Uchaguzi Oktoba baadhi ya wananchi wasema:
CCM isichume isichopanda
Imeambiwa kuwepo kwa amani, utulivu na kukosekana chuki za kikabila, si zao la juhudi za mwanasiasa yoyote au Chama.

Wakijadili hali ya uchaguzi mkuu mwaka huu, baadhi ya wananchi waliokuwa wakielekea Moshi wamesema, propaganda ya amani, utulivu na kuondoa ukabila imechuja.

"TAA ilijaa watu wa makabila tofauti; Nyerere Mzanaki alipokelewa na Wazaramo. Huo ukabila uliondolewa na Nyerere na CCM ni upi".

Alisema abiria mmoja na kuongeza, "wasitake kuchuma wasikolima wala kupanda. Watueleze ileahadi yao ya kuondoa umaskini, ujinga na maradhi imefikia wapi".

Abiria hao walikuwa wakitazama hoja inazoweza kuibuka nazo CCM wakati wa kampeni za uchaguzi.

Walisema, amani na utulivu na kutokuwepo kwa uhasama wa kikabila, haikuwa miongoni mwa matarajio ya wananchi kwani hayo hayajawahi kuwa tatizo.

"Ipo historia ya vita vya majimaji, na mashujaa kama Mkwawa, Mirambo na Abushiri. Ni historia ya mapambano dhidi ya wakoloni. Haipo historia ya mapambano kati ya makabila kwa ajili ya chuki", alisema abiria mmoja.

"CCM ikidai imeondoa ukabila, ikaleta umoja na amani, ieleze wapi nchini kulikuwa na mapambano kama yale ya Wahutu na Watutsi, halafu ikafanya juhudi kuleta hiyo amani", alidakia abiria mwingine.

Katika mjadala huo, ilielezwa kuwa mkoloni aliikuta amani, TAA na TANU vikairithi na kuikabidhi kwa CCM.

"TANU na serikari huru ya Tanganyika haikuona amani, utulivu na umoja ni tatizo la nchi hii. Ndio maana hazikuwa agenda zao", alisema mzee mmoja aliyedai kuwa mmoja wa veterani wa TANU.

"Walisema maadui wetu ni ujinga, umaskini na maradhi, sasa waeleze wametumiaje raslimali na kodi zetu kupambana na maadui hao", alisema.

Mwandishi wa habari hizi aliyekuwa miongoni mwa abiria katika basi la Dar Express, Aprili 22, mwaka huu, alishuhudia watetezi wa CCM wakishikilia hoja kuwa CCM imeleta amani. Hata hivyo, hawakuweza kueleza lini nchi hii ilikosa amani na CCM kama chama kikaingilia kati.

"Wananchi ndio wanaoendeleza utapeli katika siasa. Mtu akisema kaleta amani, hatuulizi lini haikuwepo; bali anapigiwa makofi. Akidai kaondoa ukabila anapigiwa vigelegele, haulizwi, lini ukabila ulikuwa tatizo. Wala haulizwi toka ameshika madaraka kauza dhahabu na almasi kaisi gani, utalii umeingiza kiasi gani na kakusanya kodi kiasi gani. Na mapato hayo kayatumiaje", alisema mama mmoja.

Wakati basi linakaribia kuingia Moshi mjini, mzee mmoja alisema kuwa ingefaa vyama vya upinzani na taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) ziwaelimishe wananchi wazijue hizi propaganda hewa. Akadai iwapo wananchi watakuwa wanahoji vipi umaskini wao, vipi huduma za afya, maji, barabara, ajira na elimu bora ya watoto wao, wapi zinakwenda kodi zao, utapeli katika siasa ungekoma.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook