Kipindi cha Muelekeo RTD kiendeshwe kitaalamu

Na Ahmed Hussein

NIMEKUWA nikifuatilia kwa makini kipindi cha muelekeo cha Radio Tanzania tokea pale kilipoanzishwa. Nakiri kwamba kipindi hicho ni muhimu mno katika wakati huu ambapo Taifa letu linaelekea kwenye kindumbwendumbwe cha uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na madiwani. Kwa sababu hiyo sina budi kumpongeza Mkurugenzi wa Radio hiyo kwa kuweka kipindi hicho.

HATA HIVYO, ningependa kushauri kwamba kipindi hicho kiendeshwe kitaalamu zaidi kwa kuzingatia nafasi, hadhi na uzoefu wa Radio Tanzania. Nasema hivyo kwa sababu maudhui ya vipindi vya majuma mawili yaliyopita yamedhihirisha muelekeo wa kishabiki unaoashiria kuukandamiza upande wa upinzani kwa maslahi ya chama tawala, jambo ambalo linaharibu ladha ya kipindi na kukipotezea maana.

Badala ya kutupatia habari zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi wa kitaaluma kuhusiana na uchaguzi, kipindi cha muelekeo kinakariri propaganda zisizo na ushahidi yakinifu. Kitendo cha kuwahoji watu wasiojulikana kuhusu mienendo ya vyama fulani kwa kweli kinakinzana na hadhi ya Radio ya Taifa.

RTD kama Radio ya Taifa haipaswi kabisa kuokota habari au maneno yasiyo na ushahidi wa kisayansi. Hii ni kwa sababu chombo hicho kina uwezo na mtandao mkubwa wa kupata habari sahihi kutoka vyanzo na vyombo vinavyostahiki kuzungumzia jambo husika.

Mathalan, kuhusu dai la udini dhidi ya chama fulani, si sahihi kumpa fursa mtu asiyejulikana kuzungumzia suala hilo kwani ni vigumu kufahamu mtu huyo ana hisia na mtazamo gani juu ya chama kinachotuhumiwa.

Aidha, si rahisi kujua huyo mtu ana uwezo gani wa kiakili na kitaaluma na amefanya utafiti kwa kiwango gani kuweza kutoa ushahidi madhubuti juu ya jambo hilo kiasi cha Radio ya Taifa kumpa nafasi ya kusema (redioni).

Kwa mtindo huo, upo uwezekano wa kumpa nafasi mwanachama au shabiki wa chama fulani azungumzie chama kingine, hapa ni muhali kupata maelezo sahihi. Vyovyote vile muhusika atazungumza kwa maslahi ya chama chake na kwa ajili hiyo lazima akiponde chama pinzani hata kwa kauli za urongo.

Katika kutafuta ukweli juu ya suala la udini, RTD ingepaswa kuwaalika viongozi wa chama kinachotuhumiwa kwa upande mmoja na viongozi wa dini inayotuhumiwa kwa upande mwingine. Hawa kwa pamoja wangetupatia muelekeo sahihi kama lilivyo jina la kipindi chenyewe.

Kwa mantiki hiyo, katika kipindi cha juma lililopita RTD ingewapa nafasi viongozi wa chama kinachoshutumiwa badala ya kumtumia "kijana Fowadi" azungumze kwa niaba ya chama hicho!

Si vibaya kwa RTD kuelezea matatizo ya vyama lakini lazima iwe makini mno inapochambua matatizo hayo. Isitoshe matatizo hayo hayavikabili vyama vya upinzani pekee.

Hivyo basi, ni vema pia RTD ichambue matatizo ya chama tawala ambayo ni makubwa zaidi. Chama hicho kinakabiliwa na shutuma nyingi zenye ushahidi ulio dhahiri shahiri juu ya matatizo ya kijamii, kiuchumi, kidemokrasia, kikatiba na kadhalika, yote yakiwa ni matokeo ya kushindwa kutekeleza ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 1995.

Zaidi ya hayo, chama tawala na serikali yake navyo pia vinatuhumiwa kwa udini na walalamikaji wametoa vielelezo kadhaa wa kadhaa kuthibitisha tuhuma hizo. Mojawapo ya vielelezo hivyo ni muundo wa tume ya uchaguzi ambao haukuzingatia uwiano wa kidini ambapo kwa asilimia tisini wasimamizi walioteuliwa ni watu wa dini moja.

Kana kwamba hilo halitoshi, Kanisa Katoliki nalo linasema kuwa litaweka wasimamizi wake. Chama na serikali vimenyamaza kimya! Hata RTD haijasema chochote!

Kwa kutilia maanani unyeti wa suala hilo, yabidi kipindi cha muelekeo kizungumzie jambo hilo kwa kuwahoji wale walioteua watu wa dini moja kwa asilimia kubwa na wale waliotoa kitabu kuhusu siasa ilihali wao ni wanadini.

Haitakuwa busara kwa RTD kuzungumzia propaganda dhidi ya chama au dini pasipo ushahidi na kuacha kuzungumzia suala kama hilo lenye ushahidi wa moja kwa moja kupitia kipindi cha muelekeo, ni muhimu watu wa dini zote wapewe nafasi ya kujibu shutuma za kuchanganya dini na siasa na kuelezea mitazamo ya dini zao juu ya siasa.

Napenda kuitanabaisha Radio yetu ya Taifa kuwa hivi sasa wananchi wanahitaji zaidi ukweli wa mambo kuliko blaablaa na propaganda. Watanzania wa leo wana uwezo wa na upeo mkubwa wa kuchambua na kuchuja mambo hivyo, kuyaeleza mambo kinyume na ukweli wake kwa minajili ya kuwakoga watawala wanapinzana na mawanda ya wasikilizaji jambo ambalo linaigharimu heshima na haiba ya Radio ya Taifa.

RTD iachane na yale maono ya enzi za ukiritimba wa habari ambapo wananchi walilazimika kuamini kila kilichosemwa Radioni! Kutokana na uhuru wa vyombo vya habari uliopo, ni vigumu kumuhadaa kihabari mwananchi wa leo tofauti na ilivyokuwa kwa mwananchi wa miaka ya sitini, sabini na themanini. Kung'ang'ania mfumo wa habari za kisiasa wa miaka hiyo kuna maana ya kuvipa ushindi wa chee vyombo huru na makini vya habari.

Mara nyingi watu wengi huamua kufungua stesheni za Radio nyingine kusikiliza japo muziki kuliko kusikiliza vipindi kama "Muelekeo" au "Maneno hayo" kwa sababu ya kuchoshwa na fikra za miaka ya nyuma za kutetea watawala, chama au serikali licha ya kufanya kwake makosa.

Hata hivyo, nyuma mtindo huo uliwafanya watu wengi wajitenge na siasa na hivyo siasa ikawa mali ya viongozi na makada wa chama. Kwa hali hiyo hata habari za kurasa za mbele za magazeti ya chama zilikuwa hazisomwi na wengi. Wengi walikuwa wakinunua magazeti hayo kwa ajili ya kusoma habari za michezo hususan zilizohusu Simba na Yanga.

Lakini baada ya kuibuka vyombo huru vya habari pamoja na demokrasia ya vyama vingi watu wengi sasa wanasoma zaidi masuala ya kisiasa, na kupendelea sana habari zinazoikosoa serikali kuliko hata za michezo.

Pasina shaka, magazeti ya zamani yamepoteza nguvu na umaarufu kwa sababu hiyo. Kuwapamba viongozi wa chama na serikali hata pale wanapokosea.

Viongozi wanabomoa nchi, vyombo vya habari vya chama na serikali vinashabikia, matokeo yake tumefika hapa tulipo!

Naiasa RTD kutoa habari kwa maslahi ya nchi na wananchi. Na habari hizo zitafitiwe na kuchambuliwa kitaalamu kabla ya kuzirusha hewani. RTD kama Radio ya Taifa, iepuke ushabiki wa kisiasa na isitumiwe kupiga vita upinzani na demokrasia. Vile vile isitumiwe kuendeleza siasa za ulaghai za miaka iliyopita ambazo zimeliangusha Taifa letu.

Mashauri yaliyotolewa katika semina ya waandishi na watangazaji wa RTD kule Dodoma hayana budi kufanyiwa kazi ili kwenda sambamba na wakati. Mtindo wa kuandika au kutangaza habari kwa maslahi ya chama na serikali wakati wake umekwisha.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook