MASHAIRI

‘Usiwake'

Haya goma mshumaa, mnene awe tabuni,
Kwa giza litoshupaa, tena asione ndani,
Shati kitaka kuvaa, atafute iwe soni,
Usiwake mshumaa, mnene awe gizani.

Leo goma mshumaa, tumjue bingwa nani,
Giza hajalizoea, atapandisha shetani,
Mkanda hatauvaa, tai liwe kiunoni,
Usiwake mshumaa, mnene awe gizani.

Sasa goma mshumaa, ukomeshe kisirani,
Na suti hataivaa, kugombeza jukwaani,
Atageuka kichaa, ndipo atakuthamini,
Usiwake mshumaa, mnene awe gizani.

Tena goma mshumaa, ulitupwa uvunguni,
Chumbache kilipojaa, kwani alikuthamini!
Vumbi tele ulijaa, aliyekujali nani?
Usiwake mshumaa, mnene awe gizani.

Ndiyo goma mshumaa, asiione sahani,
Atapozidiwa njaa, atatia akilini,
Adabu umemtia, hatasema kaueni,
Usiwake mshumaa, mnene awe gizani.

Hebu goma mshumaa, unachohofu ni nini?
Atabaki analia, hatasini gizani,
Hao wake mashujaa, utawatia kwapani,
Usiwake mshumaa, mnene awe gizani.

Hasa goma mshumaa, kwa kushika yako peni,
Muache mwenye kuua, weka tiki hapo chini,
Kwa cheupe kiso doa, kijani mpige chini,
Usiwake mshumaa, mnene awe gizani.

Ala!! goma mshumaa, ukifika kituoni,
Iwe jino au pua, usiwahofu wahuni,
Wewe tiki yako tia, tumbukiza sandukuni,
Kama mbwa atalia, mnene yupo tabuni.

Sawa goma mshumaa, umtie kilioni,
Mwembechai aliua, na kukuita muhuni,
Ni zamu yake kulia, usimpe afueni,
Usiwake mshumaa, mnene awe gizani.

Katu goma mshumaa, Luanda kaditamani,
Sitaki kushuhudia, mitaani wakijani,
Mitini wakipepea, wataing’oa mwakani,
BUYU hili kuling’oa, ni thawabu kwa Manani.

K.S. Luanda (NOLO),
Dar es Salaam.


Mungu na chama, bora nani?

Bismillah naanza, jinalo uliomwema,
Wa mwishoni na wa kwanza, Rabi mwingi wa rehema,
Rabi nilinde naanza, lumbano hili kusema,
Kati ya Mungu na chama, jamani mbora nani?

Rabi alotukuzika, na chama mbora nani?
Kidimu mlo kishika, huko Tanga nijibuni,
Pwani Lindi ninafika, hadi Moro kwa watani,
Kati ya Mungu na chama, jamani mbora nani?

Rabi chini mwamuweka, kisa mwapata sumni,
Yake kamwe kuyashika, anenayo vitabuni,
Kidumu hadhi chashika, namba wani Mola chini,
Kati ya Mungu na chama, jamani mbora nani?

Dini mwavua kabisa, mnakimbia misikitini,
Dini ichini kabisa, kwa vyeo vya wenyekiti,
Mwayaacha Makanisa, imara yajizatiti,
Kati ya Mungu na chama, jamani mbora nani?

Jibuni wote wa Bara, kote nako visiwani,
Yaani Mungu si mbora? Yake hayana thamani!
Kidumu mwafanya bora, dini mwanadi jamani!
Kati ya Mungu na chama, jamani mbora nani?

Sio kama nakataza, ndugu kuwepo vyamani,
Rabi hakutukataza, kama vya sawa hakini,
Rabi anavyokataza, vilivyomo dhulumani,
Kati ya Mungu na chama, jamani mbora nani?

Kaditama nafikia, kalamu naweka chini,
Kazi ninawaachia, fikirini chaguzini,
Huo ni wangu usia, ulonijia kichwani,
Kati ya Mungu na chama, jamani mbora nani?

Almasi H. Shemdoe,
“Tunda la Matumaini”
S.L.P. 33265,
Dar es Salaam.


Vipi mtani!

Mtani kafanya mambo, hili limepindukia,
Walio ndani na ng’ambo, tendo wameshuhudia,
Bosi katia mgando, misani kukimbilia,
“Makamba kawa daraja, la kuvukia Kanisa”

Ilikuwa ya wawili, safari yao Upanga,
Mmoja akaghairi, shahidi wetu Runinga,
Ilikuwa Alufajiri, hakuna mtu kupinga,
“Makamba kawa daraja, la kuvukia Kanisa”

Kawahi misa ya kwanza, kwaya pia kawekewa,
Kapewa damu ya bwana, ndio ya kuokolewa,
Mkate mwili wa bwana, dhambiyo kuondolewa,
“Makamba kawa daraja, la kuvukia Kanisa”

Akapewa kinafasi, nasaha zake alonge,
Akaanza binafusi, kupongeza meno “nite”,
Ni dola kila kikosi, budi Kanisa likingwe,
“Makamba kawa daraja, la kuvukia Kanisa”

Uchaguzi wa Rais, wakwenu ndiyo apate,
Wengine hawana chansi, kwani hawana chochote,
Na mgawane nafasi, katika wizara zote,
“Makamba kawa daraja, la kuvukia Kanisa”

Mwisho Pasaka hii, akaomba ije tena,
Apigishwe na magoti, ale mkate wa bwana,
Avae koti na tai, na msalaba mpana,
“Makamba kawa daraja, la kuvukia Kanisa”

Kweli inauma sana, lakini tutasema,
Isilamu huna tena, Mola ndiye alosema,
Cha moto utakiona, siku hiyo ya Kiama,
“Makamba kawa daraja, la kuvukia Kanisa”

Saidi M. Buweta,
Mwenge Islamic Center
S.L.P. 22010,
Dar es Salaam.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook