USHAURI NASAHA:

Kipindi kisiwepo iwapo hatujui thamani yake

Na Abu Dhar

NCHI inaelekea kwenye uchaguzi mkuu utakaotupa Rais na Wabunge.

Kwa katiba na mfumo wetu wa serikali, Rais wetu si kama Malkia wa Uingereza au kama Rais wa Israel.

Ni Rais mtendaji na Amiri Jeshi Mkuu.

Anapochaguliwa, anapewa nguvu zote za dola azitumie kuongoza nchi kwa miaka mitano.

Bunge letu pamoja na makeke yake haliwezi kumdhibiti Rais. Pamoja na hayo, yeye peke yke ni nusu ya Bunge.

Mamlaka yake yanatenza nguvu umoja wa kikabila, dini, vyama vya siasa, wafanyabiashara, wakulima na wasomi.

Akishachaguliwa hakuna anayethubutu kuzipiga kumbo sheria za serikali yake kwani huo utakuwa ni uasi.

Kwa hiyo kumchagua Rais sio sawa na kumchagua kiongozi wa Club ya mpira au kiongozi wa wacheza ngoma.

Ni wananchi wangapi wanaojua Urais maana yake nini! Wangapi wanajua umuhimu wa demokrasia ya uchaguzi! Je, wote wanajua thamani ya kura yao!

Hawako wanaouza kura yao kwa kikombe cha chai au kilo ya mchele!

Je, wale wanaoambulia kukaribishwa kula chakula cha hadhi, ikawa ndio thamani ya kura yao! Lakini wasiishie hapo wakachacharika kuwarubuni na wengine.

Wako wanaodhani zoezi la kupiga kura halina maana yoyote. Na hata ikiwemo wao haiwashughulishi. Wengine wachague tu huko. Wao huhangaikia yao binafsi.

Lakini wako wanaodai kupiga kura ni ukafiri. Madhali yeyote atakayechaguliwa hataongoza kwa kufuata Qur'an na Sunnah, wanasoma aya na hadithi.

Lakini hiki ni kipindi ambacho hafla na shughuli za kusherehekea uzawa wa Mtume (s.a.w.) zinaanza.

Hafla hizi pengine zitaendelea mpaka wakati wa zoezi la kupiga kura.

Mtume (s.a.w.) huyu anayesherehekewa uzawa wake anasemaje juu ya uongozi. Mafundisho yake yanasemaje juu ya demokrasia ya kupiga kura.

Katika jamii kama yetu ya mchanganyiko, Waislamu waishije. Je, wajitenge? Wasishiriki kupiga kura? Na kama hawakupiga, Rais atakayechaguliwa wamtii? Wamuasi?

Kama kupiga kura ni haramu, je kulipa kodi, kutafuta tasjila na kufuata sheria za serikali usiyotaka kuichagua.

Mtume anasema nini? Uislamu unasema nini. Haya ni masuala ambayo waumini wangetaka ufafanuzi. Si wote wanaoyajua kwa usahihi wake na ziko fikra nyingi.

Yahitaji weledi wa Qur'an, Hadith, historia ya Uislamu na wachambuzi wa fikra mbalimbali za wasomi wa Kiislamu wa zama mbalimbali.

Haya ndiyo Masheikh wenye majuba yao wanatakiwa wawaelimishe Waislamu.

Wanapopata fursa kwenye Televisheni ya Taifa (TvT) kila Ijumaa wajue shida ya watazamaji sio kujua: Nini maana ya Mtume, kazaliwa lini na wapi. Hayo hata wasiokwenda madrasa wanajua.

Kurusha kipindi hewani iwe kwa radio au Televisheni ni ghali sana. Ni mamilioni ya shilingi kwa saa.

Unapopewa fursa kwenda hewani, maana yake una mamilioni ya watu wanakusikiliza na kukutizama.

Watu hawa, hawatarajii somo la watoto wa 'Ibtidaiya' ndio waletewe kwenye TvT.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook