Waislamu wapinga wasimamizi wa uchaguzi
SIKU chache baada ya Amir wa Shura ya Maimamu, Sheikh Juma Mbukuzi kuwataka Waislamu wapinge uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi kwa kuwa haukuzingatia uwiano wa kidini, waumini wa Misikiti mbalimbali jijini wameungana na kiongozi huyo kushutumu uteuzi huo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, waumini wa Msikiti wa Ubungo Darajani wamesema, hawaafiki uteuzi huo na wameonesha shaka kuwa huenda ni mpango wa siri unaotekeleza agenda ya Kanisa.

Wamehoji mantiki ya kauli ya Rais kuwa serikali itahakikisha uchaguzi unakuwa wa haki ilhali wasimamizi wote ni watu wa dini moja.

"Haki gani anayodai Rais wakati wasimamizi wote wa uchaguzi ni Wakristo, Muislamu atapata wapi haki", amedai Bwana Jumbe, muumini wa Msikiti huo anayeishi Ubungo Kibangu.

Ustaadh Suleiman wa Msikiti wa Tungi amedai uteuzi huo unaelekea kuthibitisha mpango wa Kanisa ulioripotiwa na gazeti moja la dini ya Kikristo.

Gazeti hilo liliandika kuwa, Kanisa limekusudia uchaguzi wa mwaka huu viongozi wote watakaoongoza serikali watoke Kanisani.

Bwana Masoud wa Kiblatain, Kariakoo ametilia shaka mwenendo wa serikali ambao amesema, unatishia kuwagawa Watanzania kwa misingi ya dini.

Amesisitiza Waislamu hawakubaliani na mwenendo huo ambao amedai imejitokeza mara zote serikali kuwa upande wa Kanisa.

"Watu wanaoangalia usalama wa nchi hii hizi ndizo aula (priorities) za kuangalia kabla kuliko kuja kushughulikia matokeo",amedai muumini huyo ambaye ni mkazi wa Kinondoni.

Wiki mbili zilizopita, serikali ilitangaza kupitia vyombo vya habari orodha ya wasimamizi wa uchaguzi mkuu ujao.

Katika orodha zote mbili imejitokeza Wakristo kuwa zaidi ya asilimia 90 kiuwiano kulinganisha na waumini wa dini nyingine.

Hata hivyo, tangu Waislamu waanze kulalamikia udini huo, serikali haijasema lolote, badala yake imeendelea kusingizia vyama vya upinzani kuwa vinatumia Misikiti kueneza sera zao.


Rais hashauriwi vizuri?

NIMEIPENDA mno makala ya kitaalamu juu ya kiini macho cha msamaha wa madeni iliyochapishwa katika gazeti hili toleo lililopita.

Kwa hakika makala hiyo imeandikwa kitaalamu kwa maslahi ya nchi yetu. Mtaalamu ametuweka darasani kutuelimisha juu ya mwenendo wa kidhalimu wa mashirika ya fedha ya kimataifa ambayo yanaangamiza mataifa madogo kiuchumi.

Nimefarijika sana na ushauri wa mtaalamu alioutoa kwa serikali kuwa iwe inawaambia ukweli wananchi kuhusu mashirika hayo badala ya kuwapa matumaini hewa kwa kuegemea misamaha ambayo tangu hapo serikali haikuwa na uwezo wa kuyalipa.

Nimesikitishwa na namna serikali yetu ilivyopokea na kulionea fahari suala la kusamehewa madeni kana kwamba fedha zenyewe za kulipa hayo madeni yenyewe tunazo.

Jumapili iliyopita nilimsikia Profesa Lipumba katika mjadala juu ya IMF na Benki ya Dunia ulioendeshwa na Sauti ya Ujerumani.

Profesa Lipumba alisema kuwa madeni yenyewe tuliyosamehewa hatukuwa na uwezo wa kuyalipa kwa sababu hakuna pesa ya kulipia benki na kuna matatizo katika upatikanaji, ukusanyaji na utumiaji wa pesa zenyewe kwa sababu ya kutokuwepo kwa sera nzuri za kutekeleza mambo hayo.

Kwa mantiki ya maneno hayo ya Prof. Lipumba, naona basi hakukuwa na sababu yoyote kwa Rais kulihutubia Taifa kuhusu suala hilo na kuwapa wananchi tamaa ambayo hawatakidhiwa. Ingekuwa bora zaidi kama jambo hilo lingejadiliwa tu kwenye gazeti la serikali kwa ajili ya kumbukumbu.

Tangu hapo si busara kwa muungwana kujigamba kusamehewa kulipa deni ambalo limekushinda kulipa. Pia si vizuri kuyapa sifa ya utu mashirika ya fedha ambayo yanatukandamiza kiasi kwamba wenzetu wa nchi nyingine kama vile Cuba (Rais Castro) wamefikia hatua ya kudai mashirika hayo yavunjiliwe mbali kwa kuwa yanazinyonya nchi masikini.

Huenda serikali yetu imelipokea na kulizungumza suala la msamaha wa madeni kisiasa zaidi kuliko kiuchumi. Ndio maana katika hotuba ya Rais alitoa shutuma dhidi ya vyama vya siasa vya upinzani na ndio maana pia RTD ikadakia kwa kulitungia hadithi suala hilo la "msamaha" katika kipindi chake cha "Maneno hayo".

Kwa hisia zangu na bila shaka za wengi, kauli za wataalamu wetu wa masuala ya uchumi dhidi ya kiini macho cha masuala ya misamaha ya madeni zinaibua maswali mengi juu ya umakini wa serikali yao.

Masuala ambayo mtu yeyote makini anaweza kuuliza ni je serikali yetu haina washauri mahiri wa masuala ya kiuchumi? Au washauri wapo ila wanampotosha Rais Wetu? Au Rais hazingatii ushauri wa wataalamu waliomzunguka? Au serikali inatolewa "kafara" kwa maslahi ya chama chake mwezi Oktoba?

Majibu ya maswali yote haya yatatushawishi kuamini kuwa tunahitaji mabadiliko ya serikali kupitia chama na chama hicho kitupatie Rais mtaalamu ambaye atang'amua hujuma za mashirika ya fedha ya kimataifa. Rais ambaye hataona kivuno ganda la muwa la jana!
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook