WAKATI UCHAGUZI MKUU UKIWADIA

Maandalizi ya mkutano mkuu wa CCM kesho yapamba moto

UMOJA wa Wanawake wa CCM Taifa jana ulitazamiwa kukutana na makundi mbalimbali ya wanawake mjini Mwanza katika uwanja wa Nyamagana.

Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja huo Bibi Ana Abdallah ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi.

Barua za mkutano huo zilianza kusambazwa mapema wiki hii ambapo makundi ya akina mama zikiwemo madrasa, misikiti na zawiya ziliombwa kuhudhuria mkutano huo ambao ilielezwa lingezungumziwa suala la mikopo kwa ajili ya kuanzishia biashara ndogo ndogo "kuinua kipato" cha akina mama.

Suala la mikopo kwa akinamama limekuwa maarufu kila inapokaribia chaguzi mbalimbali.

Imeelezwa kuwa mikopo hii ya sasa inalenga kufuta umaskini uliojichimbia nchini.

Hata hivyo, wanawake wengi wamekuwa wakihoji hao wanaogawa mikopo hiyohivi sasa walikuwa wapi na kwa nini iwe kwa mtu mmoja mmoja badala ya kujenga au kuweka kitu cha kijamii kitakachonufaisha watu wote wakiwemo wanawake.


Ma'hdy watunukiwa vyeti

WANAFUNZI 41 wa shule ya Ma'hdy wametunukiwa vyeti baada ya kuhitimu elimu yao ya miaka minne.

Vyeti hivyo vilitolewa na Mufti wa Zanzibar, Sheikh Harith bin Hemed bin Khelef ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Shule ya Ma'hdy inashirikiana na taasisi iitwayo Sir Issac Pitman Institute iliyoko London, Uingereza.

Kwa ushirikiano huo hata vyeti vya Ma'hady ni vile vya PITMAN ambapo kila cheti hulipiwa shilingi laki moja.

Ili kuboresha huduma, shule hiyo inatarajiwa kuwa na mabweni hivi karibuni.

Mkurugenzi wa shule hiyo, Ustadh Jabir amesema, huduma hiyo itawasaidia kupata wanafunzi kutoka mikoa ya mbali.

Shule ya Ma'hdy inatoa elimu ya msingi na sekondari na ina wanafunzi 900.

Ustadh Ateeq Rashid aliye Afisa Uhusiano wa Kimataifa wa Masjid Diwil, amesema, juhudi za Ma'hdy ni kutekeleza wito wa Mtume (s.a.w.) wa kutafuta elimu.


Kamata kamata Mwanza yahamia CUF

KAMATAKAMATA iliyoendeshwa na polisi mjini Mwanza dhidi ya Waislamu sasa imeripotiwa kuelekezwa CUF.

Jumanne wiki hii, polisi waliokuwa katika Land Rover mbili walimvamia fundi seremala mmoja anayejulikana kwa jina la Bwana Hassan wakimtuhumu kupandisha bendera ya CUF juu ya mwembe yenye maneno yenye kuhatarisha amani.

Polisi baada ya uvamizi huo, walimpiga mtuhumiwa mithili ya mwizi.

Imedaiwa hatua hizo za polisi zinatokana na maelekezo wanayopokea kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama tawala.

Watu kadhaa wamesikitishwa na uvurugaji wa demokrasia unaofanywa na vyombo vya dola ambao umesababisha hali ya wasiwasi kwa familia nyingi mjini Mwanza.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Hamad aliwasili mjini Mwanza ambapo juzi alizungumza na wanachama wa chama cha CUF na kufungua matawi mapya ya chama hicho.

Katibu huyo wa CUF alitazamiwa kufanya mkutano wa hadhara jana baada ya kukamilisha taratibu.


Afya za wananchi hatarini Dodoma

MITARO ya maji machafu mjini Dodoma imefurika hali inayotishia afya ya wananchi.

Barabara pia zimekuwa katika hali mbaya, kinyume na ilivyotarajiwa kuwa kwa Mji Mkuu.

Mwandishi wa habari hizi aliyetembelea Dodoma hivi karibuni, alishuhudia mitaro kadhaa ikiwa imefurika maji machafu.

Mitaro hiyo ni ile iliyo kando kando ya barabara zenye shughuli nyingi.

Ikiwa inapita mbele ya maduka ya vyakula, mikahawa na makazi ya watu, adha na hatari yake inakuwa kubwa zaidi.

Barabara namba sita, saba, tisa na ile ya mtaa wa Tabora ndizo zilizoonekana mitaro yake kufurika zaidi.

Maji yaliyojaa kwenye mitaro hiyo iliyo wazi ni meusi tii. Mengine yakionekana dhahiri kutokea vyooni.

Wananchi walioongea na mwandishi, wameeleza kuwa hali hiyo imedumu kwa muda mrefu sasa. Hata hivyo hawakusema ni miezi mingapi.

Barabara kadhaa nazo hupitika kwa shida kutokana na kuchimbuliwa na kuachwa bila kusawazishwa.

Barabara ya kumi na moja kuanzia soko kuu hadi Mwembe Tayari haina sura tena ya barabara. Vipande katika baadhi ya barabara nyingine, vimemwagwa kokoto isiyoshindiliwa.

Pamoja na matatizo hayo, zimeelezwa kuwa ukosefu wa maji limekuwa tatizo sugu kwa baadhi ya maeneo.

Maeneo hayo ni Nkuhungu, Hazina, Kigamboni, Milembe Mahole na Chadalu A/B.

Juhudi za gazeti hili kuwapata viongozi wa mamlaka husika kuzungumzia matatizo haya hazikuweza kufanikiwa.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook