MAIMAMU Sheikh Juma wa Masjid Hijaaz
na Sheikh Rajabu Mkonga wa Masjid Kadiria Mgaza hivi karibuni waliitwa
kituo cha polisi Magomeni na kuhojiwa.
Maimamu hao ambao Misikiti wanayoiongoza iko maeneo ya Kigogo/Luhanga waliitwa kituoni hapo na kuhojiwa kwa kudaiwa kuchanganya dini na siasa na kuandaa mihadhara inayodaiwa kuwa ya kashfa.
Maimamu hao waliitwa kituo cha polisi Magomeni kwa barua rasmi. Barua zenye kumbukumbu namba MAG/A.4/9/A/Vol II/258 na MAG/A.4/9/A/VolII/259 zote za Mei 4, mwaka huu ziliwataka wenyeviti, makatibu na Maimamu wa Misikiti hiyo wafike kituo cha polisi Magomeni kuonana na OCD Mei 5, mwaka huu baada ya swala ya Ijumaa.
Hata hivyo, viongozi hao wa Misikiti walifanikiwa kuonana na OCD Mei 6, mwaka huu badala ya Mei 5, mwaka huu siku ambayo OCD hakuwepo kituoni hapo kwa muda wote viongozi hao wa Misikiti waliokaa kituoni hapo kumsubiri.
Katika mahojiano hayo yaliyoendeshwa kwa utaratibu wa kuhojiwa viongozi wa Msikiti mmoja mmoja, polisi ilidai kuwa uongozi wa Masjid Kadiria Mgaza uliandaa muhadhara wa kashfa ambao ulisababisha kero kwa watu wengine.
Aidha, uongozi Masjid Hijaaz, hasa Imamu wake alidaiwa kuchanganya dini na siasa katika mawaidha yake kwa waumini na pia Imamu huyo alidaiwa kuwa ni mwanachama wa chama cha wananchi CUF na kwamba pamoja na hayo anafanya kampeni kwa kugawa khanga.
Kutokana na madai hayo ya polisi, imamu alitaka ushahidi wa madai hayo, lakini ushahidi uliotolewa na polisi ni kuwa habari hizo ni za kuaminika zilizotolewa na wanaCCM wanaoswali Msikiti huo kwa kushirikiana na ofisi za CCM zilizopo katika eneo hilo.
Aidha, Imamu alimtaka afafanue maana ya dini na siasa ili ionekane siasa haifai kuzungumzwa Msikitini. Hata hivyo, OCD hakuweza kutoa ufafanuzi huo bali alimtaka Imamu awafundishe waumini wake namna ya kutawadha ili waswali vizuri badala ya kujiingiza katika siasa.
Kutokana na hali hiyo, ilibidi Imamu atoe
ufafanuzi wa dini na siasa na kuelezea nafasi ya siasa katika Uislamu.
Hatimaye OCD aliwaruhusu waondoke lakini huku akiwatahadharisha kuwa endapo
wataendelea kuchanganya dini na siasa basi atawakamata kwa sababu nyumba
zao aianzijua fika.
IWAPO serikali ya CCM imewakosea wananchi itaelezwa ukweli.
Kuisifu kuwa inatenda haki itakuwa kuikejeli na unafiki. Hayo yamesemwa na baadhi ya waumini mjini Dodoma.
Wamesema hayo kufuatia kukamatwa Bint mmoja na polisi na kuhojiwa kwa masaa kadhaa.
Khadija Ramadhani (24) alikamatwa Mei 9 na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.
Katika kumhoji, polisi walitaka kujua iwapo Bi Khadija alishiriki kuikashifu CCM na serikali yake.
"Watu hawakuuliwa Mwembechai, Chuki hakupigwa risasi, akina mama hawakudhalilishwa, Msikiti haukuvunjwa?" amehoji Ummu Habiba.
"Vikao vya CCM havikupongeza mauaji yale? Rais Mkapa hakukataa kuunda Tume ? Je, serikali haiwalindi waliotoa amri "piga yule" wasifikishwe mahakamani?" amehoji tena.
Amesema, hata Mhe. Rais Mkapa ataona ni unafiki na woga kwa watu waliotendewa haya kuisifu CCM na serikali yake kuwa imewaongoza vizuri.
"Rais Mkapa amesema, serikali yake ni ya ukweli na uwazi. Tutamueleza ukweli Waislamu wameuliwa Mwembechai kwa shinikizo la Paroko wa Kikatoliki. Na serikali inamlinda na walioua", amesema mama Adili.
Baadhi ya akinamama wamesema, kama polisi Dodoma ni mabingwa wa kuhoji wakamhoji Padri Cumillus Lwambano, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Yusuf Makamba na Kadinali Polycap Pengo.
"Wakawahoji waliochochea mauaji, walioua na walioyaunga mkono ndio wawafuate wanaolalamika. Au Maaskofu wao wana kinga hawaguswi?" amehoji Ukht Ramla.
Kukamatwa na kuhojiwa Bi Khadija, kunafuatia hafla ya mwaka mpya iliyofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.
Katika hafla hiyo, ilisomwa risala iliyosema
kuwa namna pekee ya kuisaidia CCM isiendelee kudhulumu ni kuinyima kura
Oktoba.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |