TAHARIRI

Japo wamechelewa, wamesema kweli

KITABU, "Uchaguzi wa Kisiasa kwa nini Tujali", ni hazina ambayo kila mwananchi anawajibika kuwa nayo.

Na ilivyokuwa ni wajibu kuutafuta ukweli na kuujua, basi kila mtu ahakikishe anakinunua kitabu hiki na kukisoma kwa makini. Itakuwa ni kosa kubwa kutosheka na maneno ya kusikia.

Qur'an (4:135) inawataka Waislamu wawe waadilifu. Watoao ushahidi wa kweli hata kama ni dhidi ya nafsi zao au waliowapenzi wao.

Kwa mtizamo huo huo, mtu hapokonywi haki yake kwa sababu ya sura yake, jina lake, dini yake au matendo yake ya nyuma. Na kweli inabakia kuwa kweli bila kujali nani kaisema.

Wametokea wasomi wa Kikatoliki wametizama mwenendo wa nchi hii wanasema, hali ni mbaya sana.

Wanasema, watu wamekata tamaa. Wanajisikia kwamba vyama na viongozi waliochaguliwa (1995) wameshindwa kutekeleza ahadi zao.

Aidha, wanasema, Ilani za uchaguzi zilitumika tu kama njia ya kuwavuta watu kuwapigia kura. Kwa ajili hiyo wanasema, wanasiasa "waliochaguliwa wanaonekana kushughulikia matakwa yao binafsi au sana sana maelekezo ya vyama vyao badala ya kutilia maanani na kuweka mikakati ya kutekeleza mahitaji ya watu...".

Lakini jingine wanalotutahadharisha ni kuwa, wakati mwingine siasa huambatana na matumizi mabaya ya madaraka kutokana na uovu au mvuto wa kutimiza malengo binafsi.

Tahadhari hii ni muhimu kuizingatia, kwani haiwezi kuwa pasipo na matumizi mabaya ya madaraka watu wauliwe kama ilivyotokea pale Mwembechai, halafu serikali yenyewe isimame kidete kuzuia shauri kufika mahakamani na kuundwa tume huru ya uchunguzi.

Tunachosikitika wanataaluma hawa wa Kikatoliki (Christian Professionals of Tanzania) wamechelewa sana. Lakini maadhali wameona huenda ikawa hatua muhimu katika kurekebisha mwenendo wa nchi yetu.

Toka ufanyike uchaguzi mwaka 1995 mambo mengi makubwa yametokea yenye kuiathiri jamii.

Mashirika mengi ya umma, makampuni, migodi ya madini na hata benki pekee ya Taifa ya Biashara imeuzwa. Japo wananchi walipinga sana kuuzwa Benki hiyo, lakini ndio imeuzwa.

Lilipoibuka suala la ubinafsishaji wa biashara ya silaha, nalo wananchi walipiga kelele sana kupinga. Lakini kelele zao hazikusaidia kitu.

Ni katika mazingira hayo, wataalamu hawa Wakikatoliki wanasema, wanasiasa waliochaguliwa wanaonekana kushughulikia matakwa yao binafsi; na wala hawana nafasi ya kusikiliza malalamiko na matarajio ya watu.

Hata hivyo, wametahadharisha jambo moja la msingi; "Watu hujipatia uongozi ambao ni stahiki yao. viongozi wanaweza kutumia vibaya madaraka kwa sababu tu watu wanaowaongoza wanawaruhusu kuchezea madaraka". (Uk. 19).

Kwa mfano, kama Waislamu wamekuwa dhaifu na woga kiasi cha kushindwa kuhoji ni kwanini Tume ya Uchaguzi, Waratibu na Wasimamizi wa Uchaguzi, Wakuu wa Wilaya na watendaji wengine muhimu serikalini wamekuwa Wakristo watupu (ila kidogo tu) nchi itaendelea kuwa na viongozi wasiojali uwepo wa Waislamu.

Au kama Waislamu hawajajifunza namna ya kutoa changamoto kwa viongozi wanaopokea shinikizo toka kwa Paroko; nchi itaendelea kuwa na uongozi unaowalinda watu waliotoa amri "piga yule" na watu wakauliwa baada ya kuvamiwa Msikitini.

Lakini pia tatizo la udini halitaondoka iwapo Waislamu hawatokuwa tayari kuhoji mantiki ya "Rais kuwa Rais pia wa wanywa pombe na wala nguruwe, halikadhalika asiyepuuza maoni ya Wakristo katika suala la OIC. Lakini msimamo huo hauonekani katika kuuliwa Waislamu Mwembechai, mazizi ya mabucha na nguruwe yanayowekwa maeneo yenye Waislamu, mamlaka za nchi kumilikiwa na Wakristo na azma ya Waislamu kujiunga na OIC.

Wanachosema wataalamu hawa wa Kikatoliki ni kuwa: "Kama watu ni wakimya na wasiotaka kubainisha matakwa yao basi hawa watasubiri kuongozwa tu, na hivyo watachagua uongozi ambao utawaongoza kwa kuwaburuza hasa katika maamuzi na kuunda sera". (Uk. 3)

Na Qur'an inasema: "Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo katika nafsi zao". (13:11).

Kama watu hawataondoa shirki ya kuwaogopa watu kiasi cha kushindwa kuuliza chochote, wakati mtu mwenye madaraka anapowaeleza kitu hata kama wanajua sio sahihi, basi wasitegemee Allah ashushe malaika wauondoe uongozi huo.

Kwa mtazamo huo huo, wasomi hao wa Kikatoliki wanasema hawapaswi kupiga kura na kuishia hapo tu, bali wanapaswa kuwaambia wanasiasa ni namna gani wanataka waongoze nchi.

Wanahoji; "Wakati vyama vya kisiasa kupitia Ilani zao za uchaguzi viliahidi kuboresha Elimu ya Msingi, maji, barabara, mfuko wa ajira kwa vijana ni kwa kiwango gani katika hali halisi tunaweza kusema matamko yao yalikuwa ya ukweli na ambayo wangeweza kuyatekeleza?

Ni wazi walioandaa Ilani hizo walijua kabisa kwamba ahadi hizo zisingeweza kutekelezeka".

Kama tulivyogusia awali, wataalamu hawa wanasema, kumekuwepo uongozi uliojaa rushwa, huku viongozi wakishindwa kutekeleza ahadi zao. Hali inayoonesha kuwa Ilani za Uchaguzi zilitumika tu kama njia ya kuwavuta watu kuwapigia kura.

Yote haya yamewafanya wananchi wakate tamaa.

Kama sehemu ya jamii ya Tanzania, wanasema, hawawezi kuikimbia hali halisi kwa kujificha makanisani wakisali kuomba maovu yaondoke. Bali watashiriki kuyaondoa. Wanasema: "Kama Wakristu tunaitwa kuathiri shughuli za kisiasa hivyo kwamba ziweze kuhudumia jamii kulingana na matakwa na mpango wa Mungu".

"Hatuwezi kuikimbia hali halisi kwa kujificha makanisani tukisali kuomba maovu yaondoke".

Kauli hii ni sahihi kwani Mtume (s.a.w.) anasema: "Yeyote miongoni mwenu atakayeona jambo ovu, na aliondoe kwa mkono wake, kama hawezi, na aliondoe kwa ulimi na kama hawezi alichukie moyoni mwake...". [Muslim]

Katika mazingira haya ya uchaguzi, ina maanisha kuwa ni lazima watu washiriki kwa kauli na vitendo kuweka uongozi unaofaa. Uongozi mbovu hauondolewi, wala mzuri kusimikwa kwa itikafu pekee na kutamka "Laanatullah" Misikitini au kwenye mihadhara.

Wanataaluma wa Kikatoliki wanasisitiza kuwa maadhali wanasiasa ni watumishi wa watu..."Kama hawatumikii watu inabidi wapigiwe kura ya kutokuwa na imani nao na waondolewe madarakani".

Na wanasisitiza kuwa, ni wale tu washiriki wazuri katika masuala haya ya siasa ndio watajaalia kuwepo uongozi ulio tayari kuwasikiliza na kushirikiana nao katika kutekeleza matakwa yao.

Kwa maana wale watakaofumbia macho mambo yanayoendelea katika siasa kwa kuogopa kuambiwa wanachanganya siasa na dini, hao hakuna atakayewajali.

Naam, haishangazi kuona jinsi Masheikh walivyodhalilishwa katika kadhia ya mabucha ya nguruwe, Mwembechai na serikali kudiriki kuteua Wakristo watupu katika sehemu muhimu.

Kwanini ijali haliyakuwa anajua Masheikh wamejificha Misikitini wakivuta uradi.

Bali, kinyume chake haithubutu. Inajua nini kitatokea kutoka kwa Maaskofu.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook