Na Mwandishi Wetu
RAIS Mkapa amesema, wanaodai CCM haijafanya kitu wana uprofesa usio na sifa.
Amewataka wananchi wasibabaishwe na wale aliowaita waongo na vipofu wa kisiasa.
Rais Mkapa alikuwa akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara.
Amesema, serikali yake imepata mafanikio makubwa, lakini vyombo vya habari haviyaelezi.
Akitoa mfano alisema, zimekuwa zikijengwa shule za sekondari takriban 60 kila mwaka toka aingie madarakani.
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Philip Mangula, amemshutumu Prof. Lipumba kwa kile alichodai kuwa na kampeni chafu.
Kampeni hizo amezifafanua kuwa ni pale inaposemwa kuwa CCM haijafanya lolote na kwamba kuichagua tena CCM ni sawa na kukumbatia maradhi, ujinga na umaskini.
Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Mangula alikuwa akiongea na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki ofisi ndogo za CCM Lumumba.
Alhamisi iliyopita, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba aliongea na waandishi wa habari na kusema, Taifa linakabiliwa na matatizo ya umaskini, ujinga na maradhi ambayo kwa miaka 40 CCM imeshindwa kuyaondoa.
Alisema, sehemu nyingi nchini barabara hazipitiki, idadi kubwa ya watoto wanakosa elimu kutokana na umaskini huku mahakama zikiwa hazina hata karatasi.
Katika hali hiyo, Prof. Lipumba alisema, "Ukiikumbatia
CCM unakumbatia ujinga, maradhi na umaskini" na kutoa wito kwa wananchi
watafute watu wengine watakaoleta mabadiliko.
VIJANA kadhaa wamedai kuwekwa ndani na kufunguliwa kesi baada ya kuhama kutoka CCM.
Wamesema, awali walikuwa na 'kijiwe' chao kikiwa na bendera ya CCM lakini wakaamua wote kuingia CUF.
Kijiwe hicho kilikuwa katika makutano ya barabara za Madenge na Yombo.
Wamesema, badala ya kupandisha bendera ya CUF katika mlingoti wa zamani waliamua kuvunja kijiwe hicho wajengee kando kidogo. Wamedai walifanya hivyo kwa vile mlingoti wa awali ulikuwa karibu na nyaya za umeme.
Wamedai, wakiwa wanajenga sehemu mpya ya kutundika bendera wiki iliyopita walivamiwa na polisi ambao walichukua vifaa vyao vya ujenzi.
Wamesema, waliwekwa mahabusu polisi Chang'ombe na kupelekwa mahakamani siku ya pili yake.
Mahakamani wamedai kufunguliwa shitaka la kumtishia mkereketwa mmoja wa CCM na kuharibu mali ya CCM.
Wamesema, kesi yao itatajwa Juni 13 mahakama ya wilaya Temeke na wapo nje kwa dhamana.
Waliodai kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi ni Abdallah S. Mwinyimvua, Njiti Shomari na Shabani Gumbo. Wengine ni Said A. Nyoni, Fikiri Magoso na Juma Kitula.
Juhudi za gazeti hili kumpata Mkuu wa Polisi Chang'ombe hadi tunakwenda mitamboni hazikuweza kufanikiwa.
Mwenyekiti wa CCM tawi la Sandali, Hamisi Mwakaluka alikiri kusikia kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo, alidai huenda ni watu binafsi sio CCM. Tawi la CCM Sandali ndilo pekee lilipo jirani na tukio.
Wakati huo huo, mtafaruku mwingine baina ya wanachama wa CCM na CUF, umetokea eneo la Mchafukoge barabara ya Lumumba.
Hali hiyo ilitokea baada ya wanacama wa CUF kutaka kutundika bendera yao. Meta chache kutoka ile ya CCM wiki iliyopita.
Wakereketwa wa CCM waliwazuia kuweka mlingoti na baadae kukimbilia polisi ambapo walidai kutishwa na CUF.
Viongozi wa CUF wamedai kuwa polisi waliamua ibaki bendera ya CCM.
Akielezea tukio hilo, Bw. Mrisho Hemed Kisuta amesema, tawi lao la Mchafukoge lilikuwepo toka CUF ianze.
Zama hizo bendera yao waliitundika juu ya mti ambao sasa upo ndani ya uzio wa uwanja wa Mnazi Mmoja.
Amesema, tawi hilo lilihamia livingstone na Mkunguni kwa muda baada ya kuhamishwa na Tume ya Jiji.
Amesema, walivyoona CCM wamerudi na kupandisha bendera, nao wakarudi sehemu yao ya awali.
Amesema, bado suala hilo linashughulikiwa kichama ili bendera yao ipepee.
Bw. Iddi Omar, mkereketwa wa CCM anadaiwa kupeleka
mashitaka polisi kwamba katishwa baada ya mzozo huo hakupatikana kuzungumzia
suala hili.
Na Mwandishi Wetu
WALIOKUWA mara yao ya kwanza hawakuamini macho yao.
Haikuwapitia akilini waliyokuwa wakiona, yametokea Tanzania.
"Hii Soweto, yule Fodae Sankoh?" alihoji na kushangaa Bwana mmoja aliyekuwa amesimama jirani na mwandishi wa habari hizi.
Mshangao huo ulikuja baada ya kuona watu kadhaa wakiuliwa kwa risasi katika mauaji ya Mwembechai.
Hiyo ilikuwa Jumapili usiku katika Msikiti wa Mtambani ambapo ilifanyika kumbukumbu ya mauaji hayo.
Maelfu ya Waislamu waliohudhuria walishindwa kujizuia pale waliposikia na kuona amri ya 'piga yule' ikitekelezwa na kumwacha Ustadh Swaleh akiwa amelalia dimbi la damu.
Kwikwi na vilio vya chini chini vilisikika kila mahali.
Viongozi wa Waislamu waliohudhuria hafla hiyo walitoa nasaha mbalimbali.
Amir Sheikh Juma Mbukuzi amesema, wanachokifanya ni kuwahamasisha waumini wajiandikishe kwa wingi na washiriki uchaguzi.
Amesema, hatarajii waumini wawachague watu wanaowakandamiza.
Sheikh Mbukuzi alitoa tahadhari kuwa, serikali lazima iheshimu kura za wananchi.
Akiongea katika hafla hiyo, Sheikh Omar Bashir amesema, huu si wakati wa kusema sana bali kutenda.
Amesema, watu watembee mikoani kuwaelimisha watu juu ya dhulma inayotendeka.
Sheikh Omar ameifananisha CCM sawa na mke aliyeshindikana, anayestahili talaka tatu zisizo na kurejea.
Sheikh Yusuf Omar, yeye aliwafananisha viongozi wa CCM sawa na Maquraish waliokuwa wakiwatesa watu kwa ajili ya imani na rangi zao.
Alisema, dhulma hiyo iliondoka baada ya wananchi kusimama imara kutetea haki.
Aliwataka Waislamu wapambane na Maquraysh wa leo.
Juni 4, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ziliandaa hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya Mwembechai.
Waislamu kadhaa waliuliwa baada ya polisi kuvamia Msikiti huo Februari 1998.
Uvamizi huo ulitokana na serikali kufanyia kazi shinikizo la Paroko Camillus Lwambano.
Paroko huyo alidai Waislamu wanamtukana Yesu na akaitaka serikali ichukue hatua.
Kufuatia mauaji hayo, Waislamu wamekuwa wakidai iundwe Tume ya uchunguzi na walioua wafikishwe mahakamani.
Rais alidai kuwa, serikali yake ni ya uadilifu na yenye kufuata sheria.
Katika suala la kuuliwa Waislamu Mwembechai, ni
vigumu kuona uadilifu na sheria inavyofuatwa, bila suala hili kufika mahakamani.
Ulipuaji
Ubalozi wa Marekani:
Wamarekani wamuachia Tanzania
yamshikilia
VYOMBO vya dola vya Tanzania vimedaiwa kuendelea kumshikilia mtuhumiwa Rashid Saleh Hemed ambaye uchunguzi wa shirika la upelelezi la FBI umemuachia huru katika kesi ya ulipuaji wa mabomu balozi za Marekani Dar es Salaam na Nairobi.
Kwa mujibu wa barua ya jamaa wa mtuhumiwa huyo iliyoandikwa Mei 26 mwaka huu kwenda kwa mkurugenzi wa mashitaka(DPP) nchini, FBI baada ya uchunguzi wake, mnamo mwezi mei mwaka jana ilivitaarifu vyombo vya dola nchini kuondolewa kwa bwana Rashid katika orodha ya watuhumiwa.
Barua hiyo imedai uthibitisho wa kuachiwa kwa mtuhumiwa huyo ulitolewa na afisa wa kitengo maalum cha FBI bwana W.T. Corbett mbele ya mwambata wa kisiasa wa ubalozi wa Marekani nchini Kenya Dk. Luciene Vandenbrouke mnamo Mei 20 mwaka huu katika Klabu ya Mombasa.
"Inashangaza kwa nini vyombo vya dola vya Tanzania viendelee kumshikilia mtu aliyeonekana hana hatia. Kuendelea kuwekwa kizuizini kwa bwana Rashid kunaonesha jinsi vyombo vya Dola vya Tanzania vilivyoipokea minong'ono kwamba waislamu walihusika moja kwa moja na ulipuaji wa balozi hizo", imedai barua hiyo iliyosainiwa na katibu wa muda wa IPK(Islamic Party of Kenya) bwana Ahmed M. Awadh.
Barua hiyo ANNUUR ina nakala yake imenakiliwa pia kwa Baraza la Maimamu na wahubiri mjini Mombasa, Tume ya haki za binaadamu Tanzania, Amnesty International makao makuu Uingereza na baraza la Bakwata Tanzania.
Gazeti hili lilipowasiliana kwa njia ya simu na Mwenyekiti wa Kamati maalum(Task Force) iliyoundwa kuchunguza chanzo cha milipuko hiyo hapa nchini bwana Adadi Rajab, alithibitisha kuendelea kushikiliwa kwa mtuhumiwa huyo, hata hivyo alisema si FBI inayomuona mtuhumiwa ana hatia au hana bali ni vyombo vya hapa nchini vinavyoshughulikia suala hilo kwa mujibu wa sheria za hapa.
"DPP amemuona mtuhumiwa ana shitaka la kujibu ndiyo maana amefunguliwa mashitaka mahakama kuu", alisema bwana Adadi ambaye pia ni mkurugenzi wa upelelezi wa jinai nchini.
Milipuko ya mabomu katika balozi za Marekani na Nairobi ilitokea Ijumaa ya agosti 7, 1998.
Zaidi ya watu 258 waliripotiwa kuuawa katika milipuko hiyo ambapo jijini Dar es Salaam idadi ya waliokufa ilikuwa 10 na Nairobi watu 248.
Kufuatia tukio hilo oparesheni ya usakaji watuhumiwa iliendeshwa dhidi ya watu waliokuwa na asili ya kiarabu wakidaiwa kuwa na mahusiano na Mwanaharakati maarufu wa kiislamu Duniani Usama Bin Laden ambaye anadaiwa kuandaa ulipuaji huo.
Katika oparesheni hiyo watu 14 waliokuwa na uraia wa nchi za Sudan, Iraq, Somalia na Uturuki walikamatwa wakidaiwa kuhusika na tukio hilo ambapo mmoja aliachiliwa baadaye baada ya kugundulika alikuwa mfanyakazi wa shirika moja la kimataifa lililokuwa na kituo chake mkoani Kigoma.
Mnamo agosti 21 Marekani ilizipiga mabomu nchi za Sudan na Afghanistani ikizituhumu kuhusika na magaidi ambao waliodaiwa kuhusika na milipuko hiyo.
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
Kutoa
maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza
hapa
Au
Andika barua
kwa: webmaster@islamtz.org
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |