Gari
Kwa jina lake Muumba, Mwenyezi Mungu mmoja,
Ambaye ameviumba, mwili na roho pamoja,
Leo tungo naipamba, inahusu gari moja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Kuna gari la mtumba, limezidisha vioja,
Laendeshwa kwa kuyumba, kweli mwisho wake waja,
Mijini na kule shamba, kwepeni gari likija,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Gari hili linatamba, mbio mbio linakuja,
Ubavuni lina namba, mwishoni nitaitaja,
Kwa rangi wamelipamba, ziko mbili kwa pamoja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Gari moto linapamba, latafuta wateja,
Kila kituo latamba, abiria kuwangoja,
Heri likabebe pamba, tumechoshwa na viroja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Dereva katoka shamba, gari kaja kulifuja,
?Konda? wake ombaomba, anatafuta natija,
Wapiga debe ni ?pumba?, wapo fedha kuzingoja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Wakianza kujigamba, kila jema hulitaja,
Nyimbo nyingi wataimba, ili wakidhiwe haja,
Nendeni nao sambamba, hadi waishiwe hoja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Gari hilo la kishamba, roho za watu lafuja,
Kama sumu ni ya mamba, yaua kila mmoja,
Heri nguo ya mtumba, yaweza pata mteja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Anzeni shimo kuchimba, mlitupe kwa pamoja,
Mlikokote kwa kamba, mlizike mara moja,
Gari lisishike namba, ili tupate faraja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Wananchi kila nyumba, kwepeni gari likija,
Msije kuwa manamba, mkajuta siku moja,
Wenzenu wanajigamba, waliita NAMBA MOJA,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Mohammed Amir,
Morogoro.
CCM ina wenyewe
Fumbo tena si fumbo, si siri bali dhahiri,
Kikao wenye matumbo, kiliketi Zanzibari,
Kwenye mambo na vijambo, kutangaza ubepari,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Ukitaka Uraisi, karatasi milioni,
Wa kwanza huo ukwasi, pesa zisizo na deni,
Kwa fukara si rahisi, japo uwe na tamani,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Na kisomo siyo shani, uchao wanabadili,
Bado kwenye kampeni, na mchujo wa batili,
Siasa za mumiani, wengine kuwa dhalili,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Ubunge ni laki moja, fomu sasa biashara,
Ni chama chenye vioja, sasa hivi ni mnyura,
Kizee chajikongoja, kimepoteza taswira,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Ni ?ruba? sasa si chama, kimeacha maadili,
Pesa ndio zinasema, imetoweka asili,
Mfumo huu dhuluma, mimi nisingekubali,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Ningekulikuwa Mjumbe, kamwe nisingeafiki,
Chama kimekuwa wembe, kwa mnyonge akishiki,
Unyanyaso kwa viumbe, bila pesa hauvuki,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Japokuwa Udiwani, ulipe elfu kumi,
Wenye kipato cha chini, umeshakuwa unyimi,
Wewe uwekwe pembeni, ijapo uwe msomi,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Milango kwa upinzani, ndio kuliko bakia,
Tuibadili ramani, kikongwe kumfukia,
Tena hatumtamani, sasa kibaki mkia,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Khamis Lali Pashua,
Kijiji cha Mavumbi Pande,
S.L.P. 5332,
Tanga.
Rafiki utanipata - jibu
Fumbo tena si fumbo, si siri bali dhahiri,
Kikao wenye matumbo, kiliketi Zanzibari,
Kwenye mambo na vijambo, kutangaza ubepari,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Ukitaka Uraisi, karatasi milioni,
Wa kwanza huo ukwasi, pesa zisizo na deni,
Kwa fukara si rahisi, japo uwe na tamani,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Na kisomo siyo shani, uchao wanabadili,
Bado kwenye kampeni, na mchujo wa batili,
Siasa za mumiani, wengine kuwa dhalili,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Ubunge ni laki moja, fomu sasa biashara,
Ni chama chenye vioja, sasa hivi ni mnyura,
Kizee chajikongoja, kimepoteza taswira,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Ni ?ruba? sasa si chama, kimeacha maadili,
Pesa ndio zinasema, imetoweka asili,
Mfumo huu dhuluma, mimi nisingekubali,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Ningekulikuwa Mjumbe, kamwe nisingeafiki,
Chama kimekuwa wembe, kwa mnyonge akishiki,
Unyanyaso kwa viumbe, bila pesa hauvuki,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Japokuwa Udiwani, ulipe elfu kumi,
Wenye kipato cha chini, umeshakuwa unyimi,
Wewe uwekwe pembeni, ijapo uwe msomi,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Milango kwa upinzani, ndio kuliko bakia,
Tuibadili ramani, kikongwe kumfukia,
Tena hatumtamani, sasa kibaki mkia,
CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.
Khamis Lali Pashua,
Kijiji cha Mavumbi Pande,
S.L.P. 5332,
Tanga.
Bismillahiri naanza, Bunga jibu kupokea,
Ulosema nitaweza, kuwa rafiki murua,
Sheria sitoipaza, karibu nakuletea,
Rafiki utanipata, tukiwa tukipatana.
Nayapenda mapatano, Mwinjilisti sikia,
Unataka muungano, furaha imeningia,
Hutaki mfarakano, urafiki wapendea,
Rafiki utanipata, tukiwa tukipatana.
Sharti uwe Silamu, wavitendo ndugu jua,
Kwa wanazuo silimu, niliopo kuingia,
Shahada taja Karimu, na Muhammadi Nabia,
Hapo nitakukubali, kuwa rafiki hakika.
Kwani utawakaribu, rahisi kukupokea,
Ukikijua kitabu, nami nina furahia,
Ni Kur-ani mujibu, yakupasa kuijua,
Hapo nitakukubali, kuwa rafiki hakika.
Rafiki wa kuachana, muda wa swala kuingia,
Furaha kwangu hakuna, pa mwena kwake Jalia,
Yapasa tunashikana, Masjidi kuingia,
Furaha isokifani, kwa urafiki mwanana.
Muda wa swala kufika, ibadani twarejea,
Siyo pekee kufika, wawili wote twangia,
Nia njema kwa Rabuka, yapasa kutilia,
Hapo nitakukubali, kuwa rafiki hakika.
Isomwapo Qur'ani, isikilize kwa hushua,
Kitabu hicho cha dini, cha kufaa kukijua,
Sikitie mashakani, usije kuangamia,
Hapo nitakukubali, kuwa rafiki hakika.
Kama hutaki Qu'ani, nami tumewajalia,
Nami pia mashakani, yapasa kukwepukia,
Isilamu muumini, ndiye nitamteua,
Rafiki utanipata, tukiwa tukipatana.
Nawahi Msikitini, jibu nadhifu pokea,
Unijibie safuni, kama wanikubalia,
Uwe ndugu wa jirani, wazo langu fikiria,
Rafiki utanipata, tukiwa tukipatana.
Fundi Omar Idrssa,
S.L.P. 19,
Pangani,
Tanga.
'Ujinga kulinda haki'
Kamwe haiwezekani, bila dhuluma kuwepo,
Hapa pana mtihani, batili ndipo ilipo,
Ujinga ni ugizani, siyo jambo la matapo,
Ujinga kulinda haki, lazima ipo dhuluma.
Nchi yajivunia vipi, iliyotanda ujinga,
Kama mtoto kwa pipi, akawa jama aringa,
Watetezi mko wapi, haki inapigwa chenga,
Ujinga kulinda haki, lazima ipo dhuluma.
Mtu bila ya elimu, haki hapa itapinda,
Lazima pawe na sumu, ujuwe ipapo inda,
Dhuluma uona tamu, unena wameshinda,
Ujinga kulinda haki, lazima ipo dhuluma.
Haki kuwepo vigumu, ujinga palo shamiri,
Wengine umwaga damu, jambo hilo siyo siri,
Ujinga huwa awamu, utokea ujasiri,
Ujinga kulinda haki, lazima ipo dhuluma.
Wajanja tahadharini, mlo kubuu dhuluma,
Watu kama hayawani, katu hamtendi wema,
Mjue ya Mungu shani, pale itaposimama,
Ujinga kulinda haki, lazima ipo dhuluma.
Hivi mwafanya dhuluma, kipi mnachofikiri,
Mwadhani watu ni duma, ama kuku wa kideri,
Mnazidisha hujuma, tena ambazo dhahiri,
Ujinga kulinda haki, lazima ipo dhuluma.
Beti saba nashiliza, ujinga una kikomo,
Linapotoweka giza, nuru huwa ni mfumo,
Fanyeni ya kupendeza, ndio uwe msimamo,
Ujinga kulinda haki, lazima ipo dhuluma.
Khamis Lali Pashua,
Kijiji cha Mavumbi Pande,
S.L.P. 5332,
Tanga.
Haki sawa
Haki ni yake Jalali, jinale kulianzia,
Haki ya pili Rasuli, sawala tunamsawalia,
Haki kitu cha awali, wajibu kinafatia,
Haki sawa siku zote, amani itabakia.
Haki tukiiheshimu, amani itaenea,
Haki tukiidhulumu, tutaja kujijutia,
Haki ni kitu adhimu, kuibeza ni balaa,
Haki sawa siku zote, amani itabakia.
Haki tuitekeleze, chaguzi zikiwadia,
Haki tusiikawize, viongozi kuchagua,
Haki zetu waeleze, watakavyozitetea,
Haki sawa siku zote, amani itabakia.
Haki zao viongozi, na zetu kama raia,
Haki hata ?wachochezi, lazima kuwapatia,
Haki huwa mchokozi, asiye izingatia,
Haki sawa siku zote, amani itabakia.
Haki huwa mtihani, viongozi haramia,
Haki hawaithamini, wabaki wajichekea,
Haki aitoe nani, pasipo ipigania,
Haki sawa siku zote, amani itabakia.
Haki ya Maaskofu, na ya Masheikh sawia,
Haki si ya maarufu, na wengine kupuzia,
Haki za watu dhaifu, lazima kuwapatia,
Haki sawa siku zote, amani itabakia.
Haki sawa kaditama, hapa ninamalizia,
Haki isiposimama, tutaja ipigania,
Haki si mali ya chama, bali ya raia pia,
Haki sawa siku zote, amani itabakia.
Ramadhani Amri L. Nkoroboko,
Dar es Salaam.
Siasa na dini
Rabuka kanijalia, kurudi tena dimbani,
Nipate kusimulia, yasemwayo jukwaani,
Ninyi mtahadithia, sokoni na kahawani,
Siasa pia na dini, kitu kimoja kamili.
Waliokosa elimu, bado wangali gizani,
Wamepoteza fahamu, hawajui ya zamani,
Vitabu vitukufu, walonena makuhani,
Siasa pia na dini, kitu kimoja kamili.
Siasa ni mapatano, ili amani idumu,
Hushikamana mikono, wakafanya ukarimu,
Wakapanua midomo, cheko kukosa fahamu,
Siasa pia na dini, kitu kimoja kamili.
Dini ndiyo njia yetu, kwake Mola kumwendea,
Alokosa watu, taenda kichekelea,
Bila ogopa watu, ya Mola kushikilia,
Siasa pia na dini, kitu kimoja kamili.
Daudi kawa Raisi, kisiasa kutawala,
Huku akiwa Nabii, akihubiri ya Mola,
Kafuta kodi fakiri, apate radhi ya Mola,
Siasa pia na dini, kitu kimoja kamili.
Mfalume Selemani, baba yake ni Daudi,
Kapewa kubwa dhamini, nyuma asirudi rudi,
Awe ndiye mdhamini, uma wake na Daudi,
Siasa pia na dini, kitu kimoja kamili.
Msijifanye wajanja, kuzigeuza sekula,
Kusema hakufa njaa, bali kakosa chakula!
Watu wakisha zubaa, mpate kuiba kura,
Siasa pia na dini, kitu kimoja kamili.
Mwisho Saidi nasema, mwezi wa kumi dimbani,
Asubuhi na mapema, na shahada mkononi,
Hiyo ndiyo hitimisho, mtaingia porini,
Siasa pia na dini, kitu kimoja kamili.
Saidi M. Buweta,
S.L.P. 220010,
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |