Ajali ya maporomoko ya Kunduchi Salasala:
Serikali yalaumiwa kutowajali wananchi

"TUNACHIMBA mawe kwa sababu ya shida. Mimi nina leseni ya udereva Class C lakini nipo hapa kwa sababu kazi hakuna na serikali haitusaidii", Bwana Mohamed Saleh aliyatamka hayo mbele ya maiti za wenziwe waliopondwa na kufa papo hapo.

Kituo kimoja cha Televisheni kilionesha tukio hilo la kusikitisha juzi ambapo maiti za vijana wawili, mtu na nduguye zilionekana zikiwa zimepasuka vichwa na ubongo kumwagika huku ngema ya dongo bichi likiendelea kuwanyemelea.

Akiongelea hatari inayowakabili wachimbaji wa mawe hayo kijana mwingine ambaye hakujitambulisha jina lake alisema ni hali ngumu ya maisha inayowalazimisha kuendelea na shughuli hiyo.

"Wameshakufa wenzetu wanane hadi sasa mbali ya hawa wawili, lakini tufanyeje, ndio tunajisaidia sisi na familia zetu", alisema kwa uchungu kijana huyo.

Lilikuwa tukio la kutisha ambalo wananchi wa eneo hilo hawakusita kuonesha hisia zao kwa kila waliye mdhania kuwa angefikisha kunakohusika.

"Kila siku viongozi wanaropoka tu watu wafanye kazi wao wenyewe hatuoni wanafanya kazi gani wanashindwa hata kuweka vijiko kuwasaidia vijana hawa wayapate kwa urahisi mawe wanayoyagonga, amelalamika Bwana mmoja mkazi wa Kunduchi.

"Mimi nilikuwa nauza mitumba Magomeni baada ya kuvunjiwa kibanda changu niko huku nagonga mawe, tuko hatarini, hasa wakati huu wa mvua, lakini tufanyeje viongozi wanachojua ni kutuvunjia vibanda tutakwenda wapi hiyo siyo kazi yao, kijana Ali amelidokeza gazeti hili.

Baadhi ya wananchi walisikika wakinung'unikia mfumo wa utawala ambao wamedai umewafikisha watu kubahatisha maisha kama inavyoendelea eneo hilo.

Wamesema, watawala na familia zao wanaishi maisha ya fahari bila ya kujali hali za wananchi ambao wengi wao hushindwa hata kujipatia mlo wa siku.

"Tumewachagua ili waboreshe maisha yetu lakini wametusaliti, kazi yao kutuhutubia na kusafiri, wanakula vizuri wao sisi tunateseka namna hii, amesikitika Bwana Sadiki mkazi wa Kunduchi jirani na shule ya Kiislamu.

Ajali ya Kunduchi Salasala ilitokea wakati viongozi wote wa nchi wakiwa katika sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika Uwanja wa Taifa Jijini.



Watishia kung'oa kahawa, wapande maharage

BAADHI ya wakulima wa kahawa Morogoro vijijini wametishia kung'oa zao hilo la biashara na kupanda maharage endapo tatizo sugu la masoko na bei hafifu ya mauzo halitatatuliwa na mamlaka husika.

Wakiongea na gazeti hili mjini hapa mapema wiki hii walisema kuwa, licha ya ukosefu wa soko la kuaminika, inapotokea wanunuzi wa zao hilo ambao aghalabu ni watu binafsi basi wao hunyimwa haki ya kupanga bei, kinyume chake mnunuzi huwa na kauli ya mwisho.

Wakaongeza kwamba, endapo hali hiyo isiyoridhisha itaendelea basi wao hawatakuwa na njia nyingine ila kufyeka mibuni na kupanda mazao mengine yenye soko la kuaminika hususan maharage.

"Haiwezekani kilo moja ya kahawa iwe sawa na kilo moja ya maharage kwa bei ya shilingi 400. Bora kufyeka tu hii mibuni na kupanda maharage ambayo yanauzika kwa wepesi zaidi", alisema mmoja wa wakulima hao Bw. Josephat Mdangu mzaliwa wa Nyiachiro.

AN-NUUR ilipokwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro Vijijini, Bw. John Gile kufuatia tishio hilo, akaahidi kuwa atazungumza na watu wake wa kilimo na ushirika, pamoja na wanunuzi binafsi kulitafutia ufumbuzi wa haraka na wa kudumu tatizo hilo sugu.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umegundua kuwa wilaya hiyo ina 'programu' ya kilimo ambayo ina lengo la kuinua kilimo vijijini. Hata hivyo, programu hiyo ingali makabatini, haikuweza kufahamika mara moja lini hasa itaingizwa vitendoni.


Mkuu wa Wilaya aamuru waumini wahame Msikiti

SERIKALI imewataka waumini wawili wa Msikiti wa Bilali Tabata wahame kufuatia kutokuelewana kati yao na Bakwata.

Katika barua yenye Kumb. Na. R.10/1vol/87 ya tarehe 5, Aprili, 2000 iliyoandikwa na Katibu tawala na kusainiwa kwa niaba yake na Bwana A.P. Marandu, serikali imewaamuru waumini hao wahame mara moja Msikiti huo.

"Kwa barua hii Mkuu wa Wilaya anawataka mhame kutoka kwenye majengo ya Msikiti huo, imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Kwa mujibu wa barua hiyo, waumini waliofukuzwa ni mabwana Said O. Chambuso na Ahmad Fadhili ambao wote ni waalimu wa madrasa inayoendeshwa katika majengo ya Msikiti huo.

Amri ya serikali imekuja baada ya majaribio kadhaa ya viongozi wa Bakwata kutaka kuwafukuza waalimu hao.

Jaribio la mwanzo lilikuwa mnamo Julai 17, 1998 ambapo Bwana M.R. Kavunga, Mwenyekiti wa Kamati ya Bakwata katika Msikiti huo alipomwandikia barua Bwana Ahmad Fadhili kumtaka ahame katika majengo ya Msikiti na arudishe vyombo vya Msikiti.

Barua hiyo ambayo nakala zake zilipelekwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala na sehemu nyingine za serikali ilimtaka Mwalimu huyo aondoke Msikitini hapo kufikia Agosti 1, mwaka huo.

Hata hivyo, waumini hawakuafiki amri na waliitisha kikao mnamo Agosti 8, 1998 kisha kumuandikia barua Mkuu wa Wilaya ya Ilala kuhoji hatua ya ofisi yake ikishirikiana na Polisi Buguruni dhidi ya Mwalimu Ahmad na waumini wa Msikiti wa Bilali.

Waumini hao walipinga hatua ya Mwenyekiti huyo wakidai haikuwa halali na kinyume na taratibu za uongozi wa Msikiti huo.

Nyaraka mbalimbali za Msikiti huo zinaonesha kuwepo kwa malumbano ya muda mrefu baina ya waumini na uongozi wa Bakwata.

Aidha, kumekuwepo na vikao vya usuluhishi ambavyo baadhi vilishauri ufanyike uchaguzi kuweka uongozi mpya.

Hata hivyo, Bakwata kwa upande wake iliendelea kushikilia msimamo wa kutowataka vijana wa Msikiti huo.

Msimamo huo iliuonesha katika barua yake ya Septemba 1998 kwenda kwa Katibu tawala.

Gazeti hili lilipomuhoji muhusika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuhusiana na suala hilo, alisema uamuzi wa Mkuu wa Wilaya kuwafukuza walimu hao ulitokana na maelekezo ya Bakwata Wilaya.

Alisema, sababu kubwa ya vijana hao kutakiwa waondoke ilikuwa ni kupinga kwao serikali ya CCM hadharani na kwamba walikuwa wanaingiza walichodaiwa kuwa ni imani ngeni.

Hata hivyo, muhusika huyo ambaye ni Mkristo hakuweza kufafanua ni aina gani hiyo ya imani wanayoingiza vijana hao Msikitini hapo.

Alipohojiwa kuhusu serikali kujiingiza katika mambo ya dini, alisema, ilifanya hivyo kwa kuwa Bakwata hawana polisi kuwalazimisha vijana hao waondoke.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook