S. Ameir, Zanzibar
KATIKA maelezo ya habari iliyotolewa hivi karibuni katika Sauti ya Zanzibar, mtayarishaji amekuwa akilaumu tabia ya ombaomba inayoenea kwa nguvu sana katika Zanzibar.
Mtayarishaji anawalaumu hawa ombaomba kwamba ni watu wenye nguvu na afya zao lakini wanaacha kuzitumia kufanya kazi na badala yake wanafanya ujanja ili kujipatia fedha za bure.
Kwa hakika kuomba ni kitendo cha udhaifu na kinachoaibisha siyo kwa mwombaji tu bali jamii nzima kwa jumla. Ni kutokana na hali hiyo ndipo Mtume Muhammad (s.a.w.) akatusisitiza kufanya kazi na akapata kusema kuwa mtu kile chakula bora zaidi anakula alichokipata kwa jasho lake mwenyewe, naye akaonya sana tabia ya ombaomba.
Pamoja na hayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesisitiza sana wajibu wa kuwasaidia wenye shida ni sawa wawe waombao au wenye kujizuia kuomba.
Binafsi nahuzunika sana nikiwaona watu wameenea mitaani wakisubiri wapitao kuwaomba, lakini kabla ya kuwalaumu hawa, hebu tujiulize mbona mambo haya yameanza leo? Mbona hatukuyashuhudia haya miaka ya nyuma? Ni nini kilichopelekea kuzuka haya leo? Jamii iliyo nzuri pamoja na serikali yake yanapotokea haya inabidi ijiulize, kulikoni? Bila shaka kila upande lazima ujiangalie, serikali ijiangalie na jamii nayo ijiangalie.
Kwa upande wa jamii ni lazima tukubali kuwa moyo wa kukinai uliokuwepo miongoni mwa wanajamii umepotea na ndipo tukafikia kiwango hiki cha watu kujitoa hadharani bila ya haya kuomba.
Mtume Muhammad (s.a.w.) alituusia kuwa kukinai ni utajiri tosha, ni kweli kabisa kuwa kama umekinai kila mtu atakuhisi wewe ni tajiri hata kama hutimizi mlo wako wa siku moja.
Zaidi ya hapo, inatia uchungu na kuhuzunisha kuwa jamii yenye Waislamu wasiopungua asilimia 95 haina hata jumuiya wala taasisi inayoshughulika na kukusanya na kugawa zaka katika jamii. Ikumbukwe kuwa zaka ni nguzo muhimu ya kuondosha umaskini katika jamii na hili lisitegemewe na serikali kulifanikisha, ni Waislamu wenyewe wa kulitekeleza.
Kwa upande mwingine, serikali yetu ina mchango mkubwa kwa kuzuka ombaomba. Serikali ijielewe kuwa ina wajibu wa kuwajengea wananchi wake msingi wa maisha bora. Binafsi nahisi serikali haiwajali sana wananchi wake, iko tayari raia wake wapate dhiki ilimradi inafanya inalotaka.
Hivi tujiulize kulikuwa na haki gani ya kuwaondoa vijana wa jua kali pale Darajani. Vijana wale waliamua kwa makusudi kutumia jasho lao na uwezo wao mdogo wa kifedha kujifungulia biashara japo ndogo ili kujiendeleza na familia zao.
Kufanya hivyo ni sababu ya wao kuepuka kuwa wezi pia kuepuka kuwa ombaomba. Lakini serikali bila ya kujali matokeo yake ilizuka na jazba ya kuwaondoa bila ya kuwatafutia mahala pengine pazuri kufanyia shughuli zao.
Hebu tujiulize, vijana wale wanafanya nini leo? Je, utawalaumu wakiangukia kwenye wizi au ombaomba? Si hayo tu, bali lau kama si uamuzi wa mahakama hivi sasa tungekuwa na kundi jingine la vijana wa makontena ya Darajani nao wakiranda mitaani bila ya kazi ya kufanya. Serikali ilishaamua kuyaondoa makontena yale! Wale nao wangefanya nini?
Mara nyingi imetokezea askari polisi na mgambo kuwavamia akina mama Lishe (mama ntilie) wa pale Darajani ambao wanawasaidia vijana na wazee wa kipato kidogo pakujipatia chakula chao na wao kujipatia riziki za kula na familia zao. Askari hao wanawavamia na kuwanyang'anya vyakula vyao na vyombo vyao na bila ya kuwaambia wapi wakauzie biashara yao hiyo. Je, katika hali hii utamlaumu mama huyu akivaa baibui lake akakaa kitako Darajani kuomba?
Akinasisi tunaotayarisha maelezo baada ya habari huwa tunashangilia serikali inapoyafanya haya. Hatuwezi hata kunyanyua midomo yetu kuishauri serikali iwafanyie nini watu wale. Sisi tumefundishwa kuipongeza na kuisifu serikali kwa lolote itakalofanya na kuwaponda na kuwalaumu wananchi kwa lolote watakalofanyiwa.
Je, kwenye uwanja wa masuala tutajibu vipi tutakapoulizwa namna tulivyowatetea
wale wenye haki kupata haki zao?
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |