Tishio la ukame
ILANI ya ukame ishalia. Sehemu nyingi hazikupata mvua ya masika kama ilivyoada.
Mazao yananyauka ikiwa ni ishara ya njaa. Lakini hata maji ya kunywa itakuwa tabu.
Katika baadhi ya maeneo mabwawa yanayotegemewa yanakauka.
Mabwawa hayo ni pamoja na lile la Nigwa mkoani Shinyanga na la Kazima, Tabora.
Wakati hali hiyo ikijiri, serikali inasema haina uwezo wa kuwekeza katika maji. Na hivyo imewataka wananchi watumie maji yanayopatikana kwa uangalifu.
Nasaha hizo zimetolewa na Waziri wa Maji, Mhe. Mussa Nkangaa wiki iliyopita mjini Arusha.
Waziri Nkangaa akinukuliwa na vyombo vya habari amesema, ukame ulioko utaathiri maisha ya watu na mifugo.
Nini ufumbuzi, Waziri anasema watu watumie maji kwa uangalifu.
Wanachotegemea ni bwawa, bwawa lenyewe linakauka. Walitumieje kwa uangalifu!
Tatizo ni ukame. Maji hakuna. Tatizo si kuwa maji yapo lakini yanatumika ovyo.
Lakini hata hivyo, maji yanatumiwaje ovyo? Kwa kunywa maji mengi, kuoga mara mbili kwa siku, kunyweshea mifugo, kufulia au kumwagilia bustani!
Hatudhani kama yupo mtu ambaye atahemea maji kutwa aambulie ndoo moja kisha iyatumie kupigia deki nyumba yake!
Nasaha kama hizi tunadhani ni za kukwepa kuwajibika. Kwamba itakapotokea watu na mifugo yao wamekufa kwa ukame, serikali idai ilitoa tahadhari na mapema.
Maadhali serikali imeona hatari inayokuja ya ukame, ieleze ina mipango gani kuepuka madhara yatokanayo na ukame huo.
Kwa kujua hali ngumu itakavyowakabili wananchi, Bw. Nkangaa amenukuliwa akisema, kwa vile ni mwaka wa uchaguzi athari ya ukame itakayojitokeza, itawafanya watu waone viongozi waliopo madarakani hawajafanya lolote.
Hili ni suala la uhai wa wananchi, wala lisiingizwe kwenye malumbano ya kisiasa.
Muhimu, nini serikali ifanye kunusuru maisha ya watu na mifugo yao.
Nchi hii Mwenyezi Mungu kaijaaliya maziwa makubwa makubwa, chemchem, mito mingi isiyo kauka.
Itakuwa ni utovu wa shukrani kumtupia tena Mungu lawama kila utokeapo ukame.
Viongozi waliopo madarakani wajiulize, yapi
muhimu sana waliyofanya, iwapo leo watu waweza kufa kwa kiu ilhali katika
miji na vijiji jirani mito na maziwa yamefurika maji!
--
![]()
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |