Wenye ndevu, kofia wazuiwa kusafiri

WASAFIRI waliokuwa wamevaa kofia walikwamishwa kwa muda na polisi kuendelea na safari zao mwishoni mwa wiki.

Waliopata adha hiyo walikuwa pia wanawake waliokuwa wamevaa Hijabu.

Adha hiyo iliwapata katika eneo la Chamakweza ambapo polisi waliweka kizuizi Mei 7, mwaka huu.

Polisi hao wakiwamo FFU walikuwa wakizuia wanachama wa CUF kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze kuhudhuria mkutano uliokuwa ukihutubiwa na Prof. Lipumba.

Wanachama hao walikuwa katika msafara wa magari matano. Magari hayo yalipofika eneo la Chamakweza walizuiwa na polisi kuendelea na safari, zikitolewa sababu za kisheria za kipolisi (Trafic).

Pamoja na wanachama hao kujieleza kuwa walikodi magari hayo, polisi walishikilia uamuzi wao wa kuyataka yarudi kwa kuwa hayana TLB ya Chalinze.

Lakini hata gari iliyokuwa na TLB ya Dar - Msata ikiwa katika safari zake za kawaida iliamuliwa irudi.

Kwa kuona abiria wenye ndevu na kofia, polisi wakaamuru gari hilo Na. TZJ 4641 lililokuwa likiendeshwa na Bw. Laswai nalo lisifike Chalinze.

Baada ya kuzuiwa kwa muda mrefu abiria hao waliruhusiwa kuendelea na safari.

Wale ambao magari yao yalizuiwa, waliamua kwenda kwa miguu kutoka Chamakweza hadi Chalinze.

Chamakweza ni eneo kati ya Ruvu na mji mdogo wa Chalinze.

Wakikimbia mchakamchaka, wengi walifika Chalinze mkutano ukiwa umekwisha.

Magari yaliyozuiwa yalibaki katika kizuizi hicho ambapo baada ya polisi kuondoka waliwafuata wanachama hao Chalinze kuwarudisha Dar es Salaam.

Watu watano walikamatwa katika sakata hiyo na kuwekwa rumande kituo cha polisi Bwilingu Chalinze. Walifikishwa mahakamani Mei 8 na kusomewa shitaka, kuwazuia polisi kufanya kazi zao katika kizuizi.

Kesi hiyo itatajwa tena Juni 30 katika mahakama ya wilaya Bagamoyo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook