BARUA


CCM bado haijayajua matatizo ya kilimo nchini

Ndugu Mhariri

USEMI wa kilimo ni uti wa mgongo ni maarufu sana hasa kwa wanasiasa wetu wa Tanzania. Kwa bahati mbaya hakuna jitihada zozote zinazoonekana katika kukipa kilimo chetu uhai. Kutokana na aidha, ukosefu wa sera madhubuti katika kilimo au kukosa viongozi ambao wana nia hasa ya kuinua kilimo chetu, kilimo kimeendelea kuwa kile kile cha mwaka arobaini na saba!

Mifano mingi ishatolewa kuonesha jinsi nchi ambazo ni jangwa zinavyoweza kujitosheleza kwa kilimo na kuuza ziada nchi za nje. Mifano ya nchi za Misri na Saudia ni maarufu miongoni mwetu. Kwa mtazamo wangu tatizo tulilonalo ni wanaoongoza nchi hii (CCM) ama hawajajua matatizo ya kilimo Tanzania au wanajua lakini kutokana na kuendeleza ulaji wanashindwa kufanya lolote katika kukinusuru kilimo chetu.

Taifa la India ni mifano ya yale mataifa ambayo yalikaa chini na kuamua kwa dhati kuwa ipo haja ya kuondokana na tatizo la ukosefu wa chakula nchini mwao. Katika kulitekeleza hilo walianzisha kilichoitwa "Green Revolution". Kutokana na mpango huo maalum wa kupambana na njaa nchini India (Green Revolution) mafanikio makubwa yalipatikana na hadi leo hawana tena tatizo la upungufu wa chakula. Kwa nini, kwa sababu walikuwa na viongozi waliokuwa na nia hasa ya kuwaondolea matatizo ya chakula na wakawaongoza wakulima wao na hadi lengo kufikiwa.

Nasema CCM bado hawajajua matatizo ya kilimo chetu au hawana nia ya kukibadili kilimo hicho kutokana na mazungumzo ya Mhe. Waziri Mkuu mara baada ya kurejea kutoka ziara ya Uchina na Indonesia. Mhe. Sumaye alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa ameongea na wamiliki wa viwanda vya matrekta huko China na wameonesha nia ya kuja kuwekeza hapa nchini kwa kujenga viwanda kama hivyo!!!

Wakati mwingine mtu unaweza ukadhani labda masikio yako ni mabovu kwani siamini kama huo ndio mtizamo wa CCM kuwa kwa kuinua kilimo chetu basi tuanze na ujenzi wa viwanda vya matrekta!! Tunakubali kuwa trekta ni nyenzo muhimu katika kurahisisha kilimo lakini siamini kama kwa hali ya kilimo cha Tanzania tunatakiwa kuanza na hilo!

Tatizo kubwa la kilimo chetu mimi nadhani ni "ukosefu" wa maji kwa ajili ya umwagiliaji na masoko kwa mazao ya kilimo. Labda inabidi tuwape shahada za uvumilivu wakulima wa Tanzania kwani wamekuwa wakionesha jitihada kubwa katika kilimo ila wanakwamishwa na mvua. Hivi kilimo cha kutegemea mvua wakati nchi imezungukwa na maji pande zote tutafika kweli? Mhe. Sumaye anataka kutueleza kuwa tukiwagawia wakulima wetu kila mmoja trekta lake leo basi kilimo kitabadilika? Ingeingia akilini kama ziara ya waheshimiwa hao ingekuja na maelezo kuwa wamepata wawekezaji katika miradi ya umwagiliaji, kuboresha barabara wilayani na vijijini, upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora na mbolea na si kujenga viwanda vya matrekta.

Wakulima wenyewe hata majembe ya kukokotwa na ng'ombe hajayaweza kuyamiliki sisi tunaongelea kuwajengea viwanda vya matrekta! Kama hayo ndiyo mawazo ya CCM basi tusitegemee kuwa kuna lolote la maana zaidi ya kuimbishwa tu kuwa "kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu".

Kuna mifano mingi ya kuonesha kuwa hawa watu bado hawajajua wanachotaka kufanya kuhusu kilimo hapa nchini. Mfano mdogo ni Wizara ya Kilimo ambayo tunategemea ndiyo itufikishe huko tunakokwenda. Miradi inayopewa umuhimu zaidi ambayo tunadhani ndiyo yenye ulaji ndani ya Wizara hiyo ni ile inayohusiana na "Extension". Magari ya Kifahari kibao utayakuta yanahusiana na usambazaji wa taaluma kwa wakulima (extension).

Tunatumia gharama kubwa kuwapelekea utaalamu wakulima wakati hatujaandaa mazingira mazuri ya kuwawezesha hao wakulima kupokea hizo "innovations". Nasema hatujaandaa mazingira mazuri kwa sababu sijui kama hao wakulima watatumiaje huo utaalamu wakati muda mwingi wanautumia misikitini na makanisani wakiomba mvua!! Ingekuwa tuna watu makini wenye uchungu na kilimo chetu wangeuza hayo "mashangingi" ya "extension" halafu gharama zake zipelekwe kwenye miradi ya umwagiliaji.

Alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara huko Ugweno - Kifula wilaya ya Mwanga, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba aliwaambia wasikilizaji wake kuwa ni kweli kuwa CCM ina wenyewe lakini wenyewe hao hawako Ugweno kwani wangekuwa Ugweno, Wagweno wasingepata taabu ya kusubiri mvua wanapolima maeneo ya tambarare ya Butu wakati ziwa Jipe liko jirani nao! Gharama ya "Shangingi" moja tu la Mbunge inatosha kabisa kununua pampu za kutosha kuyafanya maji ya ziwa Jipe yatumike kwa kilimo kwenye maeneo hayo!! Alizidi kuwaweka wazi kuwa wakati maparachihi (Avocado) yanaliwa na komba huko kwao jirani zao wa Kenya wanasafirisha Ulaya na kupata pesa za kigeni!!

Labda nimalizie kwa kusema kuwa wakulima wetu wako tayari kubadili kilimo chao lakini hawajapata viongozi thabiti wa kuwafikisha huko kwenye mabadiliko. Hivyo basi wakati umefika wa kuwaweka viongozi wanaoonesha nia ya kuleta mabadiliko na si hawa ambao kila mwaka wanawasumbua Masheikh na Maaskofu waombe dua za mvua wakati Mwenyezi Mungu alishatupa maji kibao tunashindwa kumwagilia tu mashambani!

Mvungi, M.F.
Morogoro.


Tujihadhari na 'Kibwetere' wa siasa

Ndugu Mhariri

KATIKA gazeti moja la kila siku toleo Na. 1447, Brigedia mstaafu F. Mbena ameandika makala inayozungumzia viongozi wa Kikristo waliovuta watu wengi na hatimaye wakawaangamiza.

Alitoa mfano wa Jim Jones huko Amerika ambaye mahubiri yake ya Biblia yaliwavuta wengi lakini hatimaye yeye na Wakristo waliokuwa pamoja naye katika imani walijiua kwa kunywa sumu. Hoja waliyoegemea katika kunywa sumu ni maisha bora ya baadaye.

Brigedia akatoa mfano wa kiongozi mwingine wa Kikristo David Koresh ambaye pia alipata wafuasi wengi huko Texas na hatimaye (sera) na mahubiri yake vikawapelekea kujichoma moto na wafuasi wake.

Brigedia akatoa mfano wa mwisho wa hivi karibuni katika nchi jirani ya Uganda ambapo Padri Mkatoliki Joseph Kibwetere anayedaiwa kutoka Ukatoliki aliwaburuza mamia ya watu na hatimaye kuwatumbukiza katika janga la kuangamia kwa moto.

Miongoni mwa sifa za viongozi hawa alizozitaja ni tatu: Mosi, kuwa wasemaji wazuri. Pili, walaghai na tatu, wakati mwingine hutumia vitisho.

Mwisho amewataka Watanzania wajifunze kutokana na matukio haya.

Mimi napenda kumuunga mkono Brigedia kutokana na wito wake. Watu wa aina ya Kibwetere hawapo katika dini tu. Hata kwenye siasa wapo.

Sisi hapa Tanzania tuna CCM. Hakuna tofauti kati ya sifa za viongozi wa CCM na kina Kibwetere katika kutoa ahadi tamu tamu. Tofauti tu hawaahidi kufika mbinguni haraka kwa kujichoma moto.

Ahadi walizotoa toka mwaka 1961 za kuboresha maisha ya wananchi ni ahadi hewa. Wito wa kufunga mikanda kwa miezi 18 umekuwa ndio mtindo wa maisha. Wananchi wanafunga mkanda juu ya mkanda.

Watanzania hivi sasa njaa, ukosefu wa dawa na huduma kama maji safi na salama imekuwa jambo la kawaida.

Maafa yote haya yanayowakumba Watanzania yametanguliwa na ukusanyaji kodi kubwa bila kutoa huduma za jamii.

Kibwetere alikusanya mali za waumini wote kisha akawaangamiza.

Wananchi tuwe macho na ahadi tamu tamu tusijenasa tukaangamia.

Mohammed Katunka,
Temeke,
Dar es Salaam.


Mwembechai hawakuuliwa kwa mapanga

Ndugu Mhariri

NAPENDA unipe nafasi ili nitoe dukuduku langu kutokana na hotuba ya Rais Aprili 10, mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine aliyoyazungumzia, pia alizungumzia amani na kututaka wananchi tuepukane na vurugu na jiko kwa jino na ugawaji wa mapanga unaofanywa na wanasiasa wa chama fulani.

Napenda Mhe. Rais aelewe kuwa wananchi hivi sasa tumekwenda shule na tunaelewa baya na zuri na ule wakati wa ndiyo ndiyo sasa basi (kuburuzwa).

Naomba wananchi wenzangu tuwe makini na viongozi wetu hawa wa CCM wanaojaribu kututisha eti ili waendelee kututawala na sio kutuongoza. Mhe. Rais anataka tuwe "kichogo kwa kichogo? (kutuburuza). Sasa ni wakati wa jino kwa jino, pua kwa pua.

Kuhusu mapanga: Mwembechai hawakuuliwa kwa mapanga. Mapanga kwanza hayatishii amani kwa namna yoyote. Vipi polisi wanawatwanga risasi wananchi wasiokuwa na mapanga pale Mwembechai. Mbona hatukutahadharishwa wananchi kuwa macho na risasi za moto za serikali yake, leo iweje atutahadharishe na mapanga ya kukatia katia miti mashambani? Dhulma ndiyo itakayosababisha uvunjikaji wa amani.

Shabani M. Ungando,
Tandale,
Dar es Salaam.


CCM elezeni cheo cha Makamba

Ndugu Mhariri

UZOEFU umeonesha, Yusufu Makamba (RC Dar) amekuwa msemaji mkuu wa CCM katika mambo ya dini hasa katika kukabiliana na Uislamu.

Syprus walikuwa na Askofu wao Makarios na hawakuwaficha wananchi kuwa Makarios ni Askofu wa dola. Lakini lakushangaza CCM hawatuelezi cheo cha ziada cha Makamba.

Mpaka sasa hatujui kama Makamba ni Mchungaji wa CCM, Sheikh, Muft au Paroko wa chama hicho.

Juzi hapa kaibuka na madai kuwa eti watu wakawaulize Masheikh ni wapi Mtume Muhammad (s.a.w.) aliwausia wahubiri siasa.

Lakini yeye kama RC na Kada wa Chama hajasema ni wapi katiba ya nchi au ya chama chake inamruhusu kuhubiri dini.

Mwezi huu tarehe 7, kupitia gazeti la dini (sio AN-NUUR) Kanisa Katoliki limetoa tamko kuwa lazima uchaguzi unaokuja viongozi watoke ndani ya Kanisa.

Na siku chache baadaye Polycarp Kadinali Pengo amesisitiza kwa kusema kuwa Kanisa Katoliki litaweka wasimamizi katika kila kituo cha kupigia kura.

Jambo la kushangaza msemaji huyu wa dini wa CCM mpaka sasa hajatutuma tukamuambie Pengo Yesu hakuwatuma Maaskofu wahubiri siasa.

Mshana Ramadhani,
Arusha.


CCM yamuomba radhi Kakobe?

Ndugu Mhariri

ASKOFU Kakobe katoa wito kwa Watanzania kutoichagua CCM katika uchaguzi wa Oktoba.

Katibu Mkuu wa CCM amedai kuwa CCM imemsamehe Kakobe kwa kauli hizo.

La kushangaza ni kwamba chama hicho huwatia ndani viongozi wa Kiislamu pale wanapokikosoa kwa vitendo vyake vya dhulma.

Hapa ndipo tunapoamini kuwa kauli za Kakobe zimewaamsha Wakristo wasio Wakatoliki na hivyo CCM wanalazimika kumuomba radhi "kisayansi".

Abdallah Kheri,
Mburahati,
Dar es Salaam.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook