Na Ahmed Hussein
WAKATI viongozi wakijaribu kuwalazimisha wananchi waamini kiini macho cha mafanikio yao kwa kigezo cha misamaha ya madeni, hali halisi ya maisha ya wananchi mijini na vijijini inafichua siri kubwa kuwa viongozi hawapo madarakani kwa ajili ya wananchi.
Hali duni ya maisha ya wananchi wengi inatulazimu kuhoji kuwa hiyo tathmini ya kukua kwa uchumi imefanywa katika mazingira gani. Je, imefanywa kwa kuzingatia maisha ya wananchi hao walio wengi au imefanywa katika mazingira ya Masaki, Oysterbay, Msasani na Mbezi Beach kwenye mahekalu ya wakubwa au waheshimiwa?
Matamshi ya viongozi wengi ni ya kujisifu wenyewe kuwa wamepata mafanikio katika awamu yao, yanathibitisha kuwa hawana habari na wala hawajali mateso wanayoyapata wananchi.
Hivi karibuni, RTD katika kipindi chake cha kijiji chetu, ilifanya mahojiano na wananchi wa kijiji cha Mtamba kilichopo katika wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Katika mahojano hayo, Mwenyekiti wa kijiji alielezea matatizo mbalimbali yanayokikabili kijiji hicho ambayo yalimfanya Mwenyekiti huyo aseme wazi kwamba wananchi kijijini hapo wanateseka vibaya sana.
Mtangazaji wa Radio hiyo alianza kwa kuulizia shughuli ambazo wanakijiji wanazifanya ili kuendesha maisha yao ya kila siku.
Mwenyekiti: Katika kijiji changu cha Mtamba wananchi wanaendeleza maisha yao kwa kilimo.
Mtangazaji: Kilimo cha mazao gani?
Mwenyekiti: Mazao ya chakula.
Mtangazaji: Mazao gani, hebu tutajie moja moja.
Mwenyekiti: Kama mihogo, mahindi, mtama na mazao ya biashara kama korosho.
Mtangazaji: Sasa katika haya mazao ya chakula unaonaje yanatosheleza mahitaji ya familia, kaya hadi kaya au hayatoshelezi?
Mwenyekiti: Inategemea, kwa baadhi ya watu yanatosheleza na kwa wengine kama unavyofahamu kawaida ya binadamu, huyu ana hili na huyu na hili, kuna mwingine anajimudu lakini kuna wengine hawajimudu.
Mtangazaji: Hali ya kipato cha wanakijiji wa hapa Mtamba ikoje.
Mwenyekiti: Hali ya kipato kwa kweli sio zaidi, ya wastani tu.
Mtangazaji: Mnafanya jitihada gani basi kuinua kipato hiki?
Mwenyekiti: Kuinua kipato hiki, tunakata mikaa, ukilima, ukipata vyakula ndio mapato yenyewe. Lakini maendeleo hasa ya kuzidi hapo hakuna.
Mtangazaji: Hili suala la kukata mikaa pengine unaonaje haliathiri mazingira?
Mwenyekiti: Mimi naona kamba halileti madhara yoyote kwa sababu msitu tunao mkubwa sana, tunalima na tunakata mikaa lakini haiwezi kuathiri nchi.
Mtangazaji: Na pia umezungumzia zao la biashara, korosho, je hali za zao hilo ikoje hivi sasa, je, linatosheleza mahitaji ya kibiashara kwa wanakijiji au vipi?
Mwenyekiti: Halitoshelezi kwa sababu korosho kwa mwaka huu, hakuna, mikorosho yote imealika lakini haikuzaa mapato yoyote. Tuna korosho za kutafuna tu.
Mtangazaji: Ni sababu gani iliyopelekea hali hii kuwepo?
Mwenyekiti: Sababu mimi sifahamu kwa sababu hatuna mtaalamu wa kujua nini kimefanya mikorosho iwe hivi.
Mtangazaji: Unaonaje huduma za jamii katika kijiji hiki, zipo zozote ambazo zinatosheleza mahitaji ya jamii?
Mwenyekiti: Huduma za jamii naona hakuna.
Mtangazaji: Ni huduma kama ipi mnaikosa?
Mwenyekiti: Kama zahanati hatuna, maji safi hatuna, kwa hiyo jamii inateseka vibaya sana.
Mtangazaji: Sasa katika suala la huduma za jamii, umesema hamna zahanati wala maji safi, Tukianza na zahanati ni sehemu gani wanakijji wa Mtamba wanapata huduma hii?
Mwenyekiti: Wanakijiji wanapata huduma hii Senyi au Musangani huko ndiko kwenye zahanati.
Mtangazaji: Kutoka hapa mpaka Senyi ni umbali gani?
Mwenyekiti: Kutoka hapa kwenda Senyi ni umbali wa kilometa kumi na mbili au kumi na tatu.
Mtangazaji: Na endapo kuna mgonjwa amezidiwa mnafanya vipi kufika huko?
Mwenyekiti: Kama mgonjwa amezidiwa huwa tunafanya msaada kumbeba kwa kitanda kumpeleka.
Mtangazaji: Na hili suala la maji safi umesema hapa kijijini Mtamba hampati maji kabisa, inakuwaje?
Mwenyekiti: Maji tunapata lakini si salama kutokana na visima vyetu vilivyokaa vibaya, na muda huu tunasema kinamama wanalinda.
Mtangazaji: Je kuna wataalamu wowote wa afya wanaofika hapa kijijini katika suala hilo?
Mwenyekiti: Wataalamu wa afya bado (hawajatufikia), NAPLAN walikuja kusema masuala ya visima lakini utekelezaji bado.
Mtangazaji: Huduma za barabara?
Mwenyekiti: Huduma za barabara tunajitahidi hivyo hivyo kadiri ya uwezo wetu. Tunapoona shimo tunaziba, tunapoona majani mengi tunalima lakini hakuna huduma inayoendelea.
Mtangazaji: Na kwa njia ya usafiri, pengine mkitaka kutoka hapa kwenda vijiji vingine vya jirani mnatumia nini?
Mwenyekiti: Tunatumia miguu. Tunatembea tu kwa miguu hakuna usafiri wowote.
Mtangazaji: Hebu tufahamishe mafanikio na matatizo yaliyopo hapa kijijini.
Mwenyekiti: Mafaniko na matatizo, tunajikwamua hivyo hivyo, kushirikiana na wanakijiji, tunasukumana tufanye hivi, tufanye hivi.
Mtangazaji: Tulitokea huko katika huduma za jamii, tumefahamu kuwa tatizo ni hospitali, maji safi na nini hasa kikwazo kingine?
Mwenyekiti: Kikwazo kingine tumesema kwamba tunateseka, tunalima lakini nguvu zetu zinapotea kutokana na wanyama waharibifu wanaotuathiri sana.
Mtangazaji: Hawa wanyama waharibifu ni kama wepi?
Mwenyekiti: Mkubwa hasa ni tembo.
Mtangazaji: Umesema kwamba kuna tatizo la wanyama waharibifu, ni wanyama gani hao Bwana Mwenyekiti.
Mwenyekiti: Wanyama waharibifu ni tembo.
Mtangazaji: Hawa tembo wanatoka wapi mpaka kuingia hapa kijijini Mtamba?
Mwenyekiti: Tembo wanatoka msituni huko, kuna msitu mkubwa sana kwa hiyo wanatoka huko (kuja) kushambulia vyakula. Hivi ninavyozungumza wanakijji wameshashambuliwa mashamba yao, si chini ya hekari hata sitini, mihogo yote imeliwa, hapa tulipo, tupo, hali yetu mbaya sana.
Mtangazaji: Ni hatua zipi ambazo mmechukua kufuatilia ama kuripoti tatizo hili?
Mwenyekiti: Mimi nilichukua jukumu la kutoa taarifa kwenye kata, kata wakaniambia tuma barua. Nikatuma barua kwa Mkurugenzi, akasema nitakupa jibu.
Yule Bwana niliyemtuma akasema, mimi sitokwenda (kijijini) mpaka nipate jibu, akabaki pale. Ikabidi waende Maliasili, wakaonana na jamaa (wanaohusika). Wakamwita Bwananyama. Bwananyama akasema, bunduki yangu (yake) imepasuka.
Mpaka sasa sijapata bunduki (nyingine), wewe nenda (rudi kijijini) utapata jibu. Yule Bwana akasema sikubali. Siendi mpaka nipate jibu (ili) nikirudi kijijini nikatoe taarifa (kamili). Yule Bwana nyama akaambiwa aende mkoani kutafuta bunduki. Bwana (niliyemtuma) akaambiwa nenda bunduki imeenda kutafutwa mkoani (ikipatikana) tutakuja. Tukabaki hivyo hivyo.
Halafu upande wa Pwani International walikuja kutuambia kwamba tufanye huduma ya kuchimba mchanga. Kweli tukafuatilia gari wilayani. Afisa tarafa akaja na gari.
Siku tunafuata mchanga tukataka kumgonga tembo na gari. Nikamwambia Bwana Afisa Tarafa, pamoja na kusikia si unaona mwenyewe sasa unaniambia vipi? Akaniambia andika barua, nipeleke kwa Mkurugenzi, nikaandika barua ya pili na kumpa Afisa Tarafa mpaka hivi sasa jibu sijapata. Sasa sijui viongozi wanatufikiria vipi (kuhusu) kijiji chetu?!
Baada ya mazungumzo na mwenyekiti, mtangazaji akazungumza na Katibu wa kijiji.
Mtangazaji: Hebu tufahamishe utaratibu wa kudhibiti chakula kwa akiba ya baadaye kuepukana na baa la njaa ukoje?
Katibu: Kama Mwenyekiti alivyozungumza kuhusiana na tatizo la wanyama waharibifu kwa kweli nguvu zetu haziweki (ziada) ya chakula, hivyo hatuweki kipaumbele katika (suala la) kudhibiti chakula. Isipokuwa kama tutapata mtu wa kutusaidia kuondoa wanyama hao basi nina hakika kijiji changu hakitakuwa na njaa.
Mtangazaji: Kwa hiyo, unataka kusema kwamba hata mahitaji ya chakula ya kila siku yanaathirika kutokana na tatizo la wanyama waharibifu?
Katibu: Ni hivyo hasa, sababu kuu ni hiyo. Wanakijiji wanajitahidi kulima (kidogo kidogo) nusu nusu, hawana nguvu hasa ya kulima ili kuweza kuinua uchumi, kwa mazao ya chakula na biashara.
Pia mtangazaji huyo alizingumza na Bi mkubwa mmoja wa kijiji hicho.
Mtangazaji: Bibi Maua Maulid hebu tufahamishe hapa kijiji kuna mila zozote za asili unazozifahamu?
Bi Maua: Zipo mila za asili kama vile kilimo lakini kama ilivyosemwa, neno (tatizo) la wadudu linatuchokesha. Wadudu wakiingia hawabakishi kitu. Wanakula, watu wanachoka, kila wakijitahidi wanachoka.
Vile vile hatuna kisima kizuri (na sisi) tupate maji, maji safi hamna.
Mtangazaji: Wewe ulikuwepo hapa kijijini toka zamani sasa unaweza kutufahamisha vipi kuhusiana na asili ya kijiji hiki. Mlikuwa mnaishi vipi hasa katika kuwalea watoto wenu?
Bi Maua: Tulikuwa tunawalea hivyo hivyo kimasikini masikini.
Huku viongozi wa CCM wakijipigia debe kwa ajili ya uchaguzi wa Oktoba, hiyo ndiyo hali ya wananchi ambayo kila uchao inazidi kuwa duni. Wananchi wanazidi kupata mateso na masumbuko ya maisha. Mbali ya dhiki ya maisha, wananchi wanakosa huduma muhimu za jamii. Wananchi hawa lazima wahoji yale mapesa tuliyokopa kiasi cha kushindwa kulipa mpaka wadeni wanaona bora watupunguzie madeni yalifanyiwa kazi gani.
Wanashindwa kuielewa mantiki ya misamaha ya
madeni kwani hawakuhusishwa katika kukopa wala kutumia!
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |