza wakati wa utawala wa Rais wa awamu ya pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi. Sasa mtu anaweza kujiuliza, je, tukizungumzia hali ya ukombozi, baadaye siasa ya chama kimoja, na sasa ya vyama vingi, hivi vyote vinatokea kwa bahati mbaya au kuna mpango maalum unaokusudia kutufikisha mahali fulani? Yote mawili yanaweza yakawa majibu sahihi lakini ikiwa kuna mpango maalum, je ni wewe au mimi tunaopanga au tunapangiwa?

Wakati tunatafakari majibu ya maswali haya katika mfumo wa vyama vingi Rais Salmin Amour (CCM) alichukua Urais wa Zanzibar baada ya kuchuana na Seif Sharrif Hamad (CUF). Pamekuwa na mvutano mkubwa kwamba nani hasa alikuwa mshindi kwa kura kiasi cha kuvuta watu kutoka kila pembe ya dunia kujua ukweli wa mambo. Ni vigumu kusema kwamba nia ya kila aliyevutwa katika hali kama hii ilikuwa moja au tofauti. Hatujui hali hiyo katika uchaguzi wa 2000 itakuwaje. Haya ni mambo yanatakiwa kujulikana na kuwekwa wazi kabla ya uchaguzi.
 

Nia ya Dr. Salmin kuwa mgombea 2000

Kuna mafunzo mengi yanayopatikana katika nia ya ama Salmin Amour au ya wapenzi wake kutaka Salmin agombee Urais wa Zanzibar 2000. Mazungumzo ya nia ya kugombea yalijitokeza katika magazeti na vyombo vingine vya habari. Kulikuwa na watu walioshangilia lakini palikuwa na matusi vile vile. Kati ya mambo yaliyomkwamisha Salmin ni katiba ya CCM kuwa mgombea Urais anaweza kukaa sio zaidi ya vipindi viwili. Lakini tatizo halikuwa hili pake yake kwani CCM Zanzibar ilikuwa tayari kubadilisha kipengele hiki ili kumwezesha Salmin aendelee.

Kwa kumchukiza Salmin watu wakasema "Zanzibar ni mkoa", "Rais wa Zanzibar" ni sawa na mkuu wa mkoa kwa mantiki hiyo. Hili likaonekana kama mchezo na utani wa jadi lakini kweli kilichotokea ni kuwa CCM-Zanzibar ikakaa na hapakuwa na maamuzi thabiti kuonesha kuwa wana uwezo wa kubadili katiba hiyo wenyewe kama Wazanzibari. Mwisho wake uamuzi ulitolewa na CCM - Dodoma, kwamba haitawezekana kubadili katiba. Watu wengi walifikiri kuwa CCM-Zanzibar ina uwezo wa kuamua mambo yake na kupeleka CCM-Taifa kama taarifa.

Mafunzo yanayopatikana hapa ni kuwa Wazanzibari hawana uamuzi kwenye mambo yanayoihusu Zanzibar kama walivyokuwa wanafikiri na hivyo ule usemi wa kuwa "Zanzibar ni mkoa" inaokana kama una ukweli kwa namna fulani.

Sasa wa kulaumiwa ni nani? Rais wa Zanzibar ? Wananchi wa Zanzibar? Rais wa Muungano? CCM -visiwani? CCM-Taifa? au nani hasa?

Swali jingine linalojitokeza ni je atakaye chaguliwa kutoka CCM ataweza kuondoa dukuduku za watu wa Zanzibar? Je, watu wa Zanzibar yanawatokea haya kama Wazanzibari au kuna jambo jingine pembeni yake? Je kuna ubaguzi wa ukabila, rangi, jinsia au dini katika maamuzi?

Je, chama kingine cha kisiasa kikipata nafasi ya kuwa mshindi katika uchaguzi unaokuja, matatizo haya yatapatiwa ufumbuzi? Majibu ya maswala haya yapo kwa Wazanzibari wenyewe.
 

Nani atakuwa Rais wa Zanzibar 2000

Tumeshajiuliza maswali mengi yanayohusu uongozij na matatizo ya Wazanzibari. Ni aina gani ya uongozi wanaohitaji ili kutatua matatizo yao na kuimarisha muungano iwapo kwa itikadi yao watakuwa wanaipenda.

Mara nyingi wananchi kazi yao ni kupiga kura lakini hawana sauti kwa kuchagua mgombea wanayemtaka asimame katika kugombea Urais. Kazi inafanywa na kamati ya uongozi wa juu wa vyama vyao vya kisiasa.

Zanzibar ina vyama viwili vyenye nguvu zinazokaribiana, navyo ni CCM na CUF. Huenda vyama hivi vikachagua watu wenye nguvu za kisiasa na wenye ari ya kudumisha haki ya Wazanzibari na vile vile uhusiano mzuri wa kuendeleza muungano. Vile vile huweza kumchagua mtu aliyeduni kuwa mgombea kwa sababu hizo hizo.

Lakini vile vile cha kujiuliza hapa ni kuwa kinachoangaliwa ni yule tu anayependa uzalendo wake na muungano au kuna mambo mengine ya pembeni? Nafikiri kwa kutoweka hali hii wazi mapema ni sawa na kutaka kuwashtukiza watu wakati m uda umebaki mfupi ili wakose cha kufanya. Kwa upande wa Tanzania Bara, angalau inafahamika aliyepo Rais wa sasa hivi atagombea kwa chama chake CCM. Kuna baadhi ya vyombo vya habari vimeanza kutafuta maoni kwa mgombea wa Zanzibar kupitia CCM kitu ambacho CCM-Zanzibar yenyewe ingewajibika kufanya hivyo. Au vipi? Ndio mmeshakuwa mkoa kweli?
 

Hali ya hewa itakuwaje wakati na baada ya uchaguzi

Kwa Tanzania Bara angalau hali ya hewa inafahamika kuanzia sasa hivi itakuwa mbaya na ya hatari labda hali hiyo ibadilishwe.

Serikali kupitia Tume ya Uchaguzi imechagua Wakristu watupu kuwa Wakurugenzi wa uchaguzi (zaidi ya asilimia 90%). Kitu ambacho Waislamu kabla ya wagombea kutangazwa inaonekana kuwa serikali inatafuta ushindi wa kidini - ya Wakristo. Kero ya udini bara ni kitu ambacho haijifichi siku hizi na serikali inaonesha inakusudia kuliangamiza taifa hili katika vita vya kidini kwa kujitakia yenyewe.

Kwa hiyo kwa kifupi iwapo mazingira yanayozunguka uchaguzi haitabadilishwa basi Waislamu wanaanza kusema kuanzia sasa haitakuwa haki na huru. Kwa maana ya kwamba Waislamu wa nchi hii hawatendewi haki na hivyo sio huru (Tazama AN-NUUR 2000, Muharram 1-10). Nchi yenye Waislamu zaidi ya asilmia 50.

Kwa Zanzibar, Waislamu ni asilimia 99, hivyo maudhi yatakayotokea tafsiri yake huenda isiwe ya kidini. Hata hivyo inaweza ikaonekana kuna wafuasi wenye imani ya dhati na imani dhaifu kwa wengine.

Ni wazi kuwa Zanzibar itafurahishwa kuona kuwa kila mwenye uwezo wa kugombea anapewa nafasi hiyo na asibanwe kisiasa ili ashindwe kufanya hivyo. Kwa kufanya hivyo mnajidhalilisha wenyewe.

Hivyo vile vile ni vizuri watakaokuwa viongozi wagombea waandaliwe mapema ili kuepuka kujitokeza athari za udini, ukabila, rangi, jinsia hata utashi binafsi.

Kwa upande wa Bara tungewaomba vyombo ya dini ya Kiislamu wakutane haraka na kuona jinsi ya kutatua matatizo haya ili damu isimwagike kwa kivuli cha serikali kutumia Ukristo.

Na wafanye hivyo haraka kwani licha ya kuwa tume ya uchaguzi imemilikiwa na Wakristo, Kardinali Pengo ametangaza rasmi kuwa kanisa litakuwa na waangalizi wake kila kituo cha kupigia kura ili kuhakikisha "haki" inatendeka!
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook