WAISLAMU wametakiwa wauvue uoga ili kuondoa dhulma.
Wameambiwa wasipokuwa jasiri, wataendelea kutumiwa kama vikapu vya wengine kuvunia.
Nasaha hizo zimetolewa na Sheikh Ahmed Zuberi hivi karibuni mjini Dodoma.
Sheikh Zuberi amesema, nusra haitawatafuta wanaodhulumiwa, bali wao waitafute.
Amesema, hapana budi dhalimu aelezwe wazi wazi uovu wake.
Ametoa mfano wa vijana wa pangoni ambao walimkabili bila woga mtawala katili wa Rumi, Dakyanus.
Sheikh Zuberi amesema, watu wakiwa waoga hakuna anayewajali, kwani hata wakiwa wengi huwa kama povu.
Sheikh amesema, kwa woga uliopo, zinapoelezwa dhulma wanazofanyiwa Waislamu, baadhi ya watu huona ni taarifa ngeni na kuwaandama wanaolalamika.
Amesema, dhulma iliyopo nchini itaondoka iwapo
uwingi huu wa povu utakoma.
MAUAJI ya raia wanne yaliyofanywa na polisi eneo la Mwembechai mwezi Februari mwaka juzi hayamo katika ripoti ya ukiukaji wa haki ya uhai ya kila binadamu kati ya 1997 na 1999 iliyotolewa na taasisi moja isiyo ya kiserikali.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Legal Human Rights Centre imeorodhesha vifo kadhaa vilivyotokea kati ya miaka hiyo vinavyoonesha kukiukwa kwa haki hiyo.
Mapitio ya magazeti yaliyofanywa na taasisi hiyo yanaonesha ajali za barabarani zinaongoza kwa kusababisha vifo vingi zikifuatiwa na kujinyonga na ujambazi.
Aidha, operesheni za polisi dhidi ya watu wanaotuhumiwa kufanya uhalifu nazo zimetajwa katika ripoti hiyo kusababisha vifo vingi vya raia kinyume na haki za binadamu.
Hata hivyo, taasisi hiyo inayoongozwa na Askofu mstaafu Elineza Sendoro haikuorodhesha tukio la Mwembechai katika matuko ya vifo vya aina hiyo vilivyotokea katika kipindi hicho.
Wengine wanaounda taasisi hiyo ya haki za binadamu isiyo ya kiserikali ni pamoja na Dk. Ringo Tenga, Dk. Seng'ondo Mvungi na Dk. Palamagamba Kabudi ambao wote ni wahadhiri waandamizi wa Kitivo cha sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ripoti yake LHRC imesisitiza kuwa haki ya uhai ni ya msingi ambayo bila ya hiyo haki nyinginezo hukosa maana.
Ripoti nyingine taasisi hiyo imesema ingawa Tanzania inaaminika ni nchi ya amani na utulivu, imekuwa na matukio mengi ya utesaji, ukiukaji wa haki mbalimbali za binadamu na mauaji ya watu wasio na hatia yanayofanywa na vyombo vya dola.
Ripoti hiyo imetaja matukio ya kinyama yaliyofanywa na vyombo vya dola katika hifadhi za Taifa za wanyama.
Matukio mengi yametajwa kutokea katika hifadhi ya Serengeti ambapo watu waliodaiwa kuwinda katika hifadhi hiyo wameripotiwa kuteswa kinyama hadi kufa au kupigwa risasi na askari wa wanyamapori.
"To kill person for whatever reason is violation of that person's rights", imesisitiza ripoti hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza ikiwa na maana "kumuua mtu kwa sababu yoyote ile ni kukiuka haki ya uhai ya mtu huyo".
Ripoti hiyo imeorodheshwa watu 20 waliouawa kinyama katika kuwalinda wanyama.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |