Wananchi wasiwe mitungi, wakosoe
UBAGUZI kwa misingi ya ukabila au dini ni tatizo lenye kuiangamiza jamii.
Penye ubaguzi huo, kigezo cha kukubalika mtu si utu, matendo na uwezo wake. Bali kabila au dini yake
Ubaguzi huu ni hatari. Hufanya baadhi ya watu wachukiwe bila ya sababu yoyote.
Wayahudi wapatao milioni sita walioangamizwa na Wanazi, walichukiwa kwa Uyahudi wao.
Waislamu walioangamizwa Bosnia kwa maelfu na wake zao kubakwa, hawakuwa maharamia. Walichukiwa na Waserbia kwa dini yao, Hali ni hiyo hiyo kwa Waislamu waliouliwa Kossovo.
Kilichochochea mauaji ya halaiki Rwanda si ugomvi wa mali wala ardhi. Ni kabila moja kulichukia lingine.
Wananchi wenyewe wanaweza wasiwe na tatizo. Watu wa makabila na dini tofauti wakaishi mitaani pamoja bila ya bugudha. Wakapanga hata nyumba moja na watoto wao wakacheza pamoja.
Lakini ukikuta kwa mfano, katika Wizara fulani wamejaa watu wa kabila moja tu ama dini fulani.
Ukaenda Ikulu, Ofisi ya Waziri Mkuu ukakuta ni watu wa kabila hilo hilo au dini hiyo hiyo.
Huo utakuwa ni ubaguzi katika kiwango cha taasisi.
Ni ubaguzi unaojengwa na viongozi wa serikali japo katika sera haziwaagizi hivyo.
Pengine tujitizame katika mazingira yetu ya Tanzania. Upo ubaguzi wa kikabila au dini katika vijiji na mitaa yetu?
Hali katika serikali na taasisi zake ikoje?
Viongozi wa serikali na vyama vya siasa wamekuwa wakikemea mwelekeo wowote wa kujenga ukabila au udini.
Je, mwelekeo huo upo mitaani au serikalini. Nani wa kumkemea mwenzake, serikali au wananchi?
Ufa usipozibwa kujenga ukuta hapana budi. Na majuto siku zote ni mjukuu. Ambapo pema usipopema si pema tena.
Wananchi wasione wajibu wao ni kupokea
tu nasaha au "kuelimishwa" na kwa viongozi wa serikali. Lakini watizame
pia viongozi wasijeitosa nchi Rwanda.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |