Swali kwa Ngula
Leo nashika kalamu, Ngula ninakuuliza,
Mjini Dar es Salaam, kampeni kutangaza,
Watu kututia hamu, Bungeni kukuingiza,
Mambo uliyoyasema, mbona hujayatimiza?
Kabla hujawa Mbunge, Ngula ulituambia,
Wananchi wa Ubungo, maji ntawapatia,
Wananchi kwa usongo, kura tulikupigia,
Mambo uliyoyasema, mbona hujayatimiza?
Wakati wa kampeni, Ngula ulihangaika,
Kuanzia Magomeni, hadi Mbezi ukafika,
Sasa uko bungeni, watu wamesahaulika,
Mambo uliyoyasema, mbona hujayatimiza?
Siku zinazidi kwisha, mambo hujayatimiza,
Hutaki kuturidhisha, vitu ulivyoeleza,
Wazidi kutuzungusha, bila kutupa mwangaza,
Mambo uliyoyasema, mbona hujayatimiza?
Kama hutotupatia, Ngula tunakuambia,
Kiti ulichokalia, utakuja kijutia,
Tutasita kupigia, kura inayofuatia,
Mambo uliyoyasema, mbona hujayatimiza?
Naweka chini kalamu, nikiwa ninahuzuni,
Ninasubiri kwa hamu, nikiwa nipo jimboni,
Kwani umeshafahamu, wajibu wako bungeni,
Mambo uliyoyasema, mbona hujayatimiza?
Aziza A. Mangosongo,
S.L.P. 72834,
Dar es Salaam
Lo! Umeshika shavu, uso umekunjamana,
Na umekaa kivivu, mbona unawaza sana?
Nini au ni uchovu, wa shughuli za mchana?
Usiwe nayo huzuni, huzuni inakondesha.
Huzuni inakondesha, pia mawazo mazito,
Taona mtu aisha, kama maji ya kijito,
Hadi aanze kutisha, abaki kama ufito,
Furahi ndugu furahi, nasema tena furahi.
Ni mali zimekwishia, au msiba mepata?
Ayubu livumilia, japo misiba alipata,
Alijua akilia, siyo dawa ya matata,
Likuja ukiwa tupu, utarudi tupu tupu.
Dunia inayo dhiki, lakini jipeni moyo,
Majanga misiba chuki, hayo yetu yote hayo,
Taabu zipo lukuki, hutupigisha miayo,
Siku moja zitakoma, hiyo siku ya kiama.
Jambo kubwa wanadamu, maisha kuvumilia,
Ibada iwe muhimu, kwa Muumba kimbilia,
Siku moja ufahamu, utaiaga dunia,
Na peponi ukienda, utafurahi na Bwana.
ISamweli 1:8-15 Esta 9:22
Luka 22:45-46 2 Kor 7:10
Mwinjilisti
B.E. Dettu
S.L.P. 60474,
Dar es Salaam.
Hasira kweli hasara, imehasirisha wengi,
Mtu kuwa na harara, aweza vunja mtungi,
Akivimba na kufura, tadhani mevuta bangi,
Balaa anaitaka!
Hasira kweli upofu, mtu kushindwa kuona,
Akatweta bila hofu, mzee au kijana,
Akaleta usumbufu, wa majanga kutana,
Uiepuke hasira.
Hasira meacha mke, watoto wakaumia,
Leo tu na kesho yake, tayari meinamia,
Ona mebaki mpweke, moyoni unaumia,
Uwe mtu wa subira.
Hasira kweli ujinga, mtu kufanya vituko,
Na mambo akagananga, kisha akaketi kitako,
Tayari kuchuma janga, kaleta misukosuko,
Hasara anaitaka.
Hasira kweli yaua, na tena inaumiza,
Sione kama maua, moyoni ukiwaza,
Na ghafla unatimua, tayari unachakaza,
Watakufunga maisha!
Mithali 15:18 Mithali 15:1-2
Mithali 19:19 Mhubiri 7:9
Mithali 17:14
Mwinjilisti
B.E. Dettu
S.L.P. 60474,
Dar es Salaam.
CCM namba 'wani' kwa kila ovu (1)
Jinale ilojiita, CCM namba 'wani',
Ni jina lenye utata, si sasa tangu zamani,
Ni Chama Chenye Matata, kwa uongo namba 'wani',
Kama Chama Cha Udini, CCM namba 'wani'.
Ubovu wa CCM, mkubwa ndugu zanguni,
Napenda muufahamu, ili wasiwarubuni,
Oktoba ni awamu, ya kuwapa wapinzani,
Kama propaganda, CCM namba 'wani'.
CCM namba 'wani', kwa kila ovu nchini,
Watu tupo taabani, mijini na vijijini,
Lakini nawashangaeni, mwaipendea kwanini!
Kama kwa ulaghai, CCM namba 'wani'.
Ahadi nyingi za hewa, huwa wanawapeni,
Mfano mnaambiwa, muwapo kampenini,
Mabomba mtawekewa, na madawati shuleni,
Kama sera za uongo, CCM namba 'wani'.
Siasa za Ujamaa, chanzo cha umaskini,
Ni sera zisizofaa, wananchi zipingeni,
Muwe watu mashujaa, kunyanyaswa kataeni,
Kwa kubuni sera mbovu, CCM namba 'wani'.
'Ka nchi sasa kanuka', haki haipatikani,
Sheria ukiitaka, fedha iwe mkononi,
Nchi imeharibika, shime tuiokoeni,
Kwa matatizo ya rushwa, CCM namba 'wani'.
Saba natamatia, kalamu naweka chini,
Kheri nawaombea, wasomaji gazetini,
Ni ninyi malenga pia, wote nawasalimuni,
Chonde chonde wananchi, CCM haitufai.
Mtagaluka Rashid (Mtaaluma),
P.O. Box 16388,
Dar es Salaam.
Msimamo
Msimamo ndugu zangu, Shemdoe nausia,
Kwa wote sipeke yangu, Bwana Mola atwambia,
Wito wa Mungu si wangu, FARADHI kuitikia,
Katika kujikomboa, MSIMAMO ndio njia.
Tanga mpo ndugu zangu, jana umwinyi si njia,
Chukizo kubwa kwa Mungu, msimamo ndio njia,
Vipi CUF wenzangu, msimamo kususia?
Katika kujikomboa, MSIMAMO ndio njia.
CUF cha pendwa na Mungu, HAKI tupu chapigia,
Yani mwa muasi Mungu, HAKI SAWA kukimbia,
Kina wote wacha Mungu, dini zote Tanzania,
Katika kujikomboa, MSIMAMO ndio njia.
Ili tumwabudu Mungu, msimamo ndio njia,
Watanzania wenzangu, CUF mwiko kususia,
Tusimame ndugu zangu, HAKI tupu kupigia,
Katika kujikomboa, MSIMAMO ndio njia.
Ili kupata HAKI, ELIMU na TIBA pia,
MSIMAMO bwana tiki, DHULMA itakimbia,
Wengi waliuafiki, mavuno wakajilia,
Katika kujikomboa, MSIMAMO ndio njia.
Sifa hauongelei, MSIMAMO nawambia,
Kwa uchache tuafiki, HAKI tuje simamia,
Hapa kwangu nimetiki, Mtagaruka sikia,
Katika kujikomboa, MSIMAMO ndio njia.
Almasi H. Shemdoe,
'Tunda la Matumaini'
S.L.P. 33265,
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |