TUME ya Uchaguzi hivi karibuni imeteua Wasimamizi na Waratibu wa Uchaguzi Mkuu.
Wateuliwa hawa ni waajiriwa wa serikali. Tayari wana ajira zao na hivyo kuwa na njia ya uhakika ya maisha.
Kwa vile ni watumishi wa serikali, mishahara yao hutoka Hazina. Na ni kodi za wananchi zinazojaza Hazina ya serikali.
Uteuzi wao unamaanisha ajira ya muda. Ajira ambayo itadumu kwa masiku au miezi kadhaa.
Ni ajira inayoandamana na posho za semina, usafiri, kufanya kazi nje ya kituo cha kazi, masaa ya ziada na posho ya kufanya kazi usiku.
Japo ni ajira ya muda, lakini ina kipato si haba. Mwenye kibanda chake kilichokwama anaweza kukimalizia. Anayedaiwa ada ya shule kwa watoto wake atamalizia na hata kupata mtaji wa biashara.
Mabilioni ya shilingi tunayoelezwa kutumika katika uchaguzi ni pamoja na kuwalipa watu hawa.
Na fedha hizi pia ni kodi ya wananchi.
Katika kulipa kodi hakiangaliwi kisomo cha mtu, dini yake wala kabila lake. Sheria huwabana wote sawiya.
Fursa kama hizi za kuwa Waratibu na Wasimamizi wa Uchaguzi ni chache. Si walipa kodi wote wanaoweza kuipata.
Wanateuliwa wachache kufanya kazi kwa niaba ya wengine, lakini pia kuchuma kutoka Hazina kwa niaba yao vile vile. Na hilo halina tatizo.
Lakini jaalia walioteuliwa wote ni kabila fulani au wa dini fulani. Maana yake ni: Kwanza kabila au watu wa dini hiyo ndio watadhibiti zoezi lote la uchaguzi.
Wakimchukia mtu asiye wa kabila lao au dini yao waweza kuikwamisha fomu yake. Wakatafuta dosari za 'kupika' ilimuradi tu ionekane hakutimiza masharti.
Waweza kuwa 'mahakimu' wasio waadilifu katika kupokea malalamiko na pingamizi kutoka kwa wananchi na wagombea wengine.
Zoeizi la kupiga, kuhesabu kura na kutoa matokeo laweza pia kutokufanywa kwa uadilifu.
Lakini pili, watu wa kabila hilo au dini hiyo ndio pekee wanaopewa fursa ya kula fedha hizo za Hazina kama posho.
Hao ndio watakaomalizia vibanda vyao, watakaowasomesha watoto na kuwa na miradi ya kuingiza kipato zaidi ya mshahara wa kawaida.
Na isisahaulike, wamechaguliwa kwa nafasi zao serikalini. Hivyo huteuliwa pia kwenye Tume nyingine pengine zenye posho zaidi ya hii ya Tume ya Uchaguzi.
Tatu, kwa vile wameingia kwenye kusimamia uchaguzi kwa nafasi zao, maana yake huko waliko serikalini ni kabila lao au dini yao inayotawala.
Viko vitendawili tata katika maisha ambavyo utatuzi wake wahitaji kukaa kitako na kuleta fikra.
Iwapo tunajenga Taifa lisilo na ukabila, haitarajiwi kabila fulani lihodhi mamlaka jeshini, polisi au sekta yoyote serikalini. Watu wa Mafia wakiwa wavuvi haitashangaza. Wahaya wengi wakiwa wakulima wa matoke na kahawa si jambo la kuhoji.
Lakini Wahaya hao hao wakiwa ndio waliojaa Ikulu au kushika nyadhifa zote katika wakuu wa mikoa na wilaya lazima watu wawe na wasiwasi na wahoji.
Tunasema tuna mshikamano wa kitaifa. Tunapiga vita utengano kwa misingi ya dini. Tunataka tuongozwe kwa uzalendo na hisia za utaifa sio za dini.
Lakini ni ukweli kuwa maadhali watu wanaruhusiwa kuwa na dini zao hisia za dini zipo mioyoni kwao.
Ndio maana japo serikali haina dini, wapo watumishi wa serikali wanaingia ofisini wakiwa na misalaba shingoni au kutundika msalaba kwenye gari ya kazini na wengine kuining'iniza Tasbih.
Ofisi yenye watumishi ishirini na wote wakawa wa dini moja hutawazuia kufikiri kama watu wa dini moja katika umoja wao.
Huwezi kuwatarajia kwa mfano wakaweka ratiba ya vikao yenye kugongana na siku au saa yao ya Ibada. Au wakazingatia kuepuka tatizo hilo lisitokee kwa watu wasiokuwa wa dini nyingine.
Siku za Jumapili na Ijumaa zinavyotazamwa na serikali na kutumiwa kwa kazi yaweza kuwa ni kielelezo. Ni vigumu kuamini vipi utaifa utajengwa kwa watu wa kabila au dini moja kupewa leseni ya kuhodhi mamlaka na kula fedha za Hazina kwa niaba ya wengine.
Ni mantiki ngumu kueleweka vipi hisia za kidini na ubaguzi unaoandamana nazo unavyoweza kuondolewa kwa kujaalia fursa muhimu za uongozi na utendaji serikalini kuwa milki ya watu wa dini fulani!
Je, ni kweli viongzi wa serikali wanajenga utaifa? Hawaongozwi na hisia zao za kidini, hawaangalii maslahi ya ya dini zao kabla ya Watanzania?
Kwanini kwa mfano wateue wasimamizi wa uchaguzi wa dini moja. Je, hiyo ndiyo njia ya kuendesha uchaguzi bila ya ubaguzi wa kidini?
Je, watu wa dini nyingine hayupo mwenye sifa ya kufanya kazi hizo? Kama hakuna kwanini.
Kwanini idhaniwe wale 'waliobaguliwa' au walioonekana hawafai wataikubali hali hiyo?
Je, wao hawataki hizo posho. Hawataki kusomesha watoto wao na kumalizia vibanda vyao! Je, wao ni wa kutoa kodi tu, zinaliwa vipi si juu yao!
Je, inadhaniwa hawaoni, hata wakiona hawaelewi
au hata wakielewa hawawezi kufanya kitu!
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |