CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara nyingine tena kimeshindwa uchaguzi wa marudio wa serikali za mitaa uliofanyika jumapili iliyopita mjini hapa.
Katika uchaguzi huo mgombea wa CUF bwana Madadi Hassan Maringo alimshinda bwana Hassan Ali Mlapakoro na kufanikiwa kunyakuwa tena uenyekiti wa mtaa wa Boma wenye ofisi nyingi za Serikali ikiwemo ya Mkuu wa Mkoa.
Bwana Maringo alipata kura 144 na kumshinda mpinzani wake kwa kura nne ambaye aipata kura 140 katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa kati ya vyama hivyo.
Hoi hoi na vifijo vilitawala mitaa mbali mbali ya mji huu unaoonekana kuwa na wapenzi wengi wa CUF, baada ya bwana Maringo kutangazwa rasmi mshindi katika uchaguzi huo akimuacha Bwana Hassan na wapenzi wake, wengi wa jamii ya kiasia, wakiwa wameduwaa.
Mwandishi alishuhudia vikao vya hapa na pale vilivyokuwa vikifanywa na viongozi wa CCM mara baada ya kutangazwa matokeo hayo.
Matokeo ya awali ya uchaguzi huo yalifutwa kufuatia malalamiko ya CCM dhidi ya dosari ilizodai kujitokeza katika upigaji na kuhesabiwa kwa kura.
Bwana Madadi ndiye aliyeibuka mshindi dhidi
ya mpinzani wake bwana Hassan aliyekuwa mchezaji maarufu wa Klabu ya Simba
miaka ya sabini.
WAISLAMU mjini Musoma wamemlakamikia Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba juu ya hatua ya mahakama mjini humo kuwaamuru waumini wa Kiislamu kuvua kofia kama sharti la kuwawekea wenzao dhamana.
Katika barua yao kwa Waziri huyo, waumini hao wameeleza kusikitishwa kwao na kile walichokiita udhalilishaji wa Waislamu kufuatia amri hiyo.
Barua hiyo imetaja baadhi ya vikao vya mahakama hayo vilivyowaamuru wahusika wavue kofia.
Vikao vilivyotajwa ni pamoja na kile kilichofanyika mwaka 1998 ambapo Hakimu Bwana Mutungi aliwaamuru kuvua kofia Sharifu Abdi, Mzee Tawakal na Mzee Mchumira ili waruhusiwe kuwadhamini vijana wao.
Vikao vingine ni vile vilivyofanyika mwaka wa jana na mwaka huu ambavyo vyote viliwataka wahusika wavue kofia ili waingie mahakamani na wakati wa kuwadhamini vijana wao.
Kwa hali hiyo, Waislamu wamemuomba Waziri wa Sheria atoe ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na amri hiyo.
Nakala za barua hiyo iliyosainiwa na Bwana
Nyamrasa Mbaruku zimepelekwa kwa Jaji Mkuu, Jaji Mfawidhi wa kanda na msajili
wa mahakama ya rufaa kanda ya Mwanza.
MUFTI wa Bakwata, Sheikh Hemed bin Juma bin Hemed yuko ziarani mjini Mwanza ambako imeripotiwa atazungumza na Waislamu juu ya malalamiko yao dhidi ya serikali ya CCM.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinafahamisha kuwa akiwa mjini Mwanza, Mufti Hemed atatembelea Misikiti mbalimbali kuwataka Waislamu watulizane wakati serikali ikishughulikia madai yao.
Kutoka Mwanza, Mufti ataendelea na ziara yake mikoa mingine hadi atakapomaliza mikoa yote kabla ya Maulid ya kitaifa iliyopangwa kufanyika mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi huenda akawa Dk. Omar Juma.
Haikuweza kufahamika mara moja sababu za Mufti kufanya ziara hizo hivi sasa, hata hivyo baadhi ya wakazi wa mjini Mwanza wametuhumu ni katika kampeni za kisiasa ikizingatiwa mwezi Oktoba mwaka huu, Watanzania watapiga kura kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
Wakati huo huo, kesi ya Waislamu walioandaa kongamano eneo la Igogo mjini Mwanza imeahirishwa kwa mara nyingine tena hadi Juni 26, mwaka huu.
Katika kesi hiyo, Waislamu kadhaa wanashitakiwa kwa kutamka maneno yaliyodai kuwa serikali imekuwa ikipokea maelekezo ya Kanisa katika baadhi ya utendaji wake.
Kesi hiyo itatajwa tarehe hiyo baada ya faili lililodaiwa kupelekwa kwa mwanasheria mkuu kurejeshwa tena kwa mwendesha mashitaka.
Kesi nyingine Na. 1159/99 inayowahusu wahadhiri saba nayo imehahirishwa hadi Mei 31, mwaka huu.
AKINAMAMA
MOSHI WAHOJI
Serikali kupeleka viongozi
ili wakanyanyase
AKINAMAMA mkoani Kilimanjaro, wametaka kujua iwapo serikali imewapelekea viongozi ili wakawanyanyase.
Viongozi hao wamedaiwa kuwazuia akina mama Waislamu wasifanye mkutano wao bila ya maelezo.
Akina mama waliozuiwa kufanya mkutano wamedai kunyanyaswa na kudharauliwa.
Wamesema, walifungiwa milango na kupewa maelezo kuwa aliyefunga kaenda Kanisani na kuacha maagizo wamsubiri mpaka arudi.
Imeelezwa aliyefunga milango ya ukumbi ni Mkuu wa Shule ya Mwenge.
Mwalimu huyo mama Miriam Urio amedaiwa kufunga milango na kuacha maagizo kuwa Waislamu wamsubiri mpaka arudi Kanisani.
Baada ya kusubiri hadi saa tano na nusu akina mama hao walilazimika kufanyia mkutano wao nje.
Wamesema baadae Mwalimu huyo alipohojiwa alidai alifunga ukumbi kwa agizo la Mkuu wa Mkoa.
Amedaiwa kusema, Mkuu wa Mkoa, Mhe. Philemon Sarungi alimpa agizo ukumbi wa Waislamu usitumike kwa shughuli yoyote. Taarifa nyingine zimedai kuwa Mkuu wa Polisi ndiye aliyezuia.
"Huo ni uchokozi tunataka Sarungi atueleze ndiye kaagiza uchokozi huu. "Hall" tumejenga kwa nguvu zetu vipi tuzuiwe kulitumia", alisema mama mmoja.
Bi Halima Athumani mwenye umri wa miaka ipatayo 80 aliwaliza waliohudhuria pale alipotoa historia ya ukumbi na shule ya Mwenge.
Pamoja na uzee wake unaostahili kusamehewa funga za faradh, aliamua kufunga sunna siku tatu. Alisema, hiyo ni kumshitakia Allah watu wanaouza na kudhulumu mali za Waislamu.
Juhudi za gazeti hili kumpata Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na RPC na Mkuu wa shule ya Mwenge kuzungumzia suala hili hazikuweza kufanikiwa.
Akina mama Waislamu wapatao 360 waliokutana nje ya ukumbi uliofungwa waliamua wakutane na Mkuu wa Mkoa Mei 14.
Katika mkutano huo wamesema, watamtaka Mhe. Sarungi awaeleze iwapo ndiye aliyemtuma Mama Miriam Urio awanyanyase.
Tatizo la ukumbi wa mikutano wa Waislamu ulio ndani ya shule ya Mwenge na shule yenyewe ni la muda mrefu sasa.
Imedaiwa upo mpango wa kuitoa shule hiyo kwa baadhi ya watu. Na ili kulifanikisha zoezi hilo, kupitia Bakwata ilikuwa ukumbi huo uuzwe.
Baada ya zoezi la kuuzwa kukwama imeletwa hoja ya ukumbi kujengwa eneo lingine.
Waislamu wanadai hiyo ni mbinu ya kuwapora ardhi na majengo yao, jambo ambalo hawatalikubali.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |