WAISLAMU mjini hapa wameandaa Dua kuwarehemu Masheikh na wazee wa kiislamu wa mkoa huu.
Dua hiyo imepangwa kufanyika mei 13, mwaka huu katika msikiti wa mafiga.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi Ustaadh Ramadhan Said, lengo la Dua hiyo ni kuthamini mchango mkubwa walioutoa wakongwe hao katika kuupeleka mbele Uislamu mkoani hapa.
Mwenyekiti huyo amesema katika Dua hiyo utatolewa wasifu wa baadhi ya Masheikh na wazee hao maarufu.
Amewataja baadhi ya Masheikh hao kuwa ni pamojana Sheikh Maulid bin Diwani, Sheikh Juma Kawambwa na Sheikh Ahmad Bin Juma.
Wengine ni Sheikh Athman Hassan Nzige, Sheikh Fadhil Ijihadi, Sheikh Ramadhan Khatibu, Sheikh Hassan Abubakar na Sheikh Ramadhan Haji.
Baadhi ya wazee waliotajwa kuwemo katika orodha ya watakaombewa Dua ni Mzee Salum Mlapakoro, Mzee Ali Mlapakoro, Mzee Mbegu na Mzee Abdallah Yazid.
Wengine ni pamoja na Mzee Hussein Burhan, Mzee Gwebe Mwinyimvua, Mzee Alawi Athman na aliyekuwa mpishi maarufu wa pilau mjini hapa Mzee Salum Khalfan.
Orodha kamili ya wakongwe wote wa mji huu inatazamiwa kutolewa siku ya shughuli hiyo ya kihistoria mjini hapa.
Mawaidha na nasaha mbali mbali zitatolewa kabla ya Dua rasmi kwa Marehemu
hao.
WANAFUNZI 12 wa kidato cha sita shule ya sekondari ya Dakawa wamejiandikisha kufanya mtihani wa maarifa ya Kiislamu mapema mwezi ujao.
Hayo yameelezwa wiki iliyopita na wanafunzi hao katika risala yao kwa mgeni rasmi muakilshi wa Islamic Foundation, Seleman Ally Seleman wakati wa mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa Kiislamu wanaomaliza kidato cha sita shuleni hapo.
Wamesema, mafanikio hayo ni ya kwanza kupatikana tangu shule hiyo ifunguliwe zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Aidha, wanafunzi hao wameeleza matatizo kadhaa yanayowakabili ikiwa ni pamoja na Msikiti mdogo usiotosheleza uwingi wao na wanakijiji wanaojitokeza kuswali hapo shuleni kufuatia eneo lote la Dakawa kukosa Msikiti.
Matatizo mengine waliyoeleza katika risala ni ukosefu wa mazulia ya kuswalia.
Naye mgeni rasmi katika mahafali hayo, Ustadh Seleman Ally Seleman alisema kuwa taasisi yake itajitahidi kujenga Msikiti pamoja na kutoa vitabu vya dini.
Awali, Ustadh Mbaraka Abdallah alitoa mada hali ya Waislamu hivi l eo nchini Tanzania ambapo alieleza kuwa kuna matatizo kadhaa yanayoukwaza.
Aliyataja matatizo hayo kuwa ni uhuru wa kuabudu, mfumo wa kibaguzi katika sekta zote nchini na hali mbaya ya kiuchumi inayowakabili Waislamu.
Shule ya sekondari Dakawa ipo tarafa ya Mvomero, wilaya ya Morogoro
vijijini.
SHEREHE ya kujipongeza ilifanyika wiki iliyopita Thaqafa sekondari.
Pongezi hizo zinafuatia shule hiyo kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne.
Mwaka 1999 shule hiyo ilishika nafasi ya 56 kitaifa.
Awali, 1997 shule hiyo ilikuwa ya 95 kisha ya 135 mwaka 1998.
Katika sherehe hizo, zawadi mbalimbali zilitolewa kwa waalimu na wanafunzi.
Wiki moja kabla ya sherehe hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Steven Mashishanga aliitembelea shule hiyo na kutoa pongezi zake.
Katika ziara hiyo iliyokuwa ya ghafla, Bw. Mashishanga alitoa msaada wa mifuko 50 ya saruji.
Aidha, alimzawadia shilingi 10,000 mwanafunzi Lailati Mawanda aliyemsomea shairi kwa lugha ya Kiingereza.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |