MAMIA ya waumini wa Kiislamu kutoka vitongoji mbalimbali vya mji wa Tanga na wilaya zake juzi walishiriki katika mazishi ya Sheikh Jumbe Tajiri aliyekuwa Sheikh na Imamu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Sunni Jamat ya mjini Tanga.
Sheikh Jumbe ambaye baadaye alibadili jina na kuitwa Sheikh Abubakar Suleman alifariki dunia wiki iliyopita nyumbani kwake eneo la Chumbageni mjini hapa na kuzikwa kijijini kwao Muheza.
Kwa mujibu wa mtoto wake Sheikh Shauri Abubakar, Sheikh Jumbe alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Jeneza la Sheikh Jumbe lilitolewa nyumbani kwake na kubebwa mikononi na waumini waliokuwa wamejipanga barabarani kutoka Chumbageni hadi ulipo Msikiti wa Sunni Jamat umbali wa kilometa mbili.
Maiti ya Sheikh Jumbe ilisaliwa baada ya sala ya adhuhuri. Sala hiyo ilihudhuriwa na Masheikh mbalimbali wa mjini hapa akiwemo Sheikh Ali Mkanga.
Akizungumza baada ya kuswaliwa kwa maiti, Sheikh Mkanga alimtaja marehemu kama mtu aliyekuwa muadilifu na mcha Mungu aliyetoa elimu yake kwa wengine ili kufuta ujinga.
Alisema, Sheikh Jumbe atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika uenezaji wa elimu ya dini ambao wanafunzi wake wengi hivi sasa ni walimu waliofungua madrasa sehemu mbalimbali hapa nchini.
Baada ya hotuba fupi, marehemu alisafirishwa kwenda kijiji cha Kibaoni tarafa ya Mlingano Muheza na kuzikwa.
Sheikh Jumbe alizaliwa mwaka 1914.
Alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wakubwa wa Sheikh maarufu wa Afrika Masharki wakati huo, Sheikh Ali bin Hemed ambaye ni chimbuko la Masheikh wengi maarufu hapa nchini.
Miongoni mwa Masheikh waliosoma elimu sambamba na marehemu Sheikh Jumbe kwa Sheikh Ali bin Hemed ni pamoja na Sheikh Mkanga na Mufti wa Bakwata Sheikh Hemed bin Jumaa bin Hemed.
Sheikh Jumbe baada ya kuhitimu elimu yake alichukuliwa na jumuiya ya Sunni Jamat ambako alifundisha madhehebu ya Hanafiya.
Miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Jumbe ambao sasa ni Masheikh ni pamoja
na mtoto wake Sheikh Shauri Abubakar na mwingine ni Mhadhiri maarufu hapa
nchini Sheikh Abdallah Bawazir anayefundisha jijini Dar es Salaam.
MWENYEKITI wa Baraza Kuu mkoa wa Morogoro, Sheikh Ayubu Muinge amechaguliwa kuwa Sheikh Mkuu wa Msikiti wa Uwanja wa Ndege (Dini moja Mungu mmoja) katika uchaguzi uliofanywa na waumini wa Msikiti huo Jumapili iliyopita.
Nafasi ya Imamu wa Msikiti huo ambao ni maarufu mjini hapa, ni mmoja kati ya Misikiti mingi maarufu nchini, inashikiliwa na Ustadh Abdallah Kombo, ambapo Bw. Shomari Mtogo amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Msikiti huo.
Pia waumini hao wamemchagua Bw. Juma Chunga kuwa Katibu na Mzee Mkwakwani kushika nafasi ya utunzaji fedha za Msikiti huo.
Aidha, Msikiti umepata wajumbe watatu ambao wataungana na viongozi hao na kuunda kamati ambapo waliochaguliwa ni Mzee Ramadhani, Hamim Lilumba pamoja na Mohammed Kigadu.
Akitoa nasaha zake mara baada ya kuchaguliwa, Mwenyekiti wa Msikiti huo Bw. Shomari Mtogo alisema kuwa yeye na viongozi wenzake watahakikisha kwamba Msikiti huo unaendelea kuwa kituo cha harakati za Kiislamu.
"Tunaomba ushirikiano wenu wa kuendeleza harakati katika Msikiti wetu na kuhimiza maendeleo yetu, pia tuwatenge na kuwapiga vita wanafiki ambao wanadiriki kuwapeleka wenzao mahakamani na kuacha muongozo wetu wa Qur'an na Sunnah", alisema.
Uongozi huo mpya umeahidi kufanya kila linalowezekana kukamilisha ujenzi
wa shule ya Msikiti huo ambao umekwama kwa muda mrefu na kufanya jengo
hilo kuwa maficho ya vibaka na wazinifu.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |